HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 18, 2024

RAS RUVUMA AIPONGEZA HALMASHAURI YA WILAYA TUNDURU KWA KUPATA HATI SAFI KWA MIAKA MITANO MFULULIZO

 

Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Rehema Madenge,akizungumza na baadhi ya watumishi na madiwani wa Halmashauri ya wilaya Tunduru kwenye kikao maalum cha kujadili Taarifa ya CAG yaliyotolewa kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma Said Bwanali kulia,akimuongoza Katibu Tawala mkoa wa Ruvuma Rehema Madenge kuingia ukumbini kwa ajili ya kuzungumza na watumishi kwenye kikao maalum cha Baraza la madiwani cha kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali(CAG)kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Madiwani wa Halmashauri hiyo wakiwa kwenye kikao cha Baraza.
 Baadhi ya Wakuu wa idara katika Halmashauri ya wilaya Tunduru,wakimsikiliza Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Rehema Madenge(hayupo pichani)kwenye kikao maalum cha Baraza la madiwani kwa ajili ya kujadili Taaarifa ya Mkuguzi na mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Na Mwandishi wetu, Tunduru
KATIBU Tawala wa mkoa wa Ruvuma Bi Rehema Madenge,ameipongeza Halmashauri ya wilaya Tunduru kwa kupata hati safi kwa miaka mitano mfululilzo.

Madenge ametoa pongezi hizo jana wakati akizungumza na baadhi ya watumishi na madiwani ,katika kikao maalum cha kujadili taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) katika Halmashauri ya Tunduru

Aidha katika kikao hicho Madenge alisema, Halmashauri zote nane za mkoa wa Ruvuma,zimefanikiwa kupata hati safi kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha ulioisha Tarehe 30 Juni 2023.

Madenge alisema,kwa mwaka wa fedha 2021/2022) hoja zilibaki 217 kati ya hizo 140 zimefungwa na 77 hazijafungwa na kwa mwaka 2022/2023 ulioisha tarehe 30 Juni 2023,kulikuwa na hoja 245 ambapo hoja 125 zimefungwa na 120 hazijafungwa.

“kwa ujumla katika mkoa wetu wa Ruvuma,hoja za nyuma na hoja za mwaka huu ambazo tunakwenda kuzijadili zimebaki 197 na Halmashauri ya wilaya Tunduru hoja za nyuma zimebaki 5 na hoja za mwaka huu zimebaki 9 hivyo kuwa na hoja 14 ambazo bado hazijafungwa”alisema Madenge.

Amezitaka mamlaka ya nidhamu kuchukua hatua za kinidhmu kwa mujibu wa sheria, kwa watumishi waliosababisha kuibuka kwa hoja za ukaguzi wa Hesabu za serikali katika Halmashauri zao na taarifa juu ya hatua hizo zipelekwe ofisini kwake.

Alisema,wapo watumishi waliofanya madudu katika idara zao hivyo wanapaswa kuchukuliwa hatua kwani kuwaachia hakutasaidia kufutika kwa hoja na kusisitiza kuwa, waliosababisha hoja ni lazima watafutwe popote walipo ili warudi kujibu hoja walizoziibua.

Aidha Madenge,ameziagiza Halmashauri zenye viporo vya hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, kuhakikisha zinafunga hoja zote zilizobaki ifikapo tarehe 30 Novemba mwaka huu.

“hoja zote zilizo ndani ya uwezo katika mkoa huo zisijitokeza tena kwa kuwa Halmashauri zina mfumo unaojumuisha kanuni,sheria na taratibu, hivyo mambo hayo lazima yasimamiwe kikamilifu”alisema Madenge.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Simon Chacha,ametaka kila mmoja kwenye nafasi yake kuzingatia sheria,kanuni na taratibu za utumishi wa umma wanapotekeleza shughuli za maendeleo ili kuepuka kuzalisha hoja kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Chacha alisema,fedha zote zinazokusanywa ni lazima zitumike kwa kufuata utaratibu ili ziweze kuwafikia wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo wanayoishi.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Chiza Marando alisema,pamoja na kupata hati safi Halmashauri hiyo ilikuwa na hoja za ukaguzi ambazo zilishajibiwa na kuwasilishwa ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa ajili ya kupata maoni na mapendekezo ya CAG.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Said Bwanali alisema,lengo la Halmashauri ni kuhakikisha kuwa hoja zote zilizobaki zinatafutiwa majibu na kuzifuta ili zisijirudie tena.

Bwanali,amehaidi Halmashauri hiyo kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Katibu Tawala wa mkoa ili kuhakikisha wanaendelea kupata hati safi kwa mwaka ujao wa fedha 2023/2024.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad