HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 4, 2024

NAIBU KATIBU WA TUME ATOA WITO KAMATI ZA MAADILI KUKUTANA

 

Na Mwandishi Wetu, Kiteto Manyara
NAIBU Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu) Alesia Alex Mbuya ametoa wito kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama kufanya vikao vya kamati hizo kwa kuwa vikao hivyo viko kwa mujibu wa Sheria.

Akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Wilaya ya Kiteto leo Julai 4, 2024 mjini Kibaya, Alesia amesema Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye Kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo ambapo Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya ni mojawapo.

Amesema kukutana kwa wajumbe wa Kamati mara nne kwa mwaka kama ilivyopangwa kutasaidia Kamati kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kutoa haki kwa wakati.

Amefafanua kuwa endapo Kamati itakuwa na shauri la kushughulikia haina budi kulikamilisha ndani ya siku 90 zilizowekwa kisheria na endapo kutakuwa na haja ya kuongeza muda, Jaji Mfawidhi ataongeza siku zisizozidi 30.


Aidha, Naibu Katibu Alesia pia amesisisitiza umuhimu wa wajumbe wa Kamati kula viapo kabla ya kuanza kushughulikia mashauri ya kinidhamu.

”Kwa upande wa mashahidi wa shauri, hawa wanapaswa kula kiapo mbele ya Kamati”, amesisitiza.

Kuhusu nyaraka zinazotumika katika kutekeleza kazi za Kamati za Maadili, Alesia amesema ni muhimu kwa wenyeviti wa kamati hizo kukabidhiana nyaraka pale kunapotokea uhamisho ili kuwe na muendelezo wa utekelezaji wa majukumu ya kamati hizo.

Naye Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Kiteto Fadhili Dedan Alexander amesema elimu waliyopatiwa na Tume kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Kamati za Maadili itawasaidia wajumbe kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kwa usahihi.

Ameongeza kuwa ziara ya Watumishi wa Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama Wilayani Kiteto itazihuisha Kamati hizo.

Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya inaundwa na wajumbe wafuatao; Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati, Katibu Tawala wa wilaya (Katibu), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, wajumbe wawili walioteuliwa na Mkuu wa Wilaya na Maafisa Mahakama wawili wanaoteuliwa na Jaji Mfawidhi.

Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye Kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.

Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad