HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, June 30, 2024

ZAIDI YA WANANCHI 2000 WA KIJIJI CHA BUGANDO WILAYANI MAGU WANUFAIKA NA UJENZI WA ZAHANATI

Na Yusuph Digossi- Magu DC

Zaidi ya wananchi 2000 wa Kijiji cha Bugando na vijiji vya jirani kata ya Chabula Wilayani Magu wameanza kunufaika na mradi wa ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Bugando iliyojengwa na mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF) kwa kushirikiana na wananchi ambao wamechangia asilimia 10 ya mchango wa jamii.

Zahanati hiyo imejengwa na TASAF kwa gharama za shilingi milioni 93 imekamilika ikiwa na vifaa vyote pamoja na dawa. Hata hivyo miundombinu mingine ya kuboresha utoaji wa huduma inaendelea kukamilishwa ikiwemo nyumba ya kuishi watumishi wa afya wa zahanati hiyo ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 95 huku ujenzi wa wodi ya wazazi nayo ikiendelea kujengwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zahanati hiyo iliyozinduliwa na Mbunge wa Jimbo la Magu Mhe. Boniventura Kiswaga, Mwenyekiti wa Kijiji cha Bugando, Charles Methusela Kasuka amesema Kukamilika kwa zahanati hiyo kutawaondelea adha ya kutembea umbali mrefu kufata huduma za afya katika kata za jirani.

" Tunaishukuru sana Serikali kupitia TASAF kwa kutujengea zahanati hii kwasababu kilikua ni kilio chetu cha muda mrefu, wananchi walikua wanatembea umbali mrefu kufata huduma za afya hasa akina mama na watoto. hivyo tunashukuru sana serikali kwa kutujengea zahanati hii amesema".

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Magu Mhe. Boniventura Kiswaga ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya ya Magu ikiwemo ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Bugando.

Amesema serikali ya awamu ya sita itaendelea kuboresha sekta ya afya kwa kuendelea kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na ununuzi wa vifaa tiba ili kuendelea kupeleka huduma za afya kwa wananchi kuanzia ngazi za chini.

Kwa upande wake Kaimu Mganga mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Magu, Eusebius Chanjali amewataka wananchi wa Kijiji cha Bugando kutumia zahanati hiyo kutatua changamoto za kiafya huku akiwaomba kutoa ushirikiano wa watumishi wa zahanati hiyo ili watekeleze majukumu yao ya kuwahudumia wananchi bila changamoto yoyote.

Naye Mratibu wa mfuko wa maendeleo ya jamii ( TASAF) Wilaya ya Magu , Daniel Samwel Sanyenge amesema serikali imejenga zahanati hiyo kutokana na uhitaji mkubwa uliyopo kwa wakazi wa maeneo hayo ambao wanatembea umbali huo mrefu kwenda Kata jirani kufata huduma za afya.

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Magu ndugu Mohamed Ramadhani amewaomba wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika ujenzi na ulinzi wa miradi inayojengwa na serikali ili ilite tija iliyokusudiwa ya kutoa huduma.

Muonekano wa zahanati ya Kijiji cha Bugando Kata ya Chabula Wilayani Magu yenye thamani ya shilingi milioni 93 iliyojengwa na mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF) kwa kushirikiana na wananchi ambao wamechangia  asilimia  10 ya mchango wa jamii.
Muonekano wa nyumba ya kuishi watumishi wa zahanati ya kijiji cha Bugando ambayo imekamilika kwa zaidi ya asilimia 98.
Mbunge wa jimbo la Magu Mh. Boniventura Kiswaga (aliyevaa koti jeusi) akikagua ujenzi wa nyumba ya watumishi wa zahanati ya Kijiji cha Bugando kabla ya kuzindua zahanati hiyo iliyonjengwa na TASAF kwa kushirikiana na wananchi.
Mbunge wa jimbo la Magu Mh. Boniventura Kiswaga akizungumza wakati wa uzinduzi wa zahanati ya Kijiji cha Bugando Kata ya Chabula Wilayani Magu.
Baadhi ya wananchi walioshiriki katika uzinduzi wa zahanati ya Kijiji cha Bugando Kata ya Chabula Wilayani Magu Jumamosi Juni 29, 2024.
No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad