HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, June 1, 2024

WAZIRI MKUU AMWAKILISHA RAIS DKT SAMIA MAZIKO YA MAMA WA JAJI MKUU


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo Juni Mosi, 2024 amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Bibi Amina Nyanda Juma ambaye ni Mama mzazi wa Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma yaliyofanyika Tarime mkoani Mara.


Akitoa salamu za Rais Dkt. Samia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wanafamilia, ndugu na waombolezaji kuyaenzi mema yote aliyoyafanya marehemu kipindi cha uhai wake. “Pia tumuombe Mwenyezi Mungu awape moyo wa subra na uvumilivu wanafamilia katika kipindi hiki cha huzuni.”

Kwa upande wake, Profesa Ibrahim Juma ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali pamoja, watendaji wa Mahakama, madaktari pamoja na wakazi wa Tarime kwa ushirikiano waliowapa katika kipindi cha kumuuguza mama yao hadi alipofariki.

Awali, akitoa salam za Wizara ya Katiba na Sheria, Naibu Waziri Jumanne Sagini amesema kuwa Wizara imeguswa na msiba huo na inaunhana na waombolezaji wote kufuatia msiba wa mzazi wa Jaji Mkuu “Tunatoa pole kwa Jaji Mkuu, Familia nzima, tumeguswa wote na tumefiwa wote.”

Marehemu Bibi Amina alizaliwa katika kijiji cha Misungwi mkoani Mwanza Julai 1, 1935, ambapo mwaka 1954 alifunga ndoa na Mzee Juma Hamisi mjini Musoma mkoani Mara na alijaaliwa kupata watoto 11 kati yao tisa wako hai. Pia Bibi Amina ameacha wajukuu 30, vitukuu 17 na kilembwe mmoja.

Wakati wa uhai wake Bibi alipenda kuhudumu msikitini na alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa kiislamu wa wilaya ya Tarime kuanzia mwaka 1980 hadi mwaka 1988.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad