HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 27, 2024

WANANCHI NYASA WAISHUKURU TANROADS KUANZA MATENGENEZO YA BARABARA YA UNYONI-LIPARAMBA-MKENDA

 

Wahandisi kutoka wakala wa barabara Tanzania(TANROADS)) Mkoa wa Ruvuma Peter Ndalemya kushoto na Juma Mkela wakikagua ujenzi wa Reli katika barabara ya Unyoni-Liparamba-Mkenda ambayo baadhi ya maeneo ya barabara hiyo imeharibika kutokana na mvua za masika. wakikagua ujenzi wa Reli kwenye eneo la mwinuko ili kurahisisha usafiri na usafirishaji.
Muonekano wa barabara ya Unyoni-Liparamba-Mkenda inayofanyiwa matengenezo baada ya kuharibika na mvua za masika.
kazi ya matengenezo ya barabara hiyo ikiendelea.
Wahandisi kutoka wakala wa barabara Tanzania(TANROADS)) Mkoa wa Ruvuma Peter Ndalemya kulia na Juma Mkela,wakiwasikiliza baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kingerikiti wilayani Nyasa kuhusiana na matengenezo ya barabara ya Unyoni-Liparamba-Mkenda yanayofanyika ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.


Na Mwandishi wetu, Nyasa
BAADHI ya wananchi wa vijiji vinavyopitiwa na barabara ya Unyoni –Liparamba hadi Mkenda mpakani mwa Tanzania na Msumbuji wilaya ya Nyasa ,wameishukuru Serikali kupitia wakala wa barabara Tanzania(TANROADS)kwa kuanza ujenzi wa barabara hiyo ambayo miundombinu yake imeharibiwa vibaya na mvua za masika.

Leonald Kawonga mkazi wa Liparamba amesema,wakati wa masika barabara hiyo ilikuwa changamoto kubwa kutokana na utelezi na magari kukwama,hivyo matengenezo hayo yatawezesha kupitika kirahisi na kutumika kwa ajili ya usafiri na usafirishaji wa mazao kutoka mashambani kwenda sokoni.

Lenatha Haule,ameishukuru TANROADS kwa uamuzi wa kufanya matengenezo barabara hiyo,kwani katika kipindi chote cha masika baadhi ya shughuli nyingi za kujiingizia kipato zilisimama kutokana na kukosekana kwa mawasiliano ya uhakika.

Alisema,barabara hiyo ilikuwa haipitiki kirahisi baada ya kuharibika vibaya na mvua zilizonyesha kwa wingi hasa katika wilaya ya Nyasa,hivyo kusababisha baadhi ya maeneo ya barabara kukatika na wananchi hao kutokuwa na uhakika wa mawasiliano pindi wanapotaka kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Mkazi wa kijiji cha Kingerikiti Zawadi Nyondo amesema, barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kwa sababu ndiyo inayotengeneza mapato makubwa katika wilaya ya Nyasa kutokana na ukanda huo kuwa yenye uzalishaji mkubwa wa mazao hasa Kahawa,mahindi na maharage.

“barabara hii ni tegemeo kubwa kiuchumi kwetu sisi wananchi wa wilaya ya Nyasa na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla,lakini miundombinu yake bado ni dhaifu,tunaiomba serikali ione namna ya kuijenga kwa kiwango cha lami badala ya kuendelea kufanya matengenezo mwaka hadi mwaka kwa kiwango cha changarawe”alisema.

Kwa mujibu wa Nyondo,barabara hiyo ilipochukuliwa na TANROADS zaidi ya miaka kumi iliyopita walikuwa na matumaini makubwa kwamba itejengwa kwa kiwango cha lami ili kuwaondolea adha hasa wakati wa masika,lakini hadi sasa bado ya changarawe na wanaendelea kuteseka kutokana na ubovu wake.

Mkazi wa kijiji cha Lumeme Timoth Mapunda,ameiomba serikali kupitia TANROADS kutengeneza upya baadhi ya madaraja yaliyopo kwenye barabara hiyo ili kuruhusu maji kupita chini ya madaraja,badala ya juu ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea kwa watu kusombwa na maji.

Kwa upande wake Mhandisi kutoka ofisi ya meneja wa TANROADS mkoa wa Ruvuma Peter Ndalemya,ametaja kazi zinazofanyika ni pamoja na upanuzi wa barabara hiyo ili ipitie kirahisi na kujenga reli kwa baadhi ya maeneo yenye miinuko.

Alisema,lengo ni kuruhusu magari kupita kirahisi zaidi na wananchi waendelea kuitumia barabara hiyo kwenye shughuli zao za kiuchumi ikiwemo kusafirisha bidhaa mbalimbali hasa mazao kwenda kwa wanunuzi.

Ametaja kazi nyingine zinazofanyika ni ujenzi wa makalavati mapya,kufyeka nyasi na matengenezo ya kawaida ambayo yatawezesha barabara hiyo kurudi katika hali yake ya awali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad