HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 6, 2024

WAKAZI WA KIJIJI CHA KITANDA NA LUMECHA WAOMBA KUFUNGULIWA KWA BARABARA YA LUMECHA- LONDO

Mfanyakazi wa wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS)Mkoa wa Ruvuma Hassan Gawaza,akisafisha sehemu ya Barabara ya Lumecha-Londo hadi Kilosa kwa Mpepo jana inayounganisha mkoa wa Ruvuma na Morogoro,waliosimama kushoto ni wasimamizi wa Barabara hiyo kutoka Ofisi ya meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma.
Muonekano wa daraja lililojengwa katika mto Londo linalounganisha wilaya ya Namtumbo mkoa wa Ruvuma na Kilosa mkoa wa Morogoro.


Na Mwandishi wetu, Namtumbo
WANANCHI wa kijiji cha Kitanda na Lumecha wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,wameiomba Serikali kuharakisha mpango wake wa kuifungua Barabara ya Lumecha-Londo hadi Kilosa kwa Mpepo inayounganisha mkoa wa Ruvuma na Morogoro.

Wamesema,kama serikali itafungua barabara hiyo na kuijenga kwa lami itachochea maendeleo na kukuza uchumiwao na vijiji mbalimbali vitakavyopitiwa na barabara hiyo.

Wamesema,barabara hiyo itarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji na kutoa fursa za kibiashara kati ya wananchi wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma na Kilosa mkoa jirani wa Morogoro.

Shadida Ndangwala mkazi wa kijiji cha Kitanda alisema,barabara hiyo itakapotobolewa na kujengwa kwa lami itawezesha kusafirisha mazao yanayolimwa kwa wingi wilayani Namtumbo kwenda maeneo mbalimbali hapa nchini kama mkoa wa Dodoma,Manyara na Arusha yenye mahitaji makubwa ya chakula.

Aidha amesema,itakuwa rahisi kwa wenzao kutoka mkoa wa Morogoro kuleta bidhaa mbalimbali ikiwemo samaki wanaopatikana kwa wingi Kilosa kuja wilaya ya Namtumbo na wilaya nyingine za mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya kuuza.

“sisi Namtumbo tunalima sana mahindi,ufuta na mbaazi tukitaka kupeleka Dodoma,Dar es slaam na mikoa mingine ya Kaskazini ni lazima tupite Njombe na Iringa,barabara hii ikifunguka itapunguza sana gharama na muda wa kuwepo barabarani kwani hapa ni karibu sana”alisema.

George Nungu alisema,barabara hiyo ni muhimu kwao hivyo ameiomba serikali isaidie kuijenga ili watu wanaotoka Songea ambao kwa sasa wanalazimika kuzunguka hadi Iringa kuelekea Dar es slaam wapiti Kitanda na kuingia mkoa wa Morogoro na kuendelea na safari yao.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kitanda Joseph Ngonyani alisema,barabara hiyo imeanza kuzungumziwa tangu mwaka 1974 kuwa itajengwa kwa kiwango cha lami,lakini hadi sasa yapata miaka 50 haijajengwa na wananchi wanaendelea kuteseka kutokana na kutumia gharama kubwa kila wanapohitaji kwenda makao makuu ya nchi Dodoma au Dar es slaam.

Ameitaka Serikali kupitia wizara ya ujenzi,kuhakikisha inatafuta fedha za kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili waweze kuitumia katika shughuli zao za kiuchumi, kusafiri na kusafirisha mazao wanazolima kutoka mashambani kupeleka sokoni.

Kelvin John mkazi wa kijiji cha Lumecha alisema,barabara hiyo ikijengwa kwa lami hata gharama ya usafiri kutoka Songea kwenda mikoa mingine hapa nchini itakuwa ndogo kutokana na umbali ikilinganishwa na sasa ambapo wanalazimika kuzunguka hadi mikoa ya Mtwara,Lindi na Pwani kufika Dar es slaam kwa upande wa kusini na Njombe,Makambako na Iringa.

Mwakilishi kutoka ofisi ya meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mariam Kibaga alisema,TANROADS Mkoa wa Ruvuma imeshaanza kuifungua barabara hiyo kwa kujenga daraja kubwa katika mto Londo linalounganisha mkoa wa Ruvuma na Morogoro.

Alitaja faida zitakazopatikana iwapo barabara hiyo itafunguliwa ni pamoja na kurahisisha shughuli za usafiri, kiuchumi na kijamii kati ya wananchi wa mikoa hiyo miwili.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad