HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 14, 2024

TIC yasaini mikataba na kampuni tatu kuendeleza Jiji la Kilimo Mkulazi, Ngerengere

 

Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amewataka wawekezaji waliopewa kuwekeza kwenye eneo la Mkulazi, mkoani Morogoro kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ajira na vibarua kwa wakazi wanaozunguka eneo la uwekezaji Mkulazi kwa kuwa kufanya hivyo kutajenga msingi wa ushirikiano kwa jamii inayozunguka mradi huo

Waziri Bashe ameyasema hayo leo mjini Dodoma wakati wa hafla ya kusaini mikataba mitatu (3) ya makabidhiano ya utekelezaji wa uendelezaji wa jiji la Kilimo Mkulazi, Ngerengere, mkoani Morogoro ambapo TIC (Kituo cha Uwekezaji nchini) kimesaini mikataba hiyo na makampuni ya TFP (The Food Platform), Longping Agriscience na Eagle Hills.

Amesema uzoefu unaonesha kuwa wawekezaji wanaotekeleza shughuli zao bila kuonesha ushirikiano na jamii inayozunguka eneo la uwekezaji wamekuwa wakipata wakati mgumu hasa linapokuja suala la ulinzi na usalama wa eneo hilo.


Aidha, katika hafla hiyo iliyofanyika Dodoma City Hotel, jijini Dodoma Waziri Bashe amesema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mara zote imekuwa mstari wa mbele katika kuwalinda wawekezaji, hata hivyo inataka kuona wawekezaji wanatengeneza mazingira rafiki yatakayosaidia jamii wanayowekeza inanufaika kiuchumi kutokana na uwekezaji wao.

Naye Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida amesema mradi wa utekelezaji wa uendelezaji wa jiji la Kilimo Mkulazi, uliopo Mkulazi, Ngerengere, mkoani Morogoro utafungua fursa lukuki kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kwa namna moja au nyingine kwa kuwa viwanda vitakavyowekwa eneo hilo vitajikita kwenye sekta hizo za kiuchumi

Dkt. Kida amesema mashamba hayo yamekodishwa kwa wawekezaji na TIC ikiwa ni sehemu ya kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya biashara na uwekezaji, ambapo licha ya wakulima, wafugaji na wavuvi kunufaika na uwekezaji huo lakini pia wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za serikali na zisizokuwa za serikali watapata fursa ya kujifunza kuhusu kilimo na ufugaji wa kisasa kwenye eneo hilo

Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Dkt. Binilith Mahenge amesema uwekezaji huo unakuja ikiwa ni sehemu ya matokeo ya uvutiaji wawekezaji na kuwekwa kwa mazingira rafiki kwao kutoka kwa serikali ya awamu ya sita (6) inayoongoza na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan

Amesema TIC imekuwa ikifanikisha miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo kutoka sekta ya kilimo, hivyo baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo hatua inayofuata ni kwa TIC kuhakikisha uwekezaji uliokusudiwa unafikiwa.


Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Gilead Teri (kulia) akibadilishana nyaraka na mwekezaji wa kampuni ya Foodplatform, Ibrahim Qammar mara baada ya kusaini makubaliano ya uendelezaji kilimo Mkulazi mkoani Morogoro. Wakiwa kwenye picha ya pamoja na mawaziri waliohudhuria hafla hiyo jana jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad