Mwenyekiti wa Chama Cha Watu wenye Ualbino Tanzania TASS ,Godson Mollel akizungumza katika kongamano hilo.
Na Khadija Kalili, Michuzi Tv
WATU wenye Ulemavu wa Ngozi Ualbino nchini wameiomba serikali kuwawekea nazingira ya usalama wao katika kuelekea kipindi cha Uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu ujao 2025.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Watu Wenye Ualbino (TASS),
Godson Mollel
katika leo Juni 12 katika Kongamano la Uelewa kuhusu Ualbino ambao kilele chake ni kitafanyika kesho Juni 13.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani Nickson Simon amewatoa hofu Chama Cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) kwamba serikali itahakikisha inakomesha vitendo vya mauaji kwa watu wenye changamoto ya ngozi (Albino).
"Serikali iko kazini katika kuzuia mauaji ya Albino nchini na kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakari Kunenge ambaye amenituma nije kumuwakilisha katika Kongamano hili leo nasema kuwa vitendo hivi vitakomeshwa kabisa endapo tu tutatumia njia ya kupeana elimu kwani tunaimani kubwa endapo jamii wakipata ufahamu wa kutosha kwamba vitendo vya mauaji ya Albino ni kinyume na haki za binadamu na kwamba watu wote tuna haki ya kuishi kwa misingi ya utu,undugu na amani mauaji haya yatakoma.
"Kitakwimu inaonesha kuwa kati ya watu 20,000 mtu mmoja anavinasaba vya Ualbino , kati ya watu1,400 mmoja kati yao ni Albino huku ndani ya Mkoa wa Pwani kuna watu 569 huku watu 368 ambao wanahudhuria Kliniki na wanapata misaada mbalimbali inayowahusu.
DC Nickson amesema hayo leo wakati alipokuwa mgeni rasmi akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani katika Kongamano la Uelewa kuhusu Ualbino linalofanyika kwenye Ukumbi wa mikutano wa Shule ya Siasa ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kwamfipa Kibaha Mkoani Pwani.
" Elimu zaidi inahitajika kwa jamii kuhusu kukwepa unyanyapaa dhidi ya watu wenye ualbino na mauaji yatakoma pindi tu jamii itakapokuwa na uelewa wa kutosha juu ya changamoto ya watu wenye Ualbino" amesema DC Simon.
Aidha Mwenyekiti wa TASS Godson Mollel ameiomba Mahakama kutôa adhabu kali kwa watu wanaokutwa na hatia ya kuwakata viungo au kuwaua watu wenye Ualbino.
Mwenyekiti wa Taifa wa TAS Godson Mollel alipozungumza na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho ya kitaifa ya siku kuongeza uelewa juu ya Ualbino (IAAD) duniani.
Mollel amesema kuwa Mahakama ikitoa hukumu kali kwa wahusika wa mauaji ya Albino itakuwa fundisho kwa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha kuwadhuru.
Mkurugenzi wa Kitengo Cha Huduma kwa watu Wenye Ulemavu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu Rasheed Maftah amesema kwamba serikali inaadaa sera na miongozo mbalimbali kwa watu wenye ulemavu ili kuweka usawa.
Wakati huohuo Ofisa Ustawi Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Watu wenye ulemavu Joy Maongezi amesema kuwa sheria namba 9 ya mwaka 2010 inataka kuwa na haki kwa watu wenye ulemavu ambapo watu wenye Ualbino ni sehemu yao.
Katika maadhimisho hayo huduma mbalimbali zimetolewa ikiwa ni pamoja na upimaji saratani ya ngozi, utoaji miwani, kofia na mafuta maalumu ya kuzuia ngozi kutoathirika na mionzi ya jua , upimaji wa tezi dume na kansa ya mlango wa shingo ya kizazi.
Maadhimisho hayo hufikia kilele kila ifikapo Juni 13 dunia kote na kwa mwaka huu kitaifa yamefanyika Kibaha Mkoani Pwani.
No comments:
Post a Comment