HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 7, 2024

PURA yashiriki hotuba ya bajeti Zanzibar

Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeshiriki kama mgeni mwalikwa katika wasilisho la hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kwa mwaka 2024/2025.

Wasilisho hilo ndani ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar limefanywa Juni 07, 2024 na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mhe. Shaaban Ali Othman

Katika hotuba yake, Mhe. Shaaban alieleza kuwa kwa mwaka 2024/25 Wizara itatekeleza vipaumbele kumi na mbili ikiwemo kuendelea na utafutaji wa mafuta na gesi asilia.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2024/25 Wizara itaendelea na zoezi la kuvitangaza vitalu vinane (8) vilivyopo Mashariki mwa bahari ya Zanzibar kupitia majukwaa mbalimbali na kukaribisha wawekezaji kwa ajili ya shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia na kusimamia utekelezaji wake” alieleza Mhe. Shaaban.

Pamoja na kueleza mipango kwa mwaka 2024/25, Waziri alieleza kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika mwaka 2023/24.

Miongoni mwa mafanikio hayo kwa upande wa mafuta na gesi asilia ni pamoja na uzinduzi wa duru ya kwanza ya utoaji wa vitalu vya mafuta na gesi asilia Zanzibar na malipo ya fidia kwa wananchi 3,575 walioathiriwa mali zao wakati wa zoezi la uchukuaji wa data za mitetemo.

Ili kutekeleza kazi zilizopangwa kwa mwaka 2024/25, Mhe. Waziri aliomba Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuidhinisha matumizi ya Shilingi 66,012,766,000 kwa ajili ya kazi za kawaida na miradi ya maendeleo ya Wizara.

PURA, ikiwa miongoni mwa Taasisi za Wizara ya Nishati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyoingia hati ya Mashirikiano na Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta Zanzibar (ZPRA) ilialikwa kushiriki tukio hilo muhimu.

PURA na ZPRA zilisaini Hati ya Mashirikiano tarehe 19 Februari, 2022 kwa lengo la kubadilisha uzoefu katika maeneo mbalimbali yakiwemo uandaaji wa kanuni za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia na kujengeana uwezo katika ukaguzi wa mikataba ya ugawanaji wa mapato yatokayo na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia.

Maeneo mengine ni kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa taarifa za mafuta na gesi asilia, na kujengewa uwezo kwa taasisi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad