HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 25, 2024

KUBORESHA MPAKA KATI YA ZAMBIA NA TANZANIA KUDHIBITI UTOROSHWAJI WA BIDHAA

 


Na Chedaiwe Msuya, WF, Dodoma
NAIBU Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) amesema katika kudhibiti utoroshwaji wa mazao na bidhaa nchini Serikali imeboresha mpaka kati ya Tanzania na Zambia ambapo Mamlaka ya Mapato (TRA) na Mamlaka ya Mapato Zambia (ZRA) ziliingia makubaliano (MoU) yenye lengo la kuchukua hatua mbalimbali za kulinda utoroshwaji huo.


Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Mhe. Condester Sichalwe (MOMBA), aliyetaka kujua ni lini Serikali itaboresha mpaka ya zambia na Tanzania ili kudhibiti njia za panya ambazo mazao na bidhaa hutoroshwa bila kulipiwa kodi.


Mhe. Chande, alisema ZRA na TRA zimeingia makubaliano ya kuboresha mfumo wa uondoshaji mizigo TANCIS ambapo umeunganishwa na mfumo wa ASYCUDA World wa Zambia ili kubadilishana taarifa na kurahisisha taratibu za uondoshaji mizigo.


"Serikali pia imesimika midaki (baggage and cargo scanners) za kukagua mizigo inayobebwa na abiria pamoja na magari",Alisema Mhe. Chande


Aidha, aliongeza kuwa Serikali ya Zambia pia inapanua barabara na eneo la maegesho ya upande wa Nakonde ili kupunguza msongamano upande wa Tunduma.


Pia,alisema kuwa Serikali inaendelea kubainisha vihatarishi vilivyopo katika magari ya mizigo yanayopita mpaka wa Tanzania na Zambia.


Sambamba na hayo, Mhe. Chande alisema pamoja na hatua hizo kuchukuliwa pia Serikali kupitia TRA inaendelea kuimarisha doria kwa ajili ya kudhibiti maeneo yote ya mpaka wa Tanzania na Zambia kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kulinda mapato ya serikali.


MWISHO


Caption


PIX 1


Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akijibu swali la Mbunge wa Mhe. Condester Sichalwe (MOMBA), bungeni jijini Dodoma.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Dodoma)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad