HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, June 3, 2024

DKT MWIGULU, WAZIRI AWESO NA MBUNGE CHEREHANI WASHUHUDIA UTIAJI SAINI MRADI WA MAJI ZIWA VICTORIA WA BIL 44 - USHETU

Na Mathias Canal, Ushetu-Kahama

Waziri wa Fedha Mhe Dkt Mwigulu Nchemba, Waziri wa Maji Mhe Juma Aweso na Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe Emmanuel Cherehani wameshuhudia utiaji saini mradi mkubwa wa Bilioni 44 wa maji ya ziwa Victoria.

Hafla ya utiaji saini kandarasi ya ujenzi wa mradi wa usambazaji maji ya ziwa Victoria kutoka Manispaa ya Kahama kwenda Halmashauri ya Ushetu umefanyika leo tarehe 2 Juni 2024 katika viwanja vya shule ya msingi Kangeme iliyopo kata ya Ulowa Halmashauri ya Ushetu mkoa wa Shinyanga.

Mkataba huo umesainiwa kati ya serikali ya Tanzania na Mkandarasi Kampuni ya Sihotech Engineering Company Limited kwa kushirikiana na kampuni ya MPONELA Construction and Company Limited awamu ya kwanza ni miezi 24, kuanzia Julai 2024 hadi Juni 2026.

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Fedha Mhe Dkt Mwigulu Nchemba amesema kuwa hakuna mbadala wa maji hivyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan ameendelea kuongeza Bajeti ili kuimarisha sekta ya maji kote nchini.

Amesema kuwa Mradi huo wa maji ya Ziwa Victoria katika Halmashauri ya Ushetu utachochea maendeleo ya Halmashauri kwa kutoa fursa mbalimbali kwa Wananchi ikiwemo Wananchi kupata muda mwingi wa kufanya shughuli za kiuchumi kama vile kilimo na ufugaji.

Dkt Mwigulu amesema kuwa pia mradi huo utasaidia kuimarisha afya za Wananchi kwa kupunguza magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo safi na salama kama vile kipindupindu.

Akizungumza na wananchi, Waziri Aweso amesema kuwa katika kuhakikisha serikali inamtua mama ndoo kichwani na kutambua adhima ya Serikali chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini kwa kushirikiana na Mamlaka za Maji (KASHWASA, KUWASA na SHUWASA) imefanya na kukamilisha usanifu wa mradi huo, ambapo ujenzi wake utahusisha ujenzi wa miundombinu ya majisafi na salama.

Waziri Aweso amesema kuwa taratibu za kupata Mkandarasi kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi zimefanyika na kukamilika na sasa utekelezaji wa mradi unakwenda kuanza baada ya tukio la kusaini Mkataba na utekelezaji wake utafanywa na Kampuni ya Sihotech Engineering Company Limited kwa gharama ya Tsh. Bilioni 44.

Ameitaja Miradi itakayohusika katika programu hiyo kuwa ni pamoja na Ujenzi wa kilomita 76 za bomba kuu kutoka Manispaa ya Kahama kwenda hadi Ulowa kwenye matanki ya maji lenye kipenyo cha ukubwa wa kuanzia mm.350 hadi mm.100, Ujenzi wa kilomita 74 za mabomba kwenye mtandao wa kusambaza maji yenye ukubwa wa mm. 160, 110, 90, 75, 63, 50, 40, na 32, Ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji la lita 500,000 katika eneo la Ulowa Na.2, Ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji la lita 300,000 katika eneo la Ulowa Na.4.

Ameitaja miradi mingine kuwa ni Ujenzi wa tanki la kihifadhia maji la lita 100,000 katika eneo la Ulowa Na.1, Ujenzi wa vituo 35 vya kuchotea maji (DPs), Ununuzi wa vifaa kwa ajili ya kuunganishia wateja 1,000 wa majumbani, Ujenzi wa jengo la ofisi litakalotumiwa na Chombo cha Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO),

Ujenzi wa jengo kwa ajili ya kutibu maji, Ununuzi wa Magari mawili (2) aina Toyota hardtop na Double cabin kwa ajili ya usimamizi na ufuatilaiji wa mradi, Ununuzi wa Pikipiki 2 kwa ajili ya usimamizi na ufuatilaiji wa mradi Ununuzi wa sanduku la vitendea kazi (Tool box), na Ununuzi wa mashine ya kuunganishia bomba za HDPE Ukubwa wa kuanzia milimita 40 hadi milimita 200.

Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe Emmanuel Cherehani amesema kuwa kwa ujumla mradi huo utahudumia watu takribani 189,836 wa kata za Igunda, Kisuke, Kinamapula, Nyamilangano, Mapamba, Uyogo, Bukomela, Ushetu na Ulowa.

Dkt Cherehani ameeleeza kuwa kwa awamu hii ya kwanza mradi unakwenda kuhudumia watu takribani 28,568 wa Kata ya Ulowa na baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huo pamoja na miradi mingine inayoendelea kutekelezwa kwa sasa, idadi ya watu wanaopata huduma ya majisafi na salama itaongezeka kutoka asilimia 47.3 ya sasa hadi kufikia asilimia 81.6 katika Halmashauri ya Ushetu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad