HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 22, 2024

Znz Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani Kufanyika Alhamis Mei 23, 2024 Ukumbi wa ZSSF KARIAKOO

 


KAMATI ya maandalizi ya siku ya uhuru wa habari duniani Zanzibar imeeleza kuwa maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari duniani yanategemewa kufanyika Alhamis tarehe 23 Mei, 2024 katika ukumbi wa ZSSF KARIAKOO kuanzia saa 2.30 asubuhi.

Maadhimisho hayo pia yatahudhuriwa pamoja na waandishi wa habari, wadau mbali mbali wa habari pamoja na wawakilishi kutoka asasi za Kiraia hapa Zanzibar.

Makamo mwenyekiti wa kamati hiyo DK. Mzuri Issa amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamebeba ujumbe muhimu na adhimu ambao ni “UHURU WA VYOMBO VYA HABARI NA MAGEUZI YA SERA NA SHERIA ZA HABARI ZANZIBAR. ”

Maadhimisho hayo ni muhimu katika kukuza na kuimarisha kada ya habari hapa nchini pamoja na kutoa wito maalum kwa wadau wa habari kuhusu umuhimu wa kuwa na Sera na Sheria rafiki zitakazowezesha utendaji kazi wa vyombo vya habari kuwa na ufanisi. Pia shughuli hiyo itaambatana na majadiliano katika mada mbali mbali zenye lengo la kuimarisha na kukuza kada ya habari hapa nchini.

Maadhimisho ya mwaka huu yatatanguliwa na shughuli za kukuza na kuimarisha kada ya habari ikiwemo kuandaa vipindi vya masuala ya uhuru wa habari pamoja na mikutano na mafunzo kwa waandishi wa habari katika masuala ya sheria za habari.

“Nia ya shughuli hizo ni kukuza weledi na umahiri wa waandishi wa habari katika masuala ya sheria za habari ili watumie kalamu zao katika kufanya uchechemuzi wa sheria hizo.

Kutakuwa na mijadala inayohusu mafanikio na changamoto, wapi tunatoka na upi mwelekeo wa kukuza na kuimarisha kada ya habari hasa ikizingatiwa umuhimu wa sekta ya habari katika kuleta maendeleo na kuibua kero za wananchi.

Alisema kuwa waandishi wa habari ni kada muhimu katika kukuza na kuendeleza demokrasia, uwazi na uwajibikaji hivyo waandishi hao hawana budi kuwa na sheria nzuri za habari ili ziweze kuwalinda katika kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu.

Vile vile suala la kuwa na sheria nzuri za habari hapa nchini pia litajadiliwa katika mjadala huo ambalo muda mrefu limekuwa likizungumzwa na wadau mbali mbali wa habari ambapo hadi hivi sasa kuna Sheria ya Usajili wa Mawakala wa Habari, Magazeti na Vitabu No. 5 ya 1988 na marekebisho yake mwaka 1997, na sharia ya Tume ya Utangazaji No 7 YA mwaka 1997 na marekebisho yake ya mwaka 2010.

Suala la kuwa na sheria mpya na nzuri ya habari limekuwa katika mchakato na hatua mbali mbali zimekuwa zikichukuliwa katika kukusanya maoni ya wadau hivyo Mswada huo umeshirikisha fikra na maoni tofauti.

Aidha masuala ya jinsia na vyombo vya habari yatakuwa na nafasi ya kipekee ikiwa ni sehemu muhimu ya kuimarisha masuala ya jinsia katika vyombo vya habari ili haki na usawa katika vyombo vya habari iweze kuimarishwa.

Kamati ya maadhimisho ya kuandaa siku ya uhuru wa habari hapa Zanzibar inaundwa na taasisi zifuatazo:

Baraza la habari Tanzania Ofisi ya Zanzibar (MCT ZNZ), Chama cha Waandshi wa Habari Tanzania Zanzibar (TAMWA,ZNZ)
Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo (WAHAMAZA) na Klabu ya Waandishi wa Wabari Zanzibar (ZPC)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad