HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 20, 2024

Ushirikiano wa CCM ,CPC ni Fursa kwa Zanzibar Kutangaza Sekta ya Utalii Kimataifa

 


NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt. Mohamed Said Dimwa, kuimarika kwa uhusiano wa kisiasa na kiuchumi baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Kikomunisti cha China(CPC) ni fursa kwa Zanzibar kutangaza sekta ya utalii kimataifa.

Hayo ameyasema wakati akizungumza na ujumbe maalum kutoka Chama Cha CPC huko Ofisini kwake Kisiwandui Unguja.

Alisema Zanzibar ni nchi ya visiwa ambayo uchumi wake utategemea zaidi sekta ya utalii hivyo ni muhimu kwa nchi ya China kuleta raia wake nchini kwa ajili ya kufanya utalii na uwekezaji katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

Dkt.Dimwa, alieleza kuwa CCM inathamini na kutambua mchango wa Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC) katika masuala mbali mbali ya kimaendeleo yanayotekelezwa na nchi hiyo kwa dhamira ya kuunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.

Alieleza kuwa nchi ya China imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika nyanja za kiuchumi,kijamii,kisiasa,kidiplomasia na kiteknolojia hatua ambazo ni fursa ya kujifunza kwa lengo la kupata maarifa na ujuzi kutoka kwa taifa hilo.

Katika maelezo yake Dkt.Dimwa, amefafanua kuwa kwa upande wa diplomasia kisiasa CCM inathamini na kupongeza juhudi za CPC katika utoaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watendaji na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi.

“Uhusiano wa kisiasa na kijamii kati ya CCM na CPC umeendelea kuimarika kutokana na misingi imara iliyoasisiwa na waasisi wa Vyama vyetu ambao ni aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume pamoja na muasisi wa Chama cha Kikomunisti cha China Mao Zedong.

Zanzibar ilipofanya Mapinduzi mwaka 1964 nchi ya kwanza kutambua mapinduzi hayo ilikuwa ni China hivyo tunajivunia urafiki na undugu wetu kwani busara,falsafa na mipango endelevu ya kimaendeleo iliyowekwa na viongozi hao ndio chachu ya ukuaji na ustawi wa vyama vyetu.”, alisema Dkt. Dimwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Uhusiano wa Kimataifa wa Kamati Kuu ya CPC Rao Huihua, amesema Chama hicho kimejipanga kuimarisha ushirikiano wa kisiasa baina yake na Chama Cha Mapinduzi.

Ameeleza kuwa CPC kupitia wataalamu wake wa vyuo vikuu wataendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji wa CCM kulingana na mahitaji yao ya kitaaluma na kisiasa.

Pamoja na hayo alisema lengo la ziara hiyo ni kutembelea taasisi mbali mbali za CCM nchini ili kujifunza na kubadilishana uzoefu wa masualas ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni.

Rao Huihua, alifafanua Tanzania na Zanzibar kwa ujumla kuna vivutio vingi vya utalii vinavyotakiwa kupewa kipaumbele katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad