HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 2, 2024

RUFAA NYINGINE EQUITY BANK (T) NA EQUITY BANK (K) ZASHINDWA KUENDELEA

 

Na Mwandishi Wetu
MAHAKAMA ya Rufani imeshindwa kuendelea na usikilizaji wa rufaa nyingine ya Equity Bank (T) Limited na Equity Bank (K) Limited dhidi ya kampuni mbili za Tanzania zinazobishania malipo ya mkopo wa Dola za Marekani 16,275,000 kutokana na kasoro kwenye hukumu inayikatiwa rufaa.

Benki hizo zimekata rufaa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, zikipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyozipa ushindi kampuni za za Nas Hauliers Limited, Everest Freight Limited na Tanga Petroleum, katika kesi ya madai iliyofunguliwa na kampuni hizi dhidi ya benki hizo kuhusu mggoro wa malipo ya mkopo huo.

Rufaa hiyo ilikuwa imepangwa kusikilizwa juzi Jumanne na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, linaloongoza na Jaji Rehema Mkuye, akishirikiana na Jaji Abraham Mwampashi na Jaji Zainabu Muruke.

Lakini ilishindwa kuendelea na usikilizaji wa rufaa hiyo baad aya kubaini kuwa kuna tofauti kati ya wadaawa wanaotajwa kwenye hukumu inayokatiwa rufaa, na notisi ya rufaa na hati ya sababu za rufaa zilizowasilishwa mahakamani.

Mahakama ilibainisha kuwa waliokuwa notisi ya rufaa na ile ya sababu za rufaa zinaonesha kuwa wakata rufaa ni wawili yaani benki hizo za Equity na wajibu rufaa ni 11.

Hata hivyo kwenye hukumu inayokatiwa rufaa wadai walikuwa watatu yaani kampuni hizo, ambazo ni miongoni mwa wajibu rufaa kwenye notisi ya rufaa na ya sababu za rufaa.

Kwa hiyo mahakama hiyo ilisema kuwa kwenye notisi ya rufaa na ile ya sababu za rufaa kuna wadaawa ambao wameongezeka ambao kwenye hukumu inayokatiwa rufaa hawapo na ikawahoji mawakili wa pande zote kama notisi hiyo ya rufaa na ya sababu za rufaa ziko sawa kuwepo mahakamani.

Wadaawa hao wanaoonekana kuongezeka kwenye notisi ya rufaa na ya sababu za rufaa ni baadhi ya wakurugenzi wa kampuni hizo wanane, ambao waliingizwa kwenye kesi hiyo na benki hizo zilipofungua madai kinzani dhidi ya madai ya awali ya kampuni hizo, ambao nao walijumuishwa kama wadaiwa kwenye madai kinzani ya benki hizo.

Mawakili wanaozitetea benki za Equity, ambao ni Mpaya Kamara na Timon Vitalis walikiri kuwapo kwa tofauti hiyo lakini wakasema kuwa wadaawa hao wametajwa ndani ya hukumu hiyo kuanzia ukrasa wa 45 na 59 wa hukumu.

Wakili Kamara alidai kuwa hukumu hiyo imeleeza kuwa benki hizo zilifungua madai kinzani dhidi ya kampuni hizo tatu zilizofungua kesi ya msingi; pamoja na wengine wanane zaidi, yaani wakurugenzi hao wa kampuni hizo.

Hivyo Kamara alidai kuwa notisi hiyo ya rufaa na hati ya sababu za rufaa hazina kasoro ila kama ni kasoro basi itakuwa kwenye hukumu kwam kutokuwajata juu kabisa wadaawa hao walioongezeka, lakini akadai kuwa hiyo kasoro ndogo ambayo haiathiri haki za upande wowote kwani haliendi kwenye mzizi wa kesi

“Hivyo tunaomba mahakama iione kama ni kasoro ya kawaida na isiizingatie lakini kama mahakama ikiona ni kasoro basi ielekeze hukumu hiyo irejeshwe kufanyiwa marekebisho hayo na iletwe iliyofanyiwa marekebisho”, alisema Kamara.

Wakili anayezitetea kampuni hizo ambazo ndio wajibu rufaa pamoja na wakurugenzi wake, Frank Mwalongo naye alidai kuwa kwa kuwa wadaawa hao (wakurugenzi), wametajwa ndani ya hukumu hiyo, hivyo naye haoni kama kuna shida.

“Kwa kuwa wametajwa ndani ya hukumu kwangu sioni tatizo, inatosha tu kwamba hukumu imewataja ndani", alidai Wakili Mwalongo, naye akifafanua kuwa hakuna upande unaolalamika kuathirika na kasoro hiyo.

Hata hivyo Mahakama baada ya kusikiliza hoja za mawakili wote iliiahirisha ikieleza kuwa italitolea uamuzi hoja hiyo kwa tarehe ambayo wadaawa watataarifiwa.

Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa Mei 22, 2019 kampuni hizo ziliingia makubaliano na Equity Bank ya Kenya ya ili kuzitolea hati ya udhamini wa mkopo wa Dola 16,275,000 (Letter of Credit , LC); kutoka kampuni ya Lamar Commodity Trading DMCC ya Uarabuni ya Dubai kupitia Numora Trading PTE Limited.

Kampuni hizo pia zilitoa hati za mali zake mbalimbali kama dhamana ya kudhaminiwa kupata mkopo huo ambazo zilitunzwa na Equity Tanzania kama wakala wa Equity Kenya.

Kampuni hizo zilishindwa kulipa mkopo huo badala yake Equity Kenya kama mdhamini ikalazimika kuulipa mkopo huo kisha ikazidai kampuni hizo zilipe deni hilo.

Hata hivyo baadaye kampuni hizo zilizifungulia kesi benki za Equity Tanzania na Equity Kenya zikidai zirejeshewe hati za mali zake zilizoziweka kama dhamana ya kudhaminiwa na kupata mkopo huo.

Kampuni hizo pamoja na mambo mengine zilidai kuwa mkopo huo wa Dola 16.27 milioni kutoka Lamar/Numora haukuwa na udhamini wa Equity Kenya kwa madai kuwa hati yake ya udhamini ilikuwa na kasoro.

Pia zilidai kuwa zilishalipa mkopo huo na hivyo benki hizo hazina haki ya kuzidai deni lolote

Kufuatia kesi hiyo, benki hizo nazo zilifungua madai kinzani dhidi ya kampuni hizo na wakurugenzi wake hao zikidai kulipwa pesa hizo ambazo Equity Kenya ilizilipia deni la mkopo baada ya kushindwa kulipa.

Katika kesi hiyo mkurugenzi wa Lamar na pia mwanahisa wa Numora (mkopeshaji) alikuwa miongoni mwa mashahidi na aliieleza mahakama kuwa alizipatia mkopo kampuni hizo kwa udhamini wa Equity Kenya, lakini zilishinda kurejesha mkopo, badala yake mdhamini wao, Equity Kenya ndi akaulipa.

Kata hiyo Mahakama katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Deo Nangela Aprili 19, 2023 ilitupilia mbali madai kinzani ya benki hizo akieleza kuwa zimeshindwa kuthibitisha madai yake na akazipa ushindi kampuni hizo akieleza kuwa zimeweza kuthibitisha madai yake kuwa zilishalipa mkopo huo na benki hazina haki kuzidai.

Jaji Nangela aliaamuru kampuni hizo zirejeshewe hati zake zote za mali zilizokuwa zinashikiliwa na Equity Tanzania dhamana ya mkopo, ndipo benki hizo zikakata rufaa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad