HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 24, 2024

NAMANGA SEC. YAFAIDIKA NA JENGO JIPYA LA BWENI CHINI YA UDHAMINI WA LSF KUPITIA SERIKALI YA LUXEMBURG

Namanga, Tanzania – Mei 23, 2024: Shule ya Sekondari ya Namanga leo imezindua kwa fahari jengo lake jipya la bweni, chini ya ufadhili wa Legal Services Facility (LSF) na North-South Cooperation kutoka Luxemburg. Msaada huu unalenga kuboresha miundombinu ya shule, kuwawezesha wanafunzi, hasa wasichana, kupata haki yao ya kupata elimu bora na kuwapa mazingira salama ya kufikia ndoto zao.

Legal Services Facility (LSF), kwa kushirikiana na North-South Cooperation chini ya ufadhili wa serikali ya Luxemburg, inaendesha mradi unaoitwa "Wanawake Tunaweza." Mradi huu unalenga kuwawezesha wanawake kijamii na kiuchumi kwa kutoa mitaji kwa ajili ya biashara zao, ujuzi, na kuwajengea wa uwezo ili kuimarisha biashara zao. Pia unashughulikia mila potofu zinazowakandamiza wanawake na wasichana na kupambana na ukatili wa kijinsia katika jamii. 

Aidha, mradi huu unalenga kuwawezesha wasichana kutimiza ndoto zao kwa kuboresha miundombinu ya shule, kama vile mabweni ya wasichana, kuhakikisha usalama wao dhidi ya ukatili wa kijinsia wakiwa shuleni, na kukuza uendelevu wa mazingira kwa kupanda miti. Zaidi ya wasichana 240 watanufaika na mabweni mawili mapya yaliyoko katika Shule za Sekondari za Namanga na Lekule huko Longido.

Akiongea wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Lulu Ng'wanakilala alisema, "Leo ni hatua muhimu kwani tunasherehekea kukamilika kwa jengo la bweni na kulikabidhi rasmi kwa Shule ya Sekondari ya Namanga. Tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa serikali ya Luxemburg kupitia North-South Cooperation kwa msaada huu ambao unaenda sambamba na malengo yetu ya kuhakikisha haki na usawa kwa wote ikiwemo haki ya kupata elimu bora. Bweni hili ni ushahidi wa dhamira yetu ya kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya msingi, ikiwemo mazingira mazuri ya kujifunzia. Tutaendelea na jitihada zetu za kusaidia jamii zilizo pembezoni, hususan wanawake na wasichana, huku tukifungua milango ya fursa zisizo na kikomo na hivyo kuleta maendeleo na kuondoa umaskini katika jamii zetu."

Kwa upande wake, Mwanzilishi na Meneja Mkuu wa North-South Cooperation, Roberto Marta, alisema, "Tunafurahia ushirikiano wetu na LSF, ambao umezaa matunda makubwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Leo, Tunafurahi kuona kuwa wasichana wa Kimasai sasa watakuwa na mazingira mazuri ya kusomea. Serikali ya Luxemburg inajivunia kuunga mkono miradi inayoboresha maisha ya kijamii na kiuchumi. Tunaamini kuwa elimu ni msingi wa maendeleo na ustawi, na tumejizatiti kuendelea kuunga mkono miradi inayotoa fursa kwa jamii zilizo pembezoni. Bweni hili ni ushahidi wa maono yetu ya pamoja ya mustakabali bora kwa wanafunzi wote."

Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mheshimiwa Marko Ng'umbi, ambaye pia alikuwa mgeni rasmi, alisema, "Leo ni siku ya kusherehekea na kujivunia kwa jamii ya Longido. Bweni jipya katika Shule ya Sekondari ya Namanga linawakilisha sio tu jengo, bali ni taa ya matumaini na fursa kwa wanafunzi wetu. Ninawashukuru sana Legal Services Facility na North-South Cooperation kwa msaada wao thabiti na kujitolea. Juhudi hii bila shaka itakuwa na alamai ya kudumu katika maisha ya vijana wetu, ikiwapa mazingira wanayohitaji ili kufaulu katika masomo yao na kufikia ndoto zao. Pia tunatambua i ujenzi unaoendelea huko Lekule, ambao ni sehemu ya mradi huu. Hivi karibuni, jengo hilo litakamilika, likiwa ni hatua nyingine muhimu katika kuboresha miundombinu ya elimu katika jamii yetu. Nawahimiza wanafunzi na walimu kulinda bweni hili jipya, wakilitunza vyema ili liweze kuendelea kuhudumia vizazi vijavyo vya wanafunzi."

Mkurugenzi Mtendaji wa LSF Bi Lulu Ng'wanakilala akiwa na Mwakilishi kutoka North and South Cooperation Bw. Roberto Marta wakikata utepe kuashiria Ufunguzi wa jengo jipya la Bweni ya Shule ya Sekondari Namanga, Akishuhudia ni Diwani wa Kati ya Longido Bi. Pendo Ndorosi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad