HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 30, 2024

NAIBU WAZIRI PINDA ATAKA UTUNZAJI HATI MILIKI ZA ARDHI KUEPUKA UDANGANYIFU

Na Munir Shemweta, MLELE

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amewataka wananchi wanaokabidhiwa hati Milki za ardhi kuhakikisha wanazitunza ili kuepuka udanganyifu unaoweza kufanyika kutoka watu wasio waaminifu.

Mhe. Pinda ametoa kauli hiyo tarehe 29 Mei 2024 wakati wa hafla ya uzinduzi wa wiki ya Mazingira iliyoambatana na ugawaji hati za Hakimiliki za Kimila za ardhi, Daftari la Usajili wa Wamiliki wa ardhi la Kijiji na Vyeti vya Kijiji iliyofanyika kata ya Kasansa halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.

Katika hafla hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Suleiman Jafo jumla ya Hati za Hakimiliki za Ardhi za kimila 30 kati 4450 zilizoandaliwa kupitia mradi wa urejeshwaji endelevu wa mazingira na uhifadhi wa Bioanuai Tanzania (SLR) unaosimamiwa na ofisi ya Makamu wa Rais zilitolewa.

Mhe. Pinda ambaye ni Mbunge wa jimbo la Kavuu kupitia mkutano wa hadhara amewatahadharisha wananchi kuwa, hati milki za ardhi ni nyaraka na mali ambayo haipaswi kabisa kuazimishwa kwa mtu yeyote ili akachukulie mkopo benki bila kujua utaratibu wa namna ya kurejesha mkopo.

‘’Hii hati haiazimwi kama tunavyoazimana nguo, lakini ni mali na umsimgawie jirani hata mtoto wako ili aende akakopee bila kuwa na mpangilio maalum atarudijshaje, maana mwisho wa siku benki haitamuangalie aliyekopa itaangalia kielelezo, mtakuja kunyanganywa mali kwa maana ya mashamba au nyumba, kazitunzeni’’. Alisema Mhe. Pinda

Amefafanua kuwa, iwapo mwananchi atashindwa kuzitunza hati milki ya ardhi basi anaweza kuipeleka masijala za ofisi za serikali kama vile ofisi ya mkuu wa wilaya au mkurugenzi wa halmashauri aliowaeleza kuwa wamepewa muelekewa wa namna ya kutunza kumbukumbu ili wakati wa kutumia ukifika waweze kwenda kuiomba.

Aidha, kupitia hafla hiyo, Naibu Waziri wa Ardhi Mhe. Pinda ameiomba ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) kupitia Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Uhifadhi wa Bioanuai Tanzania (SLR) kufadhili pia vijiji vingine vilivyopo kata za Mamba, Majimoto, Mbede, Usevya pamoja na Kibaoni katika halmashauri ya Mpimbwe ili kutunza mazingira sambamba na kuimarisha biashara ya hewa ya ukaa kwa lengo la kuleta manufaa kwenye vijiji vya kata hizo.

Kwa upande wake Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Suleiman Jafo ameipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Tume ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kufanikisha uandaaji wa Mipango ya matumizi ya ardhi na hatimaye kuandaa hati miliki za kimila 4,450.

‘’Hili ni jambo kubwa sana kufanikisha hati 4,450 ambalo ni jambio kubwa sana na hapa peke yake ni hati 1,046 ni faraja kubwa sana katika mradi huuu tuneona changamoto kubwa hasa watu wanaokosa hati za ardhi kupitia mradi huu tumeona mafanikio makubwa sana katika mustakabali wa maendeleo ya nchi’’ amesema Mhe, Jafo.

Mhe, Jafo amesema, ofisi yake itatoa ushirikiano katika juhudi zozote za uhifadhi mazingira kwenye halmashauri ya Mpimbwe na mkoa mzima wa Katavi ili kuleta manufaa kwa mkoa na wananchi ikiwemo uvunaji hewa ya ukaa katika vijiji husika.

Kilele cha wiki ya mazingira kinachoambatana na shughuli mbalimbali nchini kama vile uwepo wa Kongamano pamoja na shughuli za kufanya usafi kitafanyika kitaifa mkoa wa Dodoma na kimataifa kitafanyika jiji la Riadh nchini Saudia Arabia.
Waziri wan chi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Suleiman Jafo akizindua mradi wa Josho, Banio na Birika la kunyweshea mifugo katika mradi wa urejeshwaji endelevu wa mazingira na uhifadhi wa Bioanuai Tanzania (SLR) unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais katika kata ya Kasansa halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi tarehe 29 Mei 2024. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Suleiman Jafo akimnawisha maji Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda mara baada ya kupanda mti wakati wa uzinduzi wa wiki ya Mazingira katika kata ya Kasansa halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi tarehe 29 Mei 2024.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Suleiman Jafo na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda wakikabidhi Daftari la Usajili wa Wamiliki wa ardhi la Kijiji kwa viongozi wa kijiji wakati wa uzinduzi wa wiki ya Mazingira katika kata ya Kasansa halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi tarehe 29 Mei 2024.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Suleiman Jafo akikabidhi ya hati ya Hakimiliki ya pamoja (Mume na Mke) kwa mwenyekiti wa halmashauri ya Mpi
mbwe Silas Ilumba na mke wake wakati wa uzinduzi wa wiki ya Mazingira katika kata ya Kasansa halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi tarehe 29 Mei 2024.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Suleiman Jafo na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda pamoja na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na wananchi waliokabidhiwa hati ya Hakimiliki za kimila wakati wa uzinduzi wa wiki ya Mazingira katika kata ya Kasansa halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi tarehe 29 Mei 2024.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Suleiman Jafo na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Pinda wakikabidhi fedha milioni 3 zilizotolewa na Mbunge wa jimbo la Kavuu kwa kikundi cha utunzaji mazingira cha Mkombozi wakati wa uzinduzi wa wiki ya Mazingira katika kata ya Kasansa halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi tarehe 29 Mei 2024.
Sehemu ya wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa wiki ya Mazingira iliyofanyika katika kata ya Kasansa halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi tarehe 29 Mei 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad