HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, May 18, 2024

MKUU WA MKOA WA MWANZA AFANYA ZIARA YA KIKAZI KATIKA MRADI WA UWEKEZAJI WA JENGO LA HOTELI YA NYOTA TANO WA NSSF

-Aeleza matarajio ya Serikali ya awamu ya sita ni kuona miradi  ya kimkakati ukiwemo  hoteli ya nyota tano jijini Mwanza unakamilika
 
Na MWANDISHI WETU,
 
Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda amesema ni azma ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuona miradi ya kimkakati ukiwemo hoteli ya nyota tano inayojengwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) jijini Mwanza inakamilika.

Mhe. Mtanda amesema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipofanya ziara ya kikazi kukagua miradi ya kimkakati.

“Nawapongeza NSSF kwa kazi nzuri na ubunifu mkubwa wa miradi ya kimkakati wanayoitekeleza sehemu mbalimbali nchini, nawaomba waendelee kuongeza  kasi ya utekelezaji ili ile azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona miradi mbalimbali ya kimkakati inakamilika kama ilivyokusudiwa.

Mhe.Mtanda amesema mradi  wa NSSF wa hoteli ya nyota tano wa jijini Mwanza, utakapokamilika utaongeza thamani katika jiji hilo, amewahakikishia  Serikali ya Mkoa  itaendelea kutoa ushirikiano kwa NSSF kuhakikisha mradi huo unakamilika na kuanza kutumika kama ilivyokusudiwa.

Awali, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Kaimu Mkurugenzi wa Uwekezaji, Bw. Mapesi Maagi amesema uwekezaji wa mradi huo ni moja kati ya majukumu manne ya Mfuko ambayo ni kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao. 

Bw. Maagi amesema uwekezaji wa hoteli hiyo utakapokamilika utachochea maendeleo ya Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla kwa kuinua shughuli za kiuchumi hususan utalii hasa ukizingatia kuwa Mkoa wa Mwanza umepakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ipo karibu na mkoa huo.

Naye, Meneja wa NSSF Mkoa wa Mwanza, Bw. Emmanuel Kahensa amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kufanya  ziara hiyo ya kikazi katika mradi huo wa hoteli ya nyota tano.

Akitoa taarifa, Mhandisi Helmes Pantaleo ambaye ni Meneja Miradi wa NSSF ameelezea utekelezaji wa mradi  na changamoto zote ambazo zilikuwa ni kikwazo zimetatuliwa. Mhandisi Pantaleo amesema utekelezaji unaendelea ambapo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu na kuanza kazi mwezi Machi 2025.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad