HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 20, 2024

MAKAMU WA RAIS AHITIMISHA MAADHIMISHO YA SIKU YA NYUKI DUNIANI

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kijiji cha Nyuki cha mkoani Singida Philemon Kiemi kuhusu bidhaa mbalimbali zitokanazo na mazao ya nyuki wakati wa ukaguzi wa mabanda ya maonesho katika Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma tarehe 20 Mei 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma tarehe 20 Mei 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa ufugaji nyuki nchini mara baada ya kuhitimisha Maadhimisho ya ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma tarehe 20 Mei 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akikabidhiwa tuzo na Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki kwaajili ya kutambua mchango wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza sekta ya ufugaji wa nyuki na uhifadhi wa mazingira nchini. Tuzo hiyo imetolewa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma tarehe 20 Mei 2024.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Christopher Kedendula ambao ni wazalishaji wa Asali (Swahili Honey) na watengenezaji wa mitambo ya kuchakata asali wakati wa ukaguzi wa mabanda ya maonesho katika Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma tarehe 20 Mei 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Kamishna wa Uhifadhi Wakala wa Misitu Nchini (TFS) Prof. Dos Santos Silayo kuhusu mizinga ya nyuki ya kisasa wakati wa ukaguzi wa mabanda ya maonesho katika Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma tarehe 20 Mei 2024.

MAKAMU  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa wote wenye dhamana ya kusimamia maeneo yaliohifadhiwa kulinda na kuendeleza ipasavyo maeneo hayo ili yasiharibiwe kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu.

Makamu wa Rais ametoa rai hiyo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma. Amesema Utunzaji wa maeneo hayo ni lazima uende sambamba na utaratibu utakaowezesha wananchi kufuga nyuki na kujipatia kipato huku wakitunza mazingira.

Ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na Wadau katika kutoa elimu kwa wafugaji nyuki ili waweze kufuga kitaalam kwa kutumia vifaa sahihi vitakavyoongeza kiwango cha uzalishaji na ufugaji wa tija.

Makamu wa Rais ameilekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuyatambua na kuyahifadhi kisheria maeneo yote yaliyobaki yenye uoto uliotawaliwa na mimea ya aina mbalimbali inayotoa chakula kwa nyuki hususani katika Mikoa ya Dodoma na Singida. Amesema Uoto huo umetawaliwa na mimea jamii ya Mndarambwe na Mnang’ana ambao unakadiriwa kuwa kwenye eneo lenye ukubwa wa hekta 410,000 na taarifa zilizopo zinaonesha kuwa uoto huo hupatikana katika nchi mbili tu hapa duniani, yaani Tanzania na Zambia, huku sehemu kubwa ya uoto huu ikiwa Tanzania katika mikoa ya Singida na Dodoma. Aidha amesema wananchi waliopo kwenye maeneo hayo waelimishwe kuhusu ufugaji nyuki kibiashara na utunzaji wa mazingira.

Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TFS na Mfuko wa Misitu kuhakikisha wanawawezesha Wananchi hasa wale wanaopakana na maeneo ya hifadhi kwa kuwapatia mafunzo ya ufugaji nyuki pamoja na mizinga ya kisasa ya kufugia nyuki. Pia amesema TAMISEMI inapaswa kuhakikisha kuwa Halmashauri hasa zenye fursa kubwa ya ufugaji nyuki zinaajiri Wataalam wa ufugaji nyuki watakaotumika kwenda kutoa huduma ya ugani kwa wananchi.

Halikadhalika ameziasa Balozi za Tanzania nje ya Nchi kujidhatiti katika kutafuta masoko ya mazao ya nyuki yanayozalishwa nchini ili kuweza kuongeza fedha za kigeni. Amesema Wizara ya Fedha iangalie uwekezano wa kupunguza kodi katika vifaa mbalimbali vya kuchakata mazao ya nyuki kama njia ya kuhamasisha uongezaji thamani ya mazao ya nyuki na kukuza mauzo nje ya nchi.

Aidha Makamu wa Rais amesema Vyuo vya Veta vilivyopo katika maeneo ya vijijini ni muhimu kuwa na programu za ufugaji na uchakaji wa mazao ya nyuki. Ameongeza kwamba Vyuo vya Elimu ya Nyuki na Vyuo Vikuu ni vema kuwatumia wajasiriamali waliofanikiwa katika sekta ya ufugaji nyuki kutoa elimu katika vyuo hivyo ili kuwa hamasa kwa vijana waliopo vyuoni

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki amesema Wizara itaendelea kuongeza ufugaji nyuki na kuhakikisha uzalishaji wa asali unaongezeka kutoka tani 32671 za sasa hadi kufikia uzalishaji usiopungua tani 138000 ifikapo 2034. Amesema Wizara itaongeza uzalishaji wa Chavua, kuhamasisha na kuongeza idadi ya mizinga, kuongeza uzalishaji wa asali ya nyuki wasiodunga, kuongeza thamani ya aina sita za mazao ya nyuki kwa kutumia mazao mengine kama sumu ya nyuki na gundi ya nyuki.

Aidha amesema Wizara itawajengea uwezo wa wataalamu ili waweze kufanya kazi zaidi pamoja na kutenga fedha na kuhakikisha vitendea kazi na miundombinu vinaimarishwa katika maeneo ya kufugia nyuki.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad