HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, April 6, 2024

WAKAZI WA KATA YA MSAMALA WAIOMBA SERIKALI KUFANYA MATENGENEZO YA BARABARA ZA MITAA

 

 Moja kati ya barabara zilizoharibika katika mtaa wa Kiswele kata ya Msamala ambayo inapitika kwa shida baada ya kuharibika na mvua zinazoendelea kunyesha wilayani Songea.
 Maji yakiwa yametuhama katika barabara ya Songea-Njombe karibu na Hoteli ya RM iliyopo katika Msamala kutokana na mifereji ya kupitisha maji kuziba.

Na Mwandishi Maalum. Songea
WAKAZI wa mitaa mitatu ya Osterbay,Miembeni na Kiswele kata ya Msamala Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,wameiomba serikali kupitia wakala wa barabara za mijini na vijijini(Tarura)kufanya matengenezo ya barabara zake ili ziweze kupitika kirahisi.

Walisema,kwa sasa barabara nyingi kwenye maeneo hayo ni mbovu na baadhi ya watu wanalazimika kulipia gharama ya kupaki magari yao kwenye vituo vya mafuta kwa kuwa wanashindwa kufika nayo nyumbani.

Menald Mwanditi mkazi wa mtaa wa Kiswele alisema,katika kipindi hiki ambacho mvua bado zinaendelea kunyesha kwa wingi, hali inakuwa mbaya zaidi hasa maji yanayotoka barabara kuu ya Songea-Makambako iliyoko chini ya wakala wa barabara Tanzania(TANROADS).

Alisema,katika barabara hiyo kuanzia katikakituo cha mafuta Ottawa hadi Chuo cha Top One Inn maji yanapita juu ya barabara na kuelekea upande wa pili ambako kuna makazi ya watu kwa kuwa yanashindwa kupitia kwenye mifereji ambayo imeziba kutokana na kujaa mchanga na takataka mbalimbali.

Kwa mujibu wa Mwanditi,barabara nyingi za mitaa za Tarura kwa sasa zimeharibika na hazipitiki kwa kuwa hazijafanyiwa ukarabati wowote tangu zilipotengenezwa hivyo kuwa na mashimo makubwa yanayojaa maji na kuhatarisha usalama hasa kwa watoto wadogo.

Mkazi wa mtaa wa Osterbay Hamidu Ramadhan alisema,changamoto kubwa katika mtaa huo ni ubovu wa barabara ambazo zimeharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika Mkoa wa Ruvuma.

Hamidu ambaye ni dereva bodaboda alisema,wanakutana na wakati mgumu pale wanapowabeba wateja wao hasa mama wajawazito kuwapeleka kituo cha afya Msamala kwa ajili ya kupata matibabu.

Alisema,wanalazimika kuwashushia njiani badala ya kuwafikisha moja kwa moja kwenye kituo cha kutolea huduma za matibabu kwa sababu ya ubovu wa barabara.

Mkazi wa Msamala Leonald Kapinga alisema,kukosekana kwa mifereji ya kupitisha maji ya mvua katika barabara kuu ya Songea-Makambako ina sababisha mchanga unaosombwa na maji kujaa kwenye makazi yao na hivyo kuingia gharama kubwa ya kuondoa mchanga huo.

Aidha alisema,katika mitaa hiyo kuna wafanyabiashara waliochukua mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha na wanatakiwa kufanya marejesho kila wiki, lakini wanashindwa kurejesha kwa wakati kwa kukosa wateja wanaokwenda kununua bidhaa wanazouza kutokana na ubovu wa barabara.

Ameiomba Tarura na Tanroads mkoani Ruvuma,kufanya matengenezo ya barabara zao ili kuwaondolea adha inayowakabili kwani kuna hatari ya kufunga biashara zao kwa kukosa wateja.

Kaimu meneja wa Tarura wilaya ya Songea Godfey Mngale alisema,kabla ya kilio cha wananchi wa Msamala,tayari serikali kupitia Tarura ilishaanza kuchukua hatua kwa kufanya matengenezo ya barabara katika mitaa hiyo.

Mngale alisema,tatizo lililojitokeza kwa sasa ni Mkandarasi amelazimika kusimamisha kazi kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha,lakini mara mvua zitakapokatika kazi ya matengenezo ya barabara katika maeneo hayo zitaendelea kama kawaida.

Amewatoa hofu wananchi wa Msamala kuhusu ubovu wa barabara na kusisitiza kuwa,serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imejipanga kwa kuhakikisha inaboresha miundombinu ya barabara zote ili kurahisisha usafiri na usafirishaji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad