HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, April 25, 2024

ROMBO MPYA YA KUWEKEZA KWENYE ELIMU - DC MWANGALA

Na Mwandishi wetu, Rombo

MKUU wa wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, Raymond Mwangala amewataka wakazi wa eneo hilo kuwekeza kwenye elimu kwani mataifa mengi yameendelea kutokana na kuwekeza katika elimu.


Mwangala akizungumza kwenye kikao cha tathmini ya elimu ya sekondari na kugawa zawadi kwa wanafunzi waliofaulu vyema kidato cha nne, shule zilizofaulisha na walimu wao amesema Rombo mpya ya maendeleo imezaliwa hivyo jamii iwekeze kwenye elimu.


Amesema hivi sasa wilaya ya Rombo imezaliwa upya ikilenga kutazamwa kwa mtazamo chanja tofauti na awali ilivyozungumzwai na ndiyo sababu eneo la kwanza la Mamsera itawekwa taa za barabarani hadi Mkuu.


"Tunaiona Rombo mpya ya maendeleo, tuna maprofesa wengi nchi nzima wametokea Rombo, kuna madokta, mapadri hata marehemu Gadna G Habash kumbe kwao ni Tarakea na aliyekuwa mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) Ludovick Utouh ametokea Rombo," amesema.


Amesema amelenga kushirikiana na jamii ya Rombo kuwekeza kwenye elimu ili maendeleo yapatikane kwani nchi nyingi zilizoendelea zimewekeza katika elimu.


"Matajiri wengi wa Dar es salaam, Dodoma, Arusha na kwingine wametokea Rombo, tunataka Rombo mpya ya maendeleo, watu waje Rombo kuona utalii wa mtori na ndizi na watu wenye maendeleo," amesema.


Ofisa elimu sekondari wa halmashauri ya wilaya ya Rombo, Silvanus Tairo amesema kikao hicho kitakuwa chachu ya kuongeza ufaulu mzuri kwa wanafunzi kwani wamejipangia mikakati ya kuboresha elimu na kupambana na changamoto zilizopo.


Tairo amewapongeza walimu waliofanikisha wanafunzi 1,700 kupata daraja la kwanza hadi daraja la tatu ambao ndiyo wenye sifa za kuendelea na elimu ya juu na vyuo mbalimbali.


"Lengo ni kufanya tafakuri ya elimu na kuweka mikakati ambayo itatusaidia kufanya vzuri zaidi kwenye mitihani ijayo na pia kuwapa motisha wanafunzi, walimu na shule husika kufanya vyema zaidi," amesema Tairo.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda ambaye pia ni mbunge wa Rombo, akizungumza kwa njia ya simu, amewapongeza walimu kwa namna wanavyojitahidi kunyanyua kiwango cha elimu kwa kuwafundisha wanafunzi.


"Nawaahidi kuwa tutaendelea kushirikiana pamoja walimu wangu ili sekta hii muhimu iweze kuwanufaisha watoto wetu ambao watakuwa na manufaa kwa Taifa," amesema Prof Mkenda.


Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Rombo, Christina Marwa ameipongeza idara ya elimu sekondari kwa ubunifu huo wa kufanya tathimini na kutoa zawadi kwa ufaulu.


"Tumeona jambo hili ni jema mno hivyo mwakani mjipange upya na kulifanya kwani litakuwa na matokeo chanya kutokana na hamasa hii iliyofanyika kwa walimu na wanafunzi," amesema Marwa.


Mmoja kati ya wanafunzi walipatiwa zawadi kwa ufaulu mzuri Deus Mdee wa shule ya sekondari Kelamfua amesema motisha walizopata zitaongeza ari kwa wanafunzi kusoma zaidi na walimu kufundisha kwa moyo wote.


"Nashukuru kwa zawadi ya madaftari kwani lengo langu ni kuwa daktari na sasa nasubiria kupangiwa shule ili niende na masomo ya kidato cha tano," amesema.No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad