HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, April 17, 2024

BAJETI YA TAMISEMI YAWAPA TUMAINI WANAHARAKATI WA JINSIA

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

ONGEZEKO la fedha shilingi Trilioni 10 kwenye bajeti ya Wizara ya Tamisemi imeibua matumaini kwa Wanaharakati wa masuala ya kijinsia ambapo wanatarajia itakwenda kutoa chachu ya kuinua ushiriki wa wanawake katika masuala ya uongozi na kuwaepusha na vitendo vya ukatili, unyanyasaji na kuwaondolea mazingira magumu wakati wa uchaguzi.

Hayo yamesemwa leo April 17,2024 katika Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) ambazo zimekuwa zikifanyika kila Jumatano na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa Jinsia katika viwanja vya TGNP- Mtandao Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa semina, Muwasilishaji Bw.Iddi Mziray amesema wamehoji kuhusiana na urejeshwaji wa mikopo ya asilimia 10 iliyoondolewa mwaka uliopita kutokana na changamoto za marejesho endapo mifumo iliyowekwa na serikali itawasaidia kujibu changamoto za wanawake wa chini ambao ndio walengwa.

"Kulikuwa na changamoto za msimu uliopita kwa wanawake, vijana na walemavu walichukua mikopo bila elimu,je mifumo hii tuliyonayo itakwenda kutatua masuala hayo na ya vikundi hewa". Amesema Mziray.

Aidha Mziray ameeleza kuhusiana na suala la miundombinu ya shule ambapo wanatarajia ongezeko la matundu vyoo pamoja na sehemu za kubadilishia taulo za kike na fedha kwa ajili ya taulo hizo ambapo wameona bajeti haijalizungumzia suala hilo moja kwa moja na tamanio lao ni kutengwa fedha kwa ajili ya masuala hayo.

Kwa Upande wake Mdau wa masuala ya kijinsia Bw.Mophat Mapunda amelipongeza bunge kupitisha Sheria ya unyanyasaji wa kijinsia kama kosa katika uchaguzi,ambapo amedai kuwa katika kanuni za uchaguzi ambazo zinatarajiwa kupitishwa hivi karibuni hazijaonesha namna ambavyo zitampa kipaumbele mwanamke.

Aidha Mapunda ameiomba serikali kuhusiana na fedha iliyotengwa kwa lengo la kutoa elimu ya masuala ya uchaguzi,iwe inakidhi kuwezesha wanawake kushiriki katika zoezi hilo ili kuongeza usawa na kuondoa suala la mfumo dume ambalo limetawala kwa jamii kubwa.

Naye, Mwanaharakati wa Jinsia Bi.Mtumwa Nindi ambaye ni mlemavu ameiomba serikali kuwapatia elimu ili wanufaike na mikopo ya asilimia 10 ambapo ameeleza kuwa mfumo huo wa porto ambao umeundwa kwa ajili ya huduma hiyo hawatambui jinsi.ya kuutumia.

TGNP kupitia semina za Jinsia na Maendeleo imekuwa ikitoa mafunzo kwa Wanaharakati namna yakupambana ili kuwa na bajeti yenye mlengo wa kijinsia ambayo itasaidia kuunda usawa kwa jinsia zote katika masuala ya fursa za uongozi pamoja na mgawanyo wa rasilimali,na umiliki wa Mali.
No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad