HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 25, 2024

Wizara, Drum Beats Zasaini Makubaliano Kuendesha Tamasha la Utamaduni

 


Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nicholas Mkapa (kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Drum Beats Carnival (T) Limited, Selestine Mwesigwa wakisaini mkataba wa ushirikiano kuhusu uendeshaji wa Tamasha la Kitaifa la Utamaduni katika ofisi za wizara hiyo, Mtumba Jijini Dodoma leo Machi 24, 2024 Wengine kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria wa wizara hiyo, Lugano Rwetaka na mratibu,  Aggrey Marealle.

WIZARA ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na kampuni ya Drum Beats Carnival (T) Limited, ya Jijini Dar es Salaam zimesaini makubaliano ya ushirikiano ambapo kampuni hiyo itaratibu Tamasha la Kitaifa la Utamaduni  kwa niaba ya wizara.  

Makubaliano hayo yamesainiwa leo Machi 24, 2024 katika ofisi za wizara Mtumba Jijini Dodoma kati ya Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Nicholas Mkapa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Drum Beats Carnival (T) Limited Selestine Mwesigwa na viongozi waandamizi kutoka pande zote mbili.

Akizungumza baada ya utiaji saini, Mkapa amesema Wizara ina matarajio makubwa kutoka kwa Drum Beats katika kuendesha tamasha hilo ambalo ndio kubwa la kitamaduni Tanzania na kuongeza kuwa huo ni mwanzo mzuri wa kushirikiana na sekta binafsi katika kuendesha matamasha ya wizara na pia kupanua wigo kwa wadau wa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika uendeshaji wa matukio ya kijamii.

“Hii haina maana kuwa serikali imeliachia tamasha hili moja kwa moja bali tunatoa fursa kwa sekta binafsi pia itoe mchango wake na pia kuhakikisha tamasha hili linafanyika kitaalamu zaidi  na linakuwa kubwa lakini serikali itaendelea kusimamia kwa karibu,” amesema.

Aidha, Mkapa ametoa wito kwa watanzania kujitokeza kwa wingi katika hatua zote za tamasha hilo kuanzia hatua za awali hadi ngazi ya kitaifa kwani hili ni tamasha la kitaifa linalolenga kuimarisha utamaduni wa Tanzania.

Naye Mkurugenzi wa Utamaduni wa wizara hiyo. Dkt Mnata Resani amesema tamasha hilo la kitamaduni la kitaifa litafanyika Songea Mkoani Ruvuma kuanzia Agosti 25 hadi 28 huku akisisitiza kuwa ujio wa Drum Beats kushirikiana na wizara ni dalili njema kuwa tukio hilo litakuwa katika viwango vya juu zaidi.

“Kutakuwa na mambo mbalimbali kama vile vyakula vya kitanzania, zana mbalimbali, mavazi na pia kutakuwa na maonyesho barabarani yaani street carnival,” alisema na kuongeza kuwa serikali itafanya kazi kubwa ya kutoa hamasa ili watu wengi zaidi washiriki katika tukio hili kubwa.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Drum Beats Carnival (T) Limited, Bw. Selestine Mwesigwa amesema kampuni yake iko tayari kushirikiana na wizara kuhakikisha tamasha hilo linafanikiwa.

“Timu yetu imekamilika na tuko tayari kushirikiana na wizara kuhakikisha malengo yanafikiwa nap engine kuvukwa,” amesema.

Alisema baada ya utiaji saini, kampuni yake itatoa ratiba nzima ya shughuli zote za tamasha hilo. “Tunatoa wito kwa watanzania watuunge mkono ili kufanikisha jambo hili,” amefafanua.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad