HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 25, 2024

VETA yajipambanua kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi

 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore,Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore akizungumza na wafanyakazi wa VETA kuhusiana na zoezi la upandaji miti katika kuelekea Maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Baadhi ya wafanyakazi wakiwa na miti kwa ajili ya kupanda eneo la Ofisi za Makao Makuu ya VETA


Baadhi ya picha za wafanyakazi wa VETA wakipanda miti kwa ustadi katika eneo la ofisi hiyo.

*Wapanda miti 40,000 kuelekea Maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Na Mwandishi Wetu Dodoma
WATUMISHI wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) nchini wamepanda miti zaidi ya 40,000 ikiwa ni mwitikio wao kuelekea Maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Akizungumza wakati wa zoezi la upandaji miti lililohusisha wafanyakazi wa VETA Makao Makuu, jijini Dodoma, leo tarehe 25 Machi, 2024, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema zoezi hilo limefanyika kwenye vituo vya VETA nchini ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya kila mwananchi na kila taasisi kupanda miti ili kutunza mazingira.

CPA Kasore amewaasa watumishi hao kutunza miti iliyopandwa ili ikue na kuleta maana halisi ya zoezi hilo na pia akawahimiza watumishi kuendelea na zoezi hilo katika maeneo wanayoishi.

“Kupanda miti ni jambo moja na kutunza miti hiyo ni jambo lingine la muhimu sana…Nasisitiza tukatunze miti hii ili ikue na kutupa uhai pamoja na kuboresha muonekano wa mazingira yetu,” amesema.

CPA Kasore ameshukuru Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kutoa miti hiyo bure na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika shughuli mbalimbali za uhifadhi wa misitu na utunzaji mazingira.

Afisa Misitu wa TFS Kanda ya Kati, Jenipha Elius, amesema anaamini miti hiyo itatunzwa na kukua vizuri hasa kwa kuzingatia kuwa imefuata hatua zote muhimu za kitaalamu za upandaji miti.

Amewasihi watumishi wa VETA kujenga utamaduni wa kupanda miti kwenye maeneo wanayoishi na kujipatia faida mbalimbali ikiwemo hali nzuri ya hewa pamoja na matunda na kuwakaribisha kupata miti bure kutoka TFS.

Furaha Paul ni miongoni mwa watumishi wa VETA Makao Makuu walioshiriki zoezi hilo ambaye amesema amejisikia fahari kupanda miti ambayo itanufaisha watanzania wengi kwa miaka mingi ijayo.

“Kwa kweli najisikia furaha kushiriki kwenye zoezi hili la kihistoria kwa kuwa naamini miti hii itatumiwa na sisi, watoto wetu, wajukuu hadi vitukuu vyetu,”amesema

Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kinatarajiwa kuwa tarehe 26 Aprili, 2024.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad