HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, March 23, 2024

KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA HALI YA HEWA, TANZANIA YACHUKUA TAHADHARI KUJIHAMI NA MABADILIKO YA HALI YA HEWA

 


Wanafunzi wa Shule ya Secondary KIA wamepatiwa mafunzo katika kuadhimsha siku ya hali ya hewa duniani, 23/03/2024.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) Dkt. Ladislaus Chang'a.
Waziri wa uchukuzi Profesa Makame Mbarawa.

SERIKALI ya Tanzania imeungana na nchi wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuchukua hatua za kukabiliana na athari mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kwani yameendelea kuathiri utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.

Hayo yameelezwa leo Machi 23, 2024 jijini Dodoma na Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa Katika kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani.

Maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya Hali ya Hewa duniani yamebeba kauli mbiu isemayo 'Kuwa Mstari wa Mbele Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi'.

Prof. Mbarawa amesema kuwa Tanzania ikiwa Mwanachama wa WMO na Umoja wa Mataifa haijabaki nyuma katika kuchukua hatua Madhubuti kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kwani yameendelea kuathiri utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kilimo, ujenzi, utalii, miundombinu, usafirishaji, nishati na afya.

"Mifano ya hivi karibuni ni mvua kubwa zilizochagizwa na uwepo wa El Nino na kusababisha vifo na uharibifu wa miundombinu hasa barabara na nyumba za watu" amesema Prof. Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa ametanabaisha kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada za makusudi kujihami na athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa uboreshaji wa huduma za hali ya hewa na uimarishaji wa mfumo wa utoaji tahadhari nchini.

"Uboreshaji huu pia ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ibara ya 59 ikiweka malengo ya kuimarisha miundombinu na huduma za hali ya hewa nchini kwa lengo hilo la kukabiliana na kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na kuhakikisha usalama wa chakula na afya pamoja na matumizi bora ya vyanzo vya maji",amesema Prof. Mbarawa.

Amesema kuwa Serikali haijaishia kwenye mipango ya kwenye makaratasi tu imewekeza kwenye miundombinu ya hali ya hewa. "Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na ununuzi na ufungaji wa mitambo ya kisasa ya upimaji na uchakataji wa taarifa za hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na kompyuta kubwa ya kisasa na yenye uwezo mkubwa wa kuchakata data za hali ya hewa.

"Kompyuta hii inaiwezesha TMA kuboresha na kuongeza usahihi wa utabiri wa hali ya hewa hususani kwa maeneo madogomadogo, ambapo huduma hiyo imeshaanza kutolewa hadi ngazi ya wilaya kwa utabiri wa mvua za msimu", amesema Prof. Mbarawa.

Amesema kuwa serikali iko hatua za mwisho kukamilisha mtandao wa jumla ya Rada saba za hali ya hewa, ambapo katika kipidi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita, malengo ya ununuzi wa Rada nne yamefikiwa ambapo oati ya hizo, Rada mbili zinakamilishwa kufungwa katika mikoa ya Mbeya na Kigoma .

"Utengenezaji wa rada nyingine mbili (2) zitakazofungwa katika mikoa ya Kilimanjaro na Dodoma unaendelea kiwandani nchini Marekani na zinatarajiwa kukamilika na kufungwa mwaka huu wa 2024. Rada nyingine tatu (3) zimekamilika na kufungwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Mtwara" amesema Prof.Mbarawa.

Amesema kuwa kukamilika kwa ufungaji wa rada hizo kutaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki kuwa na idadi kubwa ya rada za hali ya hewa na kuimairisha huduma za uangazi na utabiri wa matukio ya hali mbaya ya hewa.

Prof. Mbarawa amesema kuwa serikali imenunua seti tano za vifaa vya utambuzi wa matukio ya radi . "Serikali imetambua changamoto kubwa iliyopo kwa baadhi ya maeneo yanayoathirika na radi za mara kwa mara na imenunua seti tano (5) za vifaa vya utambuzi wa matukio ya radi ambavyo vimefungwa katika maeneo ya Musoma, Mwanza, Kagera, Tabora na Kigoma ".

Prof. Mbarawa amesema kuwa Serikali inafanya jitahada zote kwa lengo la kuwaletea maendeleo ya uhakika wananchi wake hasa katika sekta ya kilimo ambapo serikali imenunua vituo 15vya utafiti wa maendeleo ya kilimo.

"Kwa kutambua kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa nchi yetu, Serikali imewezesha ununuzi wa vituo kumi na tano (15) vya kupima hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe (Automatic Weather Stations) ambavyo vitafungwa katika vituo vya utafiti na maendeleo ya kilimo ili kuchagiza utafiti kuhusiana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa sekta ya kilimo" amesema Prof. Mbarawa.

Waziri Mbarawa amesema kuwa miaka mitatu ya serikali ya awamu ya sita imeamua kuimarisha huduma za hali ya hewa kwa ajili ya usafiri wa anga, Serikali imeendelea kuwekeza katika kuimarisha mtandao wa vituo na uwezo wa uchakataji taarifa, ikiwemo ununuzi na ufungwaji wa vifaa vya kisasa vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe vinavyosaidia kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa kwa ndege zinaporuka na kutua.

Amesema hatua nyingine zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha hali ya hewa na ufuatiliaji wa Tsunami cha Kanda ya Mashariki, Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha ufuatiliaji wa matukio ya hali mbaya ya hewa hususan yanayoanzia baharini na ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 39.

Amesema kuwa uboreshaji huu wa miundombinu unaenda sambamba na kuwajengea uwezo wataalamu wa hali ya hewa na watumishi katika sekta hii na wameendelea kupatiwa mafunzo mbalimbali.

"Katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya sita jumla ya watumishi 228 (Wanaume 177 na Wanawake 51) wamepatiwa mafunzo ya muda mrefu katika ngazi ya diploma (33), shahada ya kwanza (90), Shahada ya Uzamili (79) na Shahada ya Uzamivu (16) kupitia vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi" amesema Prof. Mbarawa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), Dkt. Ladislaus Changa amesema Mamlaka hiyo inapambana usiku na mchana ili kuihami Tanzania na mabadiliko ya tabianchi yatakayoathiri maendeleo .

Dkt. Changa amesema kuwa mbali na vifaa vya kisasa TMA inafanya jitihada za kufanya tafiti za kila siku ili kupata suluhisho la kudumu la mabadiliko hayo.

"TMA inaendelea kuwa mstari wa mbele kutoa mchango katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kwa kufanya tafiti na kuhamasisha matumizi ya sayansi na uvumbuzi miongoni mwa wataalamu wake na wataalamu wengine katika vyuo vikuu na taasisi za utafiti nchini na barani Afrika".Amesema Dk. Changa.

Amesema kuwa Wataalamu wa TMA wameendelea kubuni mifumo mbalimbali ya kuongeza ufanisi na kuimarisha uchakataji wa data na utoaji wa huduma za hali ya hewa.

"Mifumo hiyo ni pamoja na; TMA Digital Meteorological Observatory (DMO) ambao hutumika katika kuimarisha mawasiliano ya data za hali ya hewa kutoka vituoni kote nchini; mfumo wa utoaji wa taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wa bahari na maziwa (Meteorological Marine MMAIS) na mfumo wa Meteorological Aviation Information System (MAIS) ambao hutumika katika mawasiliano na sekta ya usafiri wa anga" amesema Dkt. Changa.

Amesema kuwa Mifumo hiyo imekuwa na manufaa na kuleta tija kubwa katika mawasiliano ya taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wa huduma za hali ya hewa ikiwemo sekta ya anga na baharini. Huduma za hali ya hewa kwa ajili ya sekta ya usafiri wa anga nchini zimethibitishwa na zinatumbuliwa kukidhi vigezo na viwango vya kimataifa kwa mujibu wa Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO) kwa cheti cha ISO 9001:2015 tangu mwaka 2017 na kabla ya hapo ISO 9001:2008.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad