*Wauguzi, Madakari wanawake kupata ufadhili masomo
Na Mwandishi Wetu
Benki ya Diamond Trust (DTB) ikishirikiana na Taasisi ya Aga Khan Foudation imetoa majiko nane ya ‘Microwave’ kwa wodi za wanawake Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) pamoja na fursa ya udhamini wa masomo kwa walio na digrii ikiwa ni mkakati wa kusaidia Sekta ya Afya nchini.
Maryvine Peter, Meneja wa Benki Kituo cha DTB alisema hayo siku ya Ijumaa Jijini Dar es Salaam baada ya wawakilishi wanawake wa benki hiyo kuungana na wafanyakazi wa MNH wanawake, katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Alisema msaada huo pamoja na fursa ya udhamini, umelenga kutambua mchango wa wauguzi na madaktari wanawake katika kuhudumia wagonjwa kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyosema ‘Wekeza kwa Wanawake Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii.’
“Kama Benki ya DTB, tumetoa majiko ya ‘microwave’ kwa wodi za wanawake Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Pamoja na hayo kwa kushirikiana na Taasisi ya Aga Khan Foundation tupo hapa kuutangazia umma kwamba tuna fursa za udhamini wa elimu kwa wahitimu wenye digrii hususani kwa wauguzi na madaktari wanaotamani kuendelea na masomo yao.Tupo hapa kwa ajili ya kuwasaidia,” alisema Maryvine.
Aliongeza: “Tupo hapa kwa ajili ya kutekeleza kauli mbiu ya mwaka huu inayosisitiza ujumuiswaji kwa wanawake na kama wanawake tupo hapa kwa ajili ya kuwainua wanawake wenzetu wanaohakikisha kwamba wanatimiza mchango wao katika hospitali ya Muuhimbili.”
Tegemea Ndemo, Meneja Rasilimali Watu na Utawala wa Taasisi ya Aga Khan Tanzania alisema Taasisi hiyo inayoijumuisha Benki ya DTB huwa na utaratibu wa kudhamini masomo kwa lengo la kuwainua wanawake wasiojiweza.
“Maombi ya udhamini wa masomo kwa yanafungwa rasmi Machi 31, mwaka huu, hivyo bado mna muda.Kwa wale wanaotaka kutumia fursa hii mnione baadaye nitawapa vipeperushi ili isaidie pia wengine katika kupiga hatua mbele kielimu,” aliongeza.
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji (MNH), Dk Rachel Mhaville, aliyepokea msaada wa ‘microwave kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Profesa Mohammed Janabi, aliishukuru maamuzi ya taasisi hiyo kusaidia wauguzi na madaktari wanawake na udhamini ulilolenga kusaidia wananwake wasiojiweza nchini.
Pia aliwaasa wanawake kupendana na kushirikiana maana kwa kufanya hivyo huongeza utendaji kazi na hata kupata fursa ya kuona njia zitakazoweza kukuza Uchumi wao.
Benki ya Diamond Trust (DTB) na Taasisi ya Aga Khan Foudation wakikabidhi majiko nane ya ‘Microwave’ kwa wodi za wanawake Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani
Picha ya pamoja ya wanawake Benki ya Diamond Trust (DTB) na Taasisi ya Aga Khan Foudation mara baada ya kukakabidhi majiko nane ya ‘Microwave’ kwa wodi za wanawake Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani
No comments:
Post a Comment