HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 23, 2024

WAZIRI SIMBACHAWENE ARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA MAMLAKA YA SERIKALI MTANDAO, AITAKA IONGEZE KASI KUSANIFU MIFUMO

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akizungumza na Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGa) Kituo cha Iringa wakati wa ziara yake ya kikazi katika kituo hicho.

Na Lusungu Helela- Iringa

 WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene aridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) huku akiitaka iongeze kasi zaidi katika kusanifu na kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili kuiwezesha Serikali kutoa huduma kwa umma kwa haraka na ufanisi.

Simbachawene ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na Watumishi wa eGA-Kituo cha Iringa ambapo amewataka Watumishi hao kuhakikisha Serikali inaendeshwa kidigitali kwenye kila nyanja kupitia mifumo wanayoisanifu.

Amesema eGA ni taasisi muhimu katika dunia ya sasa ambapo Serikali inahitaji mapinduzi ya TEHAMA ili itoe huduma zake kwa wananchi kiurahisi na kwa haraka

“Dunia inakwenda kasi na teknolojia ni kila kitu kwa sasa, hivyo ni muhimu kwa eGA kufanya utafiti, kubuni na kutengeneza mifumo ya TEHAMA Serikalini kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma kwa umma” amesema Mhe. Simbachawene.

Simbachawene ameongeza kuwa eGA imeweka juhudi kubwa katika kusimamia TEHAMA Serikalini na imetengeneza na inaendelea kutengeneza mifumo ya TEHAMA ambayo imewarahisishia wananchi kupata huduma kwa haraka, mahali popote na kwa gharama nafuu na kuchagiza utawala bora.

Aidha, Simbachawene ameridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao katika ofisi zake zilizopo Iringa na amewataka watumishi wa Mamlaka kwa jumla kuendelea kubuni Mifumo ya TEHAMA inayotatua changamoto zilizopo nchini pamoja na kuwa wazalendo kwa maslahi ya Taifa.

Vile vile, amewasisitiza watumishi wa eGA kuhakikisha mifumo inayotengenezwa na iliyopo inakuwa na uwezo wa kuwasiliana ili kuleta ufanisi katika kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba amemshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Simbachawene kwa kutenga muda wake kutembelea kituo hicho cha Iringa na kuahidi kutekeleza maagizo yote aliyotoa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akisaini kitabu mara baada ya kuwasili Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGa) Kituo cha Iringa wakati wa ziara yake ya kikazi katika kituo hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba akitoa maelezo kuhusu Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGa) Kituo cha Iringa kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene kuzungumza na Watumishi hao.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete akizungumza na Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGa) Kituo cha Iringa (hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha Waziri Simbachawene kuzungumza nao.
Sehemu ya Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGa) Kituo cha Iringa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kituo hicho.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad