HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, February 18, 2024

WATOTO 174,298 WALENGWA KUFIKIWA KUPATA CHANJO YA SURUA-RUBELLA MKOANI PWANI -KUNENGE

 

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKOA wa Pwani ,unalenga kufikia watoto wenye umri chini ya miaka mitano 174,298 kwa ajili ya kupata chanjo ya Surua - Rubella inayotolewa katika maeneo mbalimbali.

Kampeni ya chanjo hiyo tayari imeanza Februari 15 mwaka huu na itamalizika Februari 18 ambapo Mkoa huo chanjo hiyo inapatikana katika ngazi ya vituo vya huduma ya afya, kaya kupitia huduma ya mKoba pamoja na maeneo mengine yaliyoainiashwa.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,alhaj Abubakar Kunenge aliyaeleza hayo kwa waandishi wa habari, wakati wa mkutano maalum wa kuhamasisha kampeni ya masuala ya chanjo ya Surua na Rubella uliofanyika ofisini kwake .


Kunenge aliwaomba wananchi hususani wenye watoto chini ya umri wa miaka mitano kuhakikisha wanawafikisha watoto wao katika vituo hivyo ili waweze kupata huduma hiyo.


"Magonjwa ya Surua na Rubella husababishwa na virusi vinavyoenea kwa haraka kwa njia ya hewa hususani pale mgonjwa anapokohoa au kupiga chafya na huathiri watu wa rika zote lakini watoto wenye umri chini ya miaka mitano huathirika zaidi".


Pia anawaelekeza viongozi mkoani hapo ,kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa kampeni kwenye maeneo yao ikiwa pamoja na kuhakikisha watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano wanafikiwa.


Kunenge aliwaomba viongozi wa dini na taasisi mbalimbali kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha zoezi hilo katika maeneo yao ili kuweza kufikia malengo ya Serikali ya kuwanusuru watoto dhidi ya magonjwa hayo.


Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Dr Benedicto Ngaiza, anasema dalili za magonjwa hayo ni homa,mafua,na kikohozi ,macho kuwa mekundu na kutoka machozi,kutoka vipele vidogovidogo vinavyoanzia katika paji la uso,nyuma ya masikio na kusambaa usoni na mwili mzima.


Magonjwa hayo madhara yake ni makubwa Kwa binadamu ikiwemo masikio kutoka usahau ambao unaweza kusababisha kutosikia ,vidonda vya macho vinavyopelekea upofu,Nimonia,utapiamulo na kwamba mgonjwa hasipopata tiba sahihi anaweza kupata ulemavu na hata kupoteza maisha.


"Magonjwa haya yanazuilika kwa chanjo,Mtoto hupata dozi mbili za chanjo ya kumkinga na Surua na Rubella ambazo hutolewa anapotimiza umri wa miezi 9 na marudio ni pale anapotimiza miezi 18",amesema Dr.Ngaiza


Ngaiza,aliiasa jamii kuacha hofu kwani Serikali inaendesha zoezi la utoaji chanjo kwa ajili ya kuwapa kinga watoto ili wasishambuliwe na magonjwa hayo .

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad