HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, February 28, 2024

CMSA YAWEZESHA KUONGEZEKA KWA THAMANI YA UWEKEZAJI KATIKA MASOKO YA MITAJI NA MAUZO SOKO LA HISA

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Masoko Mitaji na Dhamana (CMSA) imekuwa ikitekeleza mikakati ya kuanzisha bidhaa bunifu na endelevu za masoko ya mitaji ambazo zimewezesha kuongezeka kwa thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji na mauzo katika soko la hisa.

Thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 31.2 na kufikia shilingi trilioni 37.3 katika kipindi kilichoishia Januari 2024, ikilinganishwa na shilingi trilioni 28.4 katika kipindi kilichoishia Januari 2021; na mauzo katika soko la hisa yameongezeka kwa asilimia 61.6 na kufikia shilingi trilioni 9.3 katika kipindi kilichoishia Januari 2024, ikilinganishwa na shilingi trilioni 5.8 katika kipindi kilichoishia Januari 2021.

Ameyasema hayo leo Februari 28,2024 Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati akisoma hotuba kumwakilisha Waziri wa Fedha, Dkt. Mwingulu Nchemba wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Maendeleo ya Masoko ya Mitaji katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) ulioratibiwa na Taasisi ya uendelezaji wa Sekta za fedha barani Afrika (FSDA) kwa Kushirikiana na Kamati ya Masoko ya hisa ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (COSSE) na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).

Amesema baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kuanzisha bidhaa bunifu na endelevu za masoko ya mitaji nchini Tanzania, ni pamoja na utoaji wa hatifungani ya kwanza ya Kijani yaani Green Bond yenye thamani kubwa katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara iitwayo "Kijani Bond" ambayo iliwezesha kupata shilingi bilioni 171.83 sawa na mafanikio ya asilimia 430, ambapo fecha zilizopatikana zinatumika kutekeleza miradi ya kutunza na kuhifadhi mazingira.

Aidha amesema utoaji wa hatifungani ya Jasiri Bond ambayo imewezesha kupata shilingi bilioni 74.2 sawa na mafanikio ya asilimia 297, umeweka historia ya kuwa hatifungani ya kwanza yenye mguso wa Jinsia yaani Gender Bond kutolewa katika Ukanda Kusini mwa Jangwa la Sahara.

"Masoko ya mitaji ya Tanzania yamefanikiwa kutoa hatifungani ya Jamii yaani Social Bond ambayo imewezesha kupata shilingi bilioni 212.9 sawa na mafanikio ya asilimia 284". Amesema

Pamoja na hayo ameipongeza Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kwa kutekeleza hatua muhimu ambazo zinawezesha kufikia azma na malengo ya Serikali ya kuwa na uchumi shindani na endelevu kwa maendeleo ya watu.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama amesema wanawavutia wawekezaji wa kitaifa na kimataifa kuwekeza nchini ili kupata fedha za kigeni zinazochochea maendeleo ya kiuchumi nchini.

“Tunaitangaza nchi yetu duniani kupitia utoaji bidhaa bunifu kwenye masoko ya mitaji ambapo vilevile itawavutia wawekezaji ,” amesema Mkama.










No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad