HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, January 18, 2024

WAZIRI WA ULINZI, BALOZI MINGJIAN WASAINI MIKATABA YA MSAADA WA KIJESHI

Waziri wa Ulinzi na JKT, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb.) na Balozi wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Chen Mingjian   leo Januari 18, 2024 jijini Dar es Salaam, wakisaini mikataba ya msaada wa kugharamia ununuzi wa zana na vifaa vya kijeshi wenye thamani ya Chinese Yuan RMB milioni 100 sawa takriban Shilingi za Kitanzania 35,030,000,000. 

Waziri wa Ulinzi na JKT, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb.) na Balozi wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Chen Mingjian wakionesha mikataba mara baada ya kusaini leo Januari 18, 2024 jijini Dar es Salaam.msaada wa kugharamia ununuzi wa zana na vifaa vya kijeshi wenye thamani ya Chinese Yuan RMB milioni 100 sawa takriban Shilingi za Kitanzania 35,030,000,000.


Picha ya pamoja.

WAZIRI wa Ulinzi na JKT, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb.) na Balozi wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Chen Mingjian kwa pamoja wametiliana saini mikataba miwili baina ya Wizara ya Ulinzi na JKT ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Watu wa China kuhusu msaada wa kugharamia ununuzi wa zana na vifaa vya kijeshi wenye thamani ya Chinese Yuan RMB milioni 100 sawa takriban Shilingi za Kitanzania 35,030,000,000.

Akiongea maneno ya utangulizi kabla ya kusainiwa kwa mikataba hiyo, kwa niaba ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla, ametoa shukurani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China pamoja na Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (Peoples Liberation Army), kwa msaada wa zana na vifaa vya kijeshi kupitia mpango maalum wa Jumuiya ya Afrika (AU), ambapo China iliridhia kuipatia msaada Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia JWTZ.

Aidha, Mheshimiwa Waziri ameongeza kusema kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuthamini misaada isiyo na ukomo, inayoendelea kutolewa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia sekta ya ulinzi hususan JWTZ.  Jitihada zote na kujitoa huko kunaziwezesha Serikali hizi mbili kushirikiana na kufanya kazi kwa Karibu. Akitoa mfano wa tukio la leo, ambalo ni kielelezo tosha katika kukuza na kuendeleza ushirikiano wa kihistoria uliodumu kwa muda mrefu baina ya mataifa haya.

Vile vile, Dkt. Stergomena amebainisha kuwa kusainiwa kwa mikataba hii, kunaashiria ni kwa namna gani mataifa haya mawili, yalivyo na dhamira ya dhati katika kudumisha ushirikiano, kuendelea kusaidiana na kuimarisha urafiki wa kindugu.

Waziri Stergomena amemhakikishia Mheshimiwa mingjian pia, kuwa Wizara ya Ulinzi na JKT, itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China katika kuendeleza ushirikiano baina mataifa haya mawili, lengo likiwa kuimarisha majeshi haya mawili (PLA na JWTZ), na ni imani yake kuwa kwa kufanya kazi pamoja na kwa umoja wao wataweza kukabiliana na changamoto za kiulinzi zilizopo na zitakazoibuka siku za usoni.

Mheshimiwa Dkt. Stergomena pia, amemshukuru na kumpongeza Balozi Mingjian na timu yake pamoja na timu ya Wizara ya Ulinzi na JKT, kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya. Ushirikiano wa dhati baina ya mataifa ya Tanzania na China ni hatua muhimu katika kudumisha na kuimarisha mahusiano, katika kujenga umoja wenye nguvu na wa kina, na wenye undugu baina ya mataifa haya mawili.   

Kwa upande wake, Balozi anayeiwakilisha Jamhuri ya Watu wa China hapa nchini, Mheshimiwa Chen Mingjian amebainisha kuwa uhusiano baina ya Jeshi la Ukombozi la Watu wa China na JWTZ ulianza tangu mwaka 1964, mara tu baada ya kuundwa kwa JWTZ. Aidha, ameainisha maeneo mbalimbali ya ushirikiano baina majeshi ya nchi hizi mbili. Ameyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na misaada ya kijeshi, zana na vifaa, mafunzo ya pamoja, tiba, na viwanda vya kijeshi.

Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Jacob John Mkunda akitoa neno la shukrani, amemhakikishia Balozi Chen kuwa JWTZ litatumia msaada uliotolewa na Serikali yake kwa Jeshi, utatumika ipasavyo na kwa ufanisi mkubwa, ili kuleta matokea chanya katika kutimiza malengo yaliyokusudiwa. 


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad