HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 17, 2024

TUSIPOCHUKUA TAHADHARI TUTAIPOTEZA NGORONGORO IFIKAPO 2050- MATINYI

  

Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi  akizungumza  na waandishi wa habari leo mchana Msomera, Wilayani Handeni Mkoani Tanga.


Na Khadija Kalili, MSOMERA
MSEMAJI  Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara  ya Habari MAELEZO  ,
Mobhare Matinyi  amesema kuwa wataalamu wa masuala  ya ekolojia  wameiambia  Serikali  kuwa endapo hawatasimamia kidete suala la kuwahamisha wananchi wanaoishi katika hifadhi ya Ngorongoro  itapotea  ifikapo 2050 ikiwa ni pamoja na wanyama kutoweka kabisa.

Matinyi  amesema hayo leo alipokua akizungumza na waandishi wa habari kutoka katika vyombo mbalimbali  vya habari ambao wamefanya ziara  kwenye hifadhi ya taifa ya Ngorongoro  ambapo wamejionea namna wananchi wanavyoishi na mifugo yao ndani ya hifadhi hiyo na baada ya hapo wametembelea makazi mapya ya Msomera yanayojengwa na serikali.

Matinyi  amesisitiza kuwa  serikali bado inaendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi hiyo huku idadi kubwa wakiendelea kujiandikisha kuhama.

"Awali idadi ya wakazi waliokuwa wakiishi ndani  ya hifadhi ilikua chache  ambao ni 8,000  ambao pia  walikua na mifugo michache tofauti na ilivyo sasa ndani ya hifadhi kumekua na kaya 100,000 huku mifugo ya ng'ombe, mbuzi, kondoo wamezidi kuzaliana hali ambayo imesababisha kuwakimbiza wanyama wa asili.

'Hivyo basi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  chini ya  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haitakuwa tayari kuipoteza Ngorongoro ndiyo maana tunaendelea kuwahamisha wakazi kwa kuwalipa fidia na kuwajengea nyumba. "

"Serikali inatoa elimu ya uhamasishaji  inafanya tathmini ya kuwalipa kila mtu  mwenye mali anayomiliki ambao  wanaishi  katika hifadhi ya  Ngorongoro na baada ya kuwalipa kwa kila kaya ikiwa ni pamoja na kupewa kiasi cha fedha cha Milioni 10, huku mamlaka ya hifadhi  ya Ngorongoro itamhamisha kwa gharama zake bila kulipishwa  muhusika yeye, mali zake ikiwemo mifugo  pamoja  na familia  yake kwenda kwenye makazi mapya yaliyopo Msomera  Wilaya  Handeni Mkoani Tanga.

"Tayari zimeshafanyika awamu mbili huku ya kwanza  imefanyika 2022 sasa tupo  kwenye utekelezaji  awamu ya pili  ambayo  imeanza Julai 2023   na inatarajiwa  kukamilika  Machi , 2024 huku lengo kubwa la serikali  ni kujenga  nyumba  5,000 katika  eneo  linalojumuisha Kitwai, Sauni na  Msomera kwa ajili ya wakazi wa Ngorongoro  wanaohamia  kwa hiyari eneo la Msomera."
Amesema Matinyi. 
 
Matinyi amesema kuwa kila  mwananchi anajengewa nyumba yenye vyumba vitatu anapewa fursa  ya kuunganishiwa  umeme na TANESCO kwa gharama ya  27,000, huku Wizara ya Maji inachimba  visima  ambavyo vitakuwa  na sehemu za kusambazia  maji ili wananchi waweze kupata maji.

 Matinyi  amesema kuwa kwa upande wa wananchi ambao hawatopenda kuhamia Msomera watapewa fidia ya mali zao, watasafirishwa kwa gharama ya serikali hadi katika  Mkoa ambao wameuchagua nakupewa kiasi cha  Sh. MI.15  tu.

"Kuna Wizara tayari  zimefika hapa  Msomera zikaunda timu ya pamoja  ili kufanya oparesheni hii ifanikiwe zipo Wizara kumi ambazo ni Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa  na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Maliasili na Utalii, Nishati, Habari  Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kilimo, Maji, Mifugo  na Uvuvi, Maendeleo. 

Aidha Matinyi amesema kuwa Wizara ya kilimo imesema  mbali ya kuwatengea mashamba wameanzisha mashamba darasa   kwa wakazi  hao ili wananchi hawa  waweze kulima mbali na shughuli walizokuwa wamezizoea awali za ufugaji.

Akifafanua kuhusu  shughuli  za kiuchumi amesema kuwa zinakwenda  kuongezwa  ili maisha  ya wananchi hao  yawe  mazuri. 

"Milango iko wazi kwa wawekezaji waje kuwekeza katika mji huu mpya na wa kisasa amesema Matinyi.

"Kutajengwa  minada  ya  kisasa ili wananchi wapate nafasi ya kupanua ukuaji wa wigo wa uchumi, kujenga  vituo vya kukusanyia maziwa, kwani wafugaji ukiacha uuzaji wa nyama kwenye mnada huwa wanauza  maziwa kwa hiyo kutakuwa na vituo kwa ajili ya wananchi  kupeleka  maziwa na kupata pesa." Amesema Matinyi

Wakati huohuo Msemaji Mkuu wa Serikali Matinyi  ametoa wito kwa Asasi za Kiraia pamoja na vyombo vya nje ya nchi kuacha kutoa taarifa za mbaya na za uongo kuwa uhamishwajiwa wananchi unakiuka haki za binadamu.

"Hizi ni propaganda za watu wachache mbao wanania ovu  hivyo ili waweze kujiridhisha tunawakaribishawaje  Ngorongoro na Msomera ili kuona  hali halisi ya maisha  walikokua wakiishi kabla na baada kisha ndipo waende wakaitangazie dunia.

 "Serikali  haiko tayari kuona wananchi wake wanaishi katika mazingira hatarishi na wanyama wakali ambao wamekuwa wakiwasababishia maafa ikiwemo  vifo  ikiwemo kutoishi kwa uhuru wa kutembea kwani ndani  ya hifadhi mwisho wa kutembea nisaa 12 jioni.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad