Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania TPA imepongezwa kwa utendaji wenye ufanisi mkubwa na kutakiwa kuongeza juhudi ili kupata mafanikio zaidi na kuongeza mchango wa Sekta ya Bandari katika Uchumi wa Taifa.
Pongezi hizo zimetolewa na Viongozi mbalimbali wa Serikali waliotembelea Banda la TPA katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Zanzibar yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya maonesho vya Fumba, Zanzibar.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe amesema, Sekta za Viwanda na Biashara zinaitegemea sana Sekta ya Uchukuzi katika kufanikisha mipango yake ya kuhudumia Wananchi na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Bidhaa zinazozalishwa na Wajasiriamali na Viwanda vyetu vya ngazi zote, vinahitaji sana uhakika wa kupata malighafi na uhakika wa kuyafikia masoko ya ndani na nje ya Nchi. Tunaipongeza TPA na Taasisi nyingine za Uchukuzi kwa kazi kubwa ya kuwezesha Wananchi kupata tija katika shughuli zao za uzalishaji na Biashara ya mazao na bidhaa zinazozalishwa katika Sekta mbalimbali.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara ameipongeza TPA kwa kushiriki maonesho yanayoendelea na kwa mafanikio makubwa ya kuhudumia Meli na Shehena katika nusu ya kwanza ya mwaka wa Fedha 2023/2024.
‘Nimefurahi kwanza kwa kushiriki kwenu katika maonesho haya ambapo tunaungana na Watanzania wenzetu wa upande wa Visiwani kutafakari kwa pamoja namna bora ya kuongeza ufanisi wa huduma zetu kwa Wananchi na Wanufaika wengine. TPA na ZPC mnafanya kazi nzuri katika Sekta ya Bandari lakini bado zipo fursa za kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na ndio maana Serikali zote mbili zinafanya jitihada kubwa za kuwezesha ufanisi huo kupatikana.
Natoa wito kwa Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TPA kusimamia kikamilifu mipango yenu mliyojiwekea ambayo ikitekelezwa vyema, shughuli za Bandari zitakuwa na mchango mkubwa zaidi katika Pato la Taifa na Maendeleo ya Nchi yetu kwa ujumla’
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Dkt. Ally Possi amesema, ushiriki wa TPA katika maonesho haya ya Zanzibar ni fursa muhimu ya kukuza ushirikiano kati ya TPA, ZPC na Taasisi nyingine ili kubadilisha uzoefu na kukutana na Wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa Huduma zinazotolewa na Taasisi hizi.
“TPA mnafanya kazi kubwa sana, mnastahili pongezi, lakini haitoshi sisi viongozi kujua kuwa mnafanya vyema, Wananchi nao wanastahili kujua hivyo. Tumieni wasaa huu kuwaelimisha, toeni ufafanuzi wa kina kuhusu maswali yao na pokeeni hoja na ushauri wao, kwa kufanya hivyo mtakuwa mmetimiza vyema wajibu wenu wa kushiriki katika tukio hili muhimu ambalo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Akizungumza katika mapokezi ya Viongozi hao kwa Niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa TPA Bw. Nicodemus Mushi amesema, tumefurahi kupata wasaa wa kukutana na Wananchi wa Tanzania Visiwani na tunaendelea kuwapa Elimu kuhusu utendaji wa Sekta ya Bandari upande wa Bara pamoja na mipango ya kuboresha Huduma katika eneo la Majahazi katika Bandari ya Dar es Salaam ambalo linahudumia Abiria na Mizigo inayosafiri kati ya Tanzania Bara na Visiwani.
Bw. Mushi ameongeza kuwa, TPA tumejipanga vyema kuboresha Miundombinu yake katika eneo hilo pamoja na kufanya marejeo ya Kanuni zinazosimamia utoaji huduma za Bandari ili kuondoa kero zinazolalamikiwa na Wateja na Wadau wake.
‘Katika kipindi kifupi kijacho, TPA itafanya uchimbaji wa kuongeza kina katika eneo la majahazi ili Vyombo vinavyotumia eneo hilo viweze kutoa huduma kwa ufanisi wakati wote, tumejipanga pia kuimarisha gati la Abiria na Miundombinu ya ukaguzi wa bidhaa bandarini ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma katika eneo hilo, Amesema Bw Mushi.
Katika kipindi cha miezi sita ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 (Julai- Desemba, 2023) Bandari za TPA zimehudumia jumla ya tani 13.945 Milioni sawa na asilimia 109.4 ya lengo la kipindi husika la kuhudumia tani 12.752 Milioni ambapo bandari ya DSM imehudumia jumla ya tani 12.052 milioni.
Katika kipindi husika bandari za TPA pia zimehudumia jumla ya makasha 536,683 TEUs sawa na asilimia 105.8 ya kuhudumia makasha (TEUs) 507,212 ambapo bandari kuu ya DSM imehudumia makasha (TEUs) 509,594.
Aidha, TPA ilijiwekea lengo la kuhudumia magari 102,500 katika bandari ya Dar es Salaam ambapo hadi kufikia mwezi Desemba, 2023 TPA ilikuwa imehudumia 106,823 sawa na asilimia 104.2 ya lengo la kipindi husika.
Friday, January 12, 2024
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment