KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Matakatifu Francis amemualika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan mjini Vatican kwa mazungumzo rasmi ya siku mbili baina ya viongozi hao.
Hayo ameyasema leo, Januari, 21, 2024, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, amesema kuwa Rais Samia ataenda Katika Mji wa Vatican na kufanya mazungumzo na Papa Februari 11 na 12, 2024.
Makamba amesema Rais Samia ataenda na Waumini wa Kawaida kabisa kuanzia viongozi wa Jumuiya, Umoja wa Vijana Wakatoliki (VIWAWA), umoja wa Wanawake wakatoliki (WAWATA).
"Hii ni heshima kubwa kwa nchi yetu na Rais wetu, kwani mazungumzo hayo na Baba Mtakatifu ni ya heshima kubwa na watu wachache sana ndio watapata fursa ya kuhudhuria mazungumzo hayo. " Amesema Makamba
Aidha, akiwa Vatican, Rais Dkt. Samia atakutana kwa mazungumzo na Baba Mtakatifu Francis pamoja na Katibu wa Vatican, Pietro Parolin.
Kabla ya Rais Dkt. Samia kwenda kwenye mazungumzo na Papa mjini Vatcan, Februari 11 na 13, 2024, atafanya ziara ya Kitaifa nchini Indonesia kuanzia Januari 24- 26, 2024, kufuatia mwaliko wa Mheshimiwa Joko Widodo, Rais wa Jamhuri ya Indonesia.
"Ziara hiyo ya Kitaifa inafuatia ziara ya Kitaifa ya Rais Joko Widodo aliyoifanya nchini mwezi Agosti 2023, ziara hiyo italenga kukukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Indonesia kupitia sekta mbalimbali za biashara na uwekezaji, kilimo, nishati, madini, mifugo, uvuvi, uchumi wa buluu, elimu, utalii na ulinzi.
Pia atafanya ziara katika Nchi ya Norway, Februari 13- 14, 2024, Kufuatia mwaliko kutoka kwa Mfalme Herald wa Norway na Malkia Sonja.
Akiwa nchini Norway, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakutana kwa mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Serikali hiyo akiwemo Mfalme Herald, Rais pia atashiriki Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Norway pamoja na Kogamano la Nishati la Oslo.
Lengo likiwa ni kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Norway kupitia sekta mbalimbali zikiwemo biashara, uwekezaji, nishati kama mafuta na gesi, elimu na masuala ya kodi na utawala bora.
Kuimarisha na kukuza sekta ya nishati hususan kutekeleza miradi ya usambazaji umeme vijijini, kushirikiana katika program za utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi, kukuza sekta za biashara, uwekezaji na utalii.
ZIARA ZA VIONGOZI WENGINE WA NJE NCHINI WANAOTARAJIWA KUFANYA ZIARA NCHINI TANZANIA
Wakati huo huo Waziri Makamba amesema kuwa Tanzania inatarajia kumpokea, Liu Guozhong Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China na Mjumbe wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China kuanzia kesho Januari 22- 24, 2024.
Ambaye atafanya mazungumzo na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kassim Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Dkt. Dotto Biteko (Mb.), Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia Januari, 23- 25, 2024, Rais wa Jamhuri ya Cuba, Salvador Valdes Mesa, anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu, ziara hiyo imelenga kuendelea kudumusha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Cuba.
Rais huyo anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Dkt. Philip Mpango, Dkt. Tulia Akson, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuzungumza kwa simu na Dkt. Husein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Pia Rais huyo wa Cuba, Mesa atamtembelea Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mama Maria Nyerere, na atashiriki kwenye mkutano wa wanachama wa urafiki kati ya Tanzania na Cuba, Watanzania waliosoma Cuba na Taasisi ya PanAfrican Movement pamoja na kutembelea kiwanda kinachozalisha dawa ya Biolarvicide cha Kibaha, Pwani.
Licha ya hayo Rais wa Jamhuri ya Poland, Andrzej Duda atakuwa na ziara ya kikazi nchini Februari, 8 na 9 2024 na atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi.
No comments:
Post a Comment