Mkurugenzi wa EFTA, Bwana Nicomed Bohay akiwakabidhi, baadhi ya wanafufaika wa mkopo wa vifaranga vya kuku ambao kampuni hiyo imevitoa kwa wafugaji mbalimbali bila dhamana. Jumla ya vifaranga 30,000/= vimekabidhiwa kwa wafugaji wa kuku wapatao thelathini katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Bi Mwanamvua Ngocho, Meneja Masoko wa Kampuni ya Silverlands Tanzania Ltd, wazalishaji wa vifaranga bora vya kuku ambao wanahusika na kuzalisha vifaranga vinavyotolewa kwa mkopo na EFTA kwa wakulima mbalimbali nchini, akimuongoza mkurugenzi mtendaji wa EFTA, kutembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji wa vifaranga hivyo.
Mkurugenzi wa EFTA, Bwana Nicomed Bohay akiwakabidhi, baadhi ya wanafufaika wa mkopo wa vifaranga vya kuku ambao kampuni hiyo imevitoa kwa wafugaji mbalimbali bila dhamana. Jumla ya vifaranga 30,000/= vimekabidhiwa kwa wafugaji wa kuku wapatao thelathini katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Baadhi ya wanufaika wa mkopo wa vifaranga vya kuku kutoka EFTA, wakiwa katika picha ya pamoja na mkurugenzi mtendaji wa EFTA Bwana Nicomed Bohay, baadhi ya maafisa kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha, wakati wa hafla ya kuzindua utoaji wa mikopo ya kuku kwa wafugaji nchini. Picha na mpiga picha wetu.
Na Mwandishi Wetu
Arusha, Tanzania
Taasisi ya EFTA inayojishughulisha na utoaji wa mikopo
ya mashine na magari bila dhamana kwa wajasiriamali na wakulima nchini,
imetenga Zaidi ya shilingi Bilioni 3.5 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo
kwa lengo la kuwawezesha vijana na wanawake nchini kupata mikopo ya vifaranga
vya kuku, chakula Pamoja na mahitaji mengine muhimu ya ufugaji wa kuku bila
dhamana.
Mpango wa mkopo wa vifaranga vya kuku kwa wakulima na
hususani vijana na wanawake wasiokuwa na ajira au wanaotaka kujipatia kipato
cha ziada ni wa kwanza na wa aina yake kwa taasisi ya kifedha nchini kuutoa kwa wakopaji.
EFTA imezindua mpango huu ikiwa ni sehemu ya kuunga
mkono jitihada za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Dr
Samia Suluhu Hasan, ambaye amekuwa akijipambanua katika kuhakikisha kuwa
watanzania na hususani vijana na wanawake wanawezeshwa kiuchumi kwa kuwawezesha
kupata mikopo ya aina mbalimbali ambayo itawasaidia kuanzisha shughuli
mbalimbali za kiuchumi.
Kwa muda sasa kundi la vijana na wanawake nchini
Tanzania, ni miongoni mwa makundi ambayo yamekuwa yakitajwa kuwa na idadi kubwa
ya watu wasiokuwa na ajira rasmi hatua ambayo imekuwa ikichangia kuongezeka kwa
umasikini miongoni mwa kundi hili.
Serikali kupitia mpango wa Jenga Kesho Bora
unaojulikana kama “Built Better Tomorrow – Youth initiative for Agribusiness
(BBT-YIA), umewezesha vijana wengi nchini kupata fursa ya mafunzo na mikopo ya
kuanzisha na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kilimo na ufugaji hapa
nchini.
Kampuni ya EFTA katika kuunga mkono jitihada hizo za
serikali nayo imeamua kuanzisha mpango wa majaribio wa mkopo wa kuku kwa vijana
na wanawake bila dhamana. Hatua ambayo itawezesha makundi haya kushiriki moja
kwa moja katika shughuli za uzalishaji kupitia uwezeshwaji wa mkopo huu bila dhamana,
hatua ambayo itakuwa imeondoa ile kadhia ya vijana na wanawake kutokukopesheka
katika taasisi mbalimbali za kifedha kwa kukosa dhamana.
Haya yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa EFTA,
Bwana Nicomed Bohay wakati alipokuwa akiutambulisha mpango huu wa mkopo wa Kuku
kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini, katika hafla iliyofanyika katika
kiwanda ya kuzalisha kuku cha Silverland kilichoko USA-River jijini Arusha.
Bohay amesema, mpango huu wa mkopo wa kuku kwa vijana
na wanawake bila dhamana pamoja na kuunga mkono jitihada za serikali lakini
unakwenda sambamba na malengo ya uanzishwaji wa taasisi yake wa kuwawezesha
wajisiriamali na wakulima na hususani kutoka katika makundi hayo kujikwamua
kiuchumi kupitia mikopo ya EFTA inayotolewa bila dhamana.
“Vijana na wanawake wengi hawakopesheki katika taasisi
zetu za kifedha kwa sababu wengi wao hawana dhamana ya kuwawezesha kupata
mikopo hiyo, ndio maana sisi baada ya kuiona changamoto hii, tuliamua kuja na
mpango wa kuwakopesha vifaranga vya kuku bila dhamana, Na tumechagua kuku kwa
sababu uwekezaji wake ni wa muda mfupi na mkopaji ndani ya miezi michache
anaanza kuona matunda ya uwekezaji wake”
“Kwa mfano kwa kuku hawa tunaowakopesha wakopaji
wataweza kuanza kuwauza baada ya siku sitini, hii ni aina ya uwekezaji ambao
unaweza kuona matunda yake ndani ya muda mfupi na ndio maana tunawahimiza
vijana wengi na wanawake wajitokeze kuchangamkia fursa hii” amesema Bohay.
Bohay ameongeza kuwa katika mwaka wa kwanza wa mpango
huu EFTA inategemea kutoa mkopo wa kuku 250,000 nchi nzima, ambapo mpaka sasa
wamekwisha kabidhi zaidi ya Kuku 30,000 kwa wafugaji kutoka maeneo mbalimbali
nchini.
“Tayari tumeanza mafunzo kwa wafugaji walio tayari
kukopa na kwa waliohitimu mafunzo tayari tumeisha wakabidhi katika awamu ya
kwanza ambayo wafugaji takribani 30, wamenufaika kwa kupata mkopo wa kuku zaidi
30,000. Hivyo niwahimize vijana wengi zaidi wajitokeze mikopo hii ni kwa ajili
yako” Amesisitiza Bohay
Kwa kushirikiana na wazalishaji wa vifaranga vya kuku
kama vile Silverland Ltd, na wengine EFTA itamwezesha mkopaji kupata mahitaji
yote muhimu kama vile chakula, madawa na vifaa mbalimbali kama mkopo kwa wakati
wote mpaka atakapokuwa tayari kuwapeleka kuku wake sokoni.
Kwa upande wake Meneja Masoko wa Silverlands Ltd, Bi.Mwanamvua
Ngocho, ambao ni mojawapo wa wazalishaji wa vifaranga vya kuku ambao EFTA
itashirikiana nao katika mpango huu kuhakikisha wafugaji wanapata vifaranga
bora, chakula na chanjo ili kumhakikishia mfugaji anapata matokeo chanya kwa
wakati.
"Hapo awali, wateja wetu walikuwa wafugaji wenye
uzoefu na mitaji mikubwa. Lakini sasa, kwa ujio wa EFTA, fursa zaidi kwa vijana
na wanawake zitafunguka, na sisi kwa kweli tuko tayari kuhakikisha kwanza
tunatoa mafunzo makini ya namna ya kufuga kisasa, lakini pia kuzalisha
vifaranga vya kuku vyenye ubora zaidi," alibainisha Ngocho.
“Tunatamani kuona watu wetu wanaimarika kiuchumi kwa
kuwa wafugaji wa kuku, lakini pia afya ya jamii yetu ikiimarika zaidi kwa kula
nyama na mayai ya kuku bora kutoka kwa wafugaji wetu, Na hii sasa ndio fursa
ambayo naamini hakuna kijana wala mwanamke anaehitaji kujiajiri ataiacha impite”
ameongeza Ngocho
Kwa upande wake kaimu katibu tawala msaidizi mkoa wa
Arusha anaeshughulikia Uchumi na Uzalishaji, Bwana Daniel Loroku, ameishukuru taasisi
ya EFTA na kampuni ya Silverland kwa kuja na mpango huu wa kusaidia vijana na
wanawake kupitia mikopo ya vifaranga vya kuku bila dhamana.
“Jukumu la serikali ni kuona kila mmoja wetu wetu
anashiriki katika ujenzi wa taifa kwa kuchangia pato kupitia shughuli
mbalimbali za kiuchumi tunazozifanya, hata hivyo changamoto ya mitaji kwa
baadhi ya watanzania imekuwa ni kikwazo cha wao kuwa sehemu ya wachangiaji wa
pato la Taifa” Amesema Bwana Loroku.
“Ujio wa EFTA na aina hii mpya ya mkopo wa vifaranga
vya kuku bila dhamana, kwa kweli kwetu kama serikali ni fursa muhimu sana maana
itasaidia kuwezesha kundi hili la vijana na wanawake kuweza kujikwamua kiuchumi
maana sasa wataweza kuwa na shughuli za kufanya na ambazo zitawapatia kipato
ndani ya muda mfupi” Ameongeza Bwana Loroku
Kwa upande wake Flora Danford Sando, mmoja wa
wanufaika wa mpango huu, anaelezea namna ambayo fursa hii itakavyomsaidia
katika kuyabadili Maisha yake na hasa baada ya kutafuta ajira kwa muda mrefu
bila mafanikio.
"Baada ya kuhitimu masomo yangu, nilitafuta
ajira, lakini kwa Bahati mbaya sikufanikiwa kupata kazi. Nilijaribu pia
kutafuta mikopo katika mabenki ili nianze biashara lakini huko nako
sikufanikiwa maana nilitakiwa kuwa na dhamana, Nikiwa katika hali ya kukata
tamaa ndio nikapata Habari za uwepo wa mkopo huu kutoka EFTA bila dhamana”
Anasimulia Sando
“Haraka sana niliwatembelea EFTA na wakanielezea
taratibu zao ambazo nilizifuata, na baada yapo walinipeleka Iringa katika Chuo
cha Ufugaji wa Kuku cha Silverlands, ambapo nilipata elimu ya namna bora ya
kufuga kuku kisasa, Na leo Nimekabidhiwa rasmi vifaranga zaidi ya miatano
ambavyo nitavifuga kwa siku 60, na kisha nitaviingiza sokoni, ambapo baada ya
kuuza ndio nitakuja kulipa mkopo wangu” anaeleza Frola kwa furaha.
Mpango huu wa mkopo kwa wafugaji wa kuku nchini
utakuwa ni sehemu ya mwarobaini wa changamoto ya ajira kwa vijana na wanawake
maana utatoa fursa nyingi kwa vijana kujiajiri na hivyo kuwafanya vijana wengi
kuwa sehemu ya wachangiaji katika uchumi wa Taifa.
No comments:
Post a Comment