HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 24, 2024

BALOZI FATMA AKUTANA KWA MAZUNGUMZO NA JUMUIYA MBALIMBALI NCHINI OMAN

Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Mohammed katika picha ya pamoja na Uongozi wa Jumuiya ya Al-Wadood Charitable Group Sheikh Abdulqadir Al-Jahdhamy (wa kwanza kulia) katika Ofisi za Ubalozi Oman 

Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab katika picha ya Pamoja na Uongozi wa Jumuiya ya Maimamu wa Kitanzania ulioongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Sheikh Zubeir Nkwavi
Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Rajab akimkabidhi nyaraka kiongozi wa Jumuiya ya Maimamu wa Kitanzania ukiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Sheikh Zubeir Nkwavi.

BALOZI wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Mohammed amekutana kwa nyakati tofauti na Viongozi wa Jumuiya ya Maimamu wa Kitanzania waliopo Oman pamoja na Uongozi wa Jumuiya ya Al-Wadood Charitable Group ya Oman waliomtembelea ofisini kwake jijini Muscat hivi karibuni.

Pamoja na mambo mengine, Jumuiya hizo zilimtembelea Balozi Fatma kwa lengo la kujitambulisha kwake rasmi baada ya kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchini humo pamoja na kuwasilisha maoni ya Jumuiya hiyo kuhusu ajira zao nchini Oman na changamoto wanazokabiliana nazo

Katika taarifa yao, maimamu wa kitanzania wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Sheikh Zubeir Nkwavi waliwasilisha maoni kuhusu ajira zao nchini humo na changamoto wanazokabiliana nazo. Walieleza kuwa, Jumuiya hiyo ambayo ilianzishwa rasmi mwaka 2020 imefanikiwa kusajili wanachama 88 wakiwemo maimamu na walimu katika misikiti mbalimbali nchini Oman.

Pia Jumuiya hiyo imefanikiwa kuendesha shughuli mbalimbali ikiwemo kusaidiana wakati wa misiba, kutoa michango wakati wa maafa, kuendesha mafunzo ya dini na kuanzisha mfuko wa akiba nchini humo.

Alisema kuwa pamoja na mafanikio hayo, Umoja huo unakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa Bima za Afya kwa wanachama wake, kukosa mlezi wa Jumuiya na kukosa udhamini wa masomo na kumuomba Mhe. Balozi Fatma kuwasaidia kutafuta suluhu ya changamoto hizo kwa kushirikiana na Serikali ya Oman.

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Fatma aliwashukuru Viongozi hao na kuwapongeza kwa kufanikiwa kupata ajira nchini Oman na hivyo kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini Tanzania.

Kuhusu mikataba ya ajira alisema ipo haja ya kuwepo makubaliano baina ya Taasisi za Kidini za nchi mbili hizi ili kuwa kuweka mustakbali mzuri wa ajira zao.

Kadhalika Balozi Fatma aliwaahidi viongozi hao kuwa, atazungumza na Mamlaka husika za nchini Oman katika kutafuta suluhisho kwa changamoto zinazowakabili pamoja na kusisitiza umuhimu wa kuwa na mikataba rasmi ya ajira ili kupata haki zinazostahili ikiwemo bima ya Afya, likizo na stahiki nyingine.

Kwa upande wao, Jumuiya ya Al-Wadood Charitable Group ambayo inajihusisha na utoaji wa misaada kwa watu wenye mahitaji, wajane, wasiojiweza na yatima hapa nchini ikiongozwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Sheikh Abdulqadir Al-Jahdhamy waliwasilisha taarifa na mipango yao ya mwaka kuhusu utoaji wa misaada hiyo.

Naye Mhe. Balozi Fatma ameishukuru Jumuiya hiyo kwa misaada yao nchini na kuwaomba kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kusaidia miradi mbalimbali ya kupunguza umasikini na ukali wa maisha kwa Watanzania. Pia amewaomba kusaidia kujenga mabweni katika mikoa yenye uhitaji hususan kwa wanafunzi wa kike.

Jumuiya ya Al-Wadood Charitable Group pia imekuwa ikishiriki katika ujenzi wa misikiti, kutoa vifaa tiba, kuchimba visima na kugharamia masomo kwa Watanzania katika mikoa mbalimbali nchini


Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Fatma Mohammed akimkabidhi nyaraka Mwenyekiti wa Jumuiya ya Al-Wadood Charitable Group Sheikh Abdulqadir Al-Jahdhamy

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad