HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 18, 2023

Shirika la Bima Zanzibar Lashinda Tuzo

 


SHIRKA la bima la Zanzibar ( Zanzibar Insurance Corporation (ZIC) limeshinda tuzo ya Pacesetters Awards katika kutambua mchango wake wa kutoa huduma kwa Watanzania.

Tuzo hizo zimetolewa na Jubilant Stewards of Africa na kushirikisha makampuni mbalimbali ya ndani na nje ya nchi katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Akiongea baada ya kushinda tuzo hiyo, Afisa Masoko na Uhusiano wa Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) Mohamed Shaaban amesema tuzo hiyo inaonyesha ni kwa namna gani wanatoa huduma bora za kuwakinga watu na majanga yasiyotarajiwa.

Pia ametoa ushauri kwa watu kuwa na utamaduni wa kukatia bima vyombo vya moto yakiwemo magari bila kusahau umuhimu wa kukatia bima nyumba na biashara zao zinazowaingizia vipato kuendesha maisha yao.

Amesema hii itawasaidia kuepukana na majanga ya moto yasiyotarajiwa.

”Kwa maisha ya sasa, bima zote zina umuhimu, zikiwemo bima za majumbani, bima dhidi ya wizi, bima ya kusafirisha mizigo na nyinginezo,”

”Tumeshuhudia wafanyabiashara wakipoteza mitaji yao pale inapotokea majanga ya moto au wizi kwa sababu ya kutokata bima,”amesema Shaaban.

Tuzo hizo zilishirikisha makampuni mbalimbali ndani na nje ya nchi, ambayo yalipewa tuzo katika kutambua mchango wao wa kutoa huduma kwa wananchi.

Akiongea katika tuzo hizo zilizoandaliwa na Jubilant Stewards of Africa, Dr.John Shusho, mgeni rasmi ambaye ni Balozi wa Amani amesifu jitihada za makampuni mbalimbali katika kuleta mabadiliko ya uchumi kupitia ushindani wa kibiashara na utoaji huduma bora.

Ameyataka makampuni hayo kutumia ubunifu unaotokana na ukuaji wa teknolojia ili kuendelea kuwa na ushindani katika soko la dunia.

”Wakati tunafurahia maendeleo tuliyonayo, ni lazima tutambue kuwa uongozi bora hupelekea ukuaji wa uchumi kupitia uwajibikaji, uwazi na utoaji maamuzi sahihi,” amesema.

Pia ameyataka makampuni hayo kurudisha sehemu ya faida yao katika jamii, akisema kuwa ukuaji wa biashara haupimwi kupitia faida kubwa pekee, bali kupitia michango mbalimbali inayotolewa na makampuni hayo katika kuleta mabadiliko ya jamii.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad