HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 27, 2023

TUME YA MIPANGO SHIRIKISHENI WANANCHI UANDAAJI DIRA YA MAENDELEO YA TAIFA 2050 - DKT.BITEKO

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Mhe. Dkt. Doto Biteko ameiagiza Tume ya Mipango nchini kuweka uratibu wa ushiriki wa makundi mbalimbali ya wananchi na Wadau wengine katika kutoa maoni kwenye mchakato unaoendelea wa uandaaji  Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
 
Amesema hayo wakati akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa,katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano la kwanza Wanamipango 2023 iliyofanyika tarehe 27 Novemba 2023 jijini Arusha.
 
"Tume ya Mipango hakikisheni Wananchi wote wanashiriki kikamilifu kutoa maoni yao kuhusu Tanzania wanayoitaka katika miaka 25 ijayo, maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 
yameanza na kutokana na umuhimu wa Dira kwa Taifa letu, wanamipango na wadau wote ni muhimu kila mmoja 
kwa nafasi yake ashiriki kikamilifu katika hatua zote za maandalizi kama atakavyohitajika." Amesisitiza Dkt. Biteko
 
Suala jingine alilosisitiza ni kwa Maafisa Mipango kubadilika na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya Miradi na Programu zote zinazotekelezwa katika maeneo yao ikiwemo zinazofadhiliwa na Wadau wa Maendeleo badala ya ile inayogharamiwa na Serikali Kuu au Halmashauri pekee.
 
Vilevile, Dkt. Biteko ameelekeza Wakurugenzi wa Mipango kuzingatia utamaduni wa kuwa na mawazo ya pamoja katika kupanga mipango ya Serikali na nchi kwa ujumla ili kuleta mipango imara itakayosaidia Taifa kufikia uchumi wa juu.
 
Suala jingine alilosisitiza Dkt. Biteko ni Wanamipango waliopewa jukumu la kusimamia miradi pamoja na ufuatiliaji na tathmini kuzingatia utaratibu wa kutoa taarifa za utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo inayotekelezwa.
 
Sanjari na hayo, Dkt. Biteko amesema kuwa, Shughuli za tathmini na ufuatiliaji ni muhimu nchini hivyo zinapaswa kupewa kipaumbele cha kutengewa rasilimali za kutosha.
 
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, amewataka Maafisa  Mipango kuona thamani ya kada yao na wahakikishe kuwa wanakuwa wafuatiliaji wakubwa katika upangaji wa mipango kutoka ngazi ya chini hadi Taifa, kwa ajili ya manufaa ya nchi. 
 
Vilevile, amewaagiza Wakurugenzi wa Sera na  Mipango kuhakikisha kuwa  wanaweka mipango inayotekelezeka kwa manufaaa ya nchi kiuchumi.
 
Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa,  Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na 
Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad