HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 21, 2023

TRA Kuongeza Waendeshaji Uchumi Walioidhinishwa, Kurahisisha Mchakato wa Uondoshaji bidhaa

 

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata akizungumza leo Novemba 21, 2023 wakati wa kufungua mkutano wa wafanyabiashara, wenye viwanda, wamiliki wakampuni za Mafuta, Waingizaji na wanaotoa bidhaa nchini na wasafirishaji kwa kutumia viwanja vya ndege na bandari kwa lengo la kupunguza gharama za uondoshaji wa bidhaa hapa nchini.
Kaimu Kamishna wa Forodha kutoka TRA, Juma Hassan akizungumza leo Novemba 21, 2023 juu ya faida za kujiunga na mfumo wa AEO wakati wa kufungua mkutano wa wafanyabiashara, wenye viwanda, wamiliki wakampuni za Mafuta, Waingizaji na wanaotoa bidhaa nchini na wasafirishaji kwa kutumia viwanja vya ndege na bandari kwa lengo la kupunguza gharama za uondoshaji wa bidhaa hapa nchini.

Na Mwandishi wetu, Michuzi Tv
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) iko imara katika kubadilisha mazingira ya biashara kwa njia ya kidijitali, kuwezesha biashara na kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa kuongeza Waendeshaji Uchumi Walioidhinishwa na Mamlaka hiyo.

Hayo yamesemwa leo Novemba 21, 2023 na Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata wakati wa kufungua mkutano wa wafanyabiashara, wenye viwanda, wamiliki wakampuni za Mafuta, Waingizaji na wanaotoa bidhaa nchini na wasafirishaji kwa kutumia viwanja vya ndege na bandari. Amesema kuwa moja ya mipango ya TRA ni kusajili Wafanyabiashara kama Waendeshaji Uchumi Walioidhinishwa (AEO).

Amesema mpango huo unalenga kurahisisha mchakato uondoshaji wa bidhaa katika viwanja vya ndege nchini na Bandarini.

“Kwa kuwa AEO, unaweza kufaidika kutokana na vivutio vya upendeleo, ikijumuisha kibali cha haraka na madirisha mahususi ya kuwezesha, upunguzaji wa muda na gharama zinazohusiana na kufanyabiashara.” Amesema Kidata.

Aidha, Kidata amesema kuwa kwa TRA kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali zinazosimamia matakwa ya udhibiti wakati wa uingizaji na usafirishaji nje ya nchi bidhaa wataanzisha Mkataba wa Kutambuana (Mutual Recognition Agreement -MRA) ambao utaongeza hamasa katika mashirika yote ya serikali, kuhakikisha mchakato wa kibali.

Amesema muhimu kutambua kuwa dhamira ya TRA haiishii kwenye mipaka ya nchi yetu ni wawezeshaji waliojitolea kwa jumuiya ya wafanyabiashara wa Tanzania wanaotafuta upatikanaji wa masoko ya kikanda ya COMESA, SADC, na EAC.

Kwa Upande wa Kaimu Kamishna wa Forodha kutoka TRA, Juma Hassan amesema leo wamekaa na viongozi wa wenye viwanda na wafanyabiashara wanaotumia bandari ya Dar es Salaam na viwanja vya ndege kutoa na kuingiza bidhaa nhini kwaajili ya kuwapa elimu juu ya mfumo wa wafanyabiashara kama Waendeshaji Uchumi Walioidhinishwa (AEO).

“Lengo la kuwatambulisha Mfumo huo wa Waendeshaji uchumi walioidhinishwa (Authorized Economic Operators- AEO) kwaajili ya kuwatambua na kuwapa zawadi wafanyabiashara ambao ni waadilifu kwenye kazi zao na wapate faida zinazoendana na uadilifu wao, tumewaalika wenye viwanda, wamiliki wa kampuni za Mafuta, Waingizaji na wanaotoa bidhaa nchini na wasafirishaji ili waweze kujiunga katika mfumo.” Amesema

Akizungumzia faida wanazoweza kupata wafanyabiashara hao amesema kuwa ni kurahisisha utoaji wa mizigo kwani utaratibu wake ni mrefu na unachukua muda mwingi, katika mfumo huo unaweza kupata urahisi zaidi kwa kuruka baadhi ya hatua za uondoshaji bidhaa.

Ametaja hatua ambazo mfanyabiashara anaweza kuruka wakati wa uondoshaji bidhaa bandarini na kwenye viwanja vya ndege ni katika ukaguzi wanyaraka, kama unajulikana ni mwadilifu katika utendaji wako, ukaguzi mrefu wa nyaraka unapungua kuna baadhi ya hatua unaweza usikaguliwe.

Amesema kuwa tayari wafanyabiadhara 29 wameshasajiliwa kwenye mfumo lakini malengo ni kufikisha wafanyabiasha 100 hadi kufikia Juni 2024.

Amesema anatamani waingie wengi zaidi kwenye mfumo huo ili waweze kupunguza msongamano katika maeneo ya viwanja vya ndege na bandari.

"Mfanyabiashara atakayeingia kwenye mfumo huo anafursa ya kujipunguzia gharama za biashara kwasababu mzigo unapokaa bandarini siku moja maana yake ni gharama kwake, kwahiyo akiingia anaweza kupunguza gharama na kuongeza faida kwenye biashara yake, anauwezo wa kushindana na biashara za nje ya nchi kwa sababu yeye anakuwa nauwezo wa kufanya biashara kwa gharama za chini kuliko washindani wenzake waliopo nchini na waliopo nje ya nchi." Ameeleza faida za kujiunga na mfumo huo.

Kwa Upande wa rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Edward Urio wamemshukuru Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata kwa kuonesha ushirikiano kwenye kila jambo linalokuja kwenye masuala ya kodi.

Amesema kuwa Mpango wa Waendeshaji wa Uchumi walioidhinishwa (AEU), ulianzishwa 2010 lakini hatukuwa na uelewa wa kutosha ili watu waweze kutumia kama njia moja wapo ya kupunguza gharama za uagizaji mizigo kupitia wafanyabiashara wenye viwanda na wazalishaji.

“Ujio wa mfumo huu umeleta faida kwani tulikuwa tukienda kwenye mikutano ya kikanda na Afrika Mashariki, Tanzania tulikuwa na watu wa chache sana, utasikia Tanzania tuna AEO wasiozidi watatu, lakini ukisikia namba za nchi jilani ni kubwa kuanzia 200 na kuendelea." Amesema Urio

Ameeleza kuwa mwanzo huu tuliouanza umekuwa mzuri kwa kushirikiana na Trade Mark Africa umefikisha wafanyabiashara 29 mpaka sasa na bado milango inafunguliwa ili watumiaji wawe wengi na waweza kujiunga kwenye mfumo huo.

“Mfumo wa AEO ni unasaidia kupewa huduma kwa kipaumbele kwenye masuala ya kiforodha kwenye Masuala ya Kikodi na Masuala ya kutoa huduma kwenye taasisi za serikali kwa mfano kama sehemu ulitakiwa kupanga foleni ukifika pale unakuwa sio mtu wa kupanga foleni na unachukiliwa kama mlipa kodi bora, mlipakodi anayelewana na TRA.” Ameeleza

Amesema kuwa Mfumo huo utasaidia kuhuisha, kuchakata na kushughulikia nyaraka kwa waagizaji wakubwa wa bidhaa hasa kwa wenye viwanda, kwani gharama kubwa kwenye masuala ya forodha zinamwendea mlaji wa mwisho.

"Ushirikiano wa TRA na Trade Mark Africa ni naimani kwamba matunda yake yatazidi kuonekana kwa wenye viwanda kupunguza gharama na kuvutia bandari ya Dar es Salaam kuongeza mzigo kwa sababu muda wa uondoshaji bidhaa utakuwa umepungua.”

Mkurugenzi wa Kampuni ya Dow Elef International-Tanzania Ltd, Emmanuel Kazimoto ametoa rai kwa wafanyabiashara mwengine kujiunga na mfumo wa uondoshaji wa mizigo bandarini na katika viwanja vya ndege kwani unapunguza gharama na muda ya Uondoshaji mizigo.

Kwa Upande wa Mkurugenzi wa Motisun Group, Ratish Kamania amesema, kuwa mmoja wa Waendeshaji wa Uchumi walioidhinishwa (AEU), umewasaidia katika kupunguza gharama.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Dow Elef International-Tanzania Ltd, Emmanuel Kazimoto akizungumza leo Novemba 21, 2023 mara baada ya kupata uelewa juu ya mfumo wa AEOkwa lengo la kupunguza gharama za uondoshaji wa bidhaa hapa nchini.
Mkurugenzi wa Motisun Group, Ratish Kamania akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 21, 2023 juu ya faida za kujiunga na mfumo wa AEO wakati wa kufungua mkutano wa wafanyabiashara, wenye viwanda, wamiliki wakampuni za Mafuta, Waingizaji na wanaotoa bidhaa nchini na wasafirishaji kwa kutumia viwanja vya ndege na bandari kwa lengo la kupunguza gharama za uondoshaji wa bidhaa hapa nchini.








Picha za Pamoja.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad