HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 22, 2023

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kuongoza mapambano dhidi ya saratani.

 Na Zuhura Rashidi,Dar es Salaam.

WAKATI hali ya ugonjwa wa saratani ikizidi kuwa mbaya, Rais Mstaafu wa Awamu ya nne, Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, amejitolea kuongoza kampeni yenye lengo la kuhamasisha mapambano ya ugonjwa huo huku watanzania wakitakiwa kujitokeza mapema kupima saratani pale waonapo viashiria vya ugonjwa huo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa mkutano na baadhi ya viongozi wa dini, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi inayojishughulisha na masuala ya afya ya Gezi Health Initiative, Dk. John Zomola alisema, mkutano huo ulikuwa na madhumuni ya kujadili mikakati ya pamoja ya namna bora ya kupambana na janga hilo.

“Baada ya kuona hali halisi katika kuangalia namna gani nzuri ya kuwasaidia watanzania wenzetu kupambana na saratani, tuliamua kuja na mpango kazi wa kupambana na kudhitibi ongezeko la saratani nchini na ndipo tulipoamua kwenda kumuomba Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete akiwa mmoja wa wahanga wa ugonjwa huo aweze kutusaidia katika mapambano haya.

“Mheshimiwa Rais Kikwete ndiye atakayetuzindulia mpango mkakati wetu hapo Januari 18 mwakani, anapenda kuona mabadiliko, anapenda kuona watu wakitibiwa, sababu ana uzoefu wa ugonjwa huu kwa kupitia yeye mwenyewe, hivyo ameamua kushirikiana nasi na wadau mbalimbali, ili tupige kelele pamoja, tupambane kwa pamoja dhidi ya ugonjwa wa saratani”, alisema Dk. Zomola.

Akizungumza zaidi kuhusu kampeni hiyo, Dk. Zamola alisema pamoja na mambo mengine itasaidia kuongeza uelewa wa saratani katika jamii hasa kwa walio vijijini, kuboresha rufaa kwa wagonjwa ili wapate matibabu mapema, uboreshaji wa sera za matibabu ya saratani, kuboresha ushirikiano katika sekta mbalimbali, kuboresha mfumo wa kumbukumbu za wagonjwa, kuimarisha tafiti na kuwawezesha wataalamu wa saratani wa kada mbalimbali kimafunzo.

“Tokea tumeanzisha harakati hizi Novemba mwaka jana tumeshirikiana na taasisi za umma na binafsi, taasissi zote zinazohusiana na saratani,na sasa tumeona ni vyema kuwashirikisha ninyi ndugu zetu watumishi wa Mungu.

“Tunafarijika sana kuwa nanyi watumishi wa Mungu katika mapambano haya, ninyi pia ni madaktari wenzetu, mnatibu watu wengi kwa kupitia imani, hata matibabu tunayofanya hospitali kama hakuna imani hakuna uponyaji”, alisema.

Aidha alisema Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imepiga hatua mahususi na za haraka kwa kununua mashine muhimu kabisa za uchunguzi na ugunduzi wa saratani nchini hivyo juhudi za taasisi ya Gezi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zinahitaji sana katika kuongeza nguvu kukabiliana na saratani.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Daktari Bingwa wa magonjwa ya saratani na mmoja wa wakurugenzi wa taasisi ya Gezi, Dk. Hellen Makwani aliwataka watanzania Kuwahi kwenda kupima endapo wataona aina yoyote ya uvimbe ama changamoto yoyote ya kiafya ambayo hawakuwa nayo kabla na kuacha mara moja matumizi holela ya dawa bila kufuata ushauri wa madaktari.

“Utumiaji holela wa madawa unachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la saratani na tatizo figo nchini, lakini pia matumizi holela ya dawa za kienyeji na kutokufuata kanuni za usalama katika matumizi ya madawa ya kilimo mashambani na usalama kwa wafanyakazi wa vituo vya mafuta.

“Hali ya saratani ni mbaya sana, takwimu zinaonesha kuwa tunapokea wagonjwa wapya zaidi ya 40,000 na vifo zaidi ya 27,000 kwa mwaka, huku tafiti zikionesha kuwa endapo hakutachukuliwa hatua stahiki hadi kufikia mwaka 2030, takwimu zitakuwa mara mbili ya ilivyo sasa.

Pamoja na hayo alisema, saratani inayoongoza kwa wanawake ni ya shingo ya kizazi na matiti, huku saratani ya tezi dume kwa upande wa wanaume, akitanabaisha kuwa saratani za matiti na tezi dume zikisababishwa na mfumo wa maisha ilihali saratani ya shingo ya kizazi ikisababishwa na maambuzi ya muda mrefu ya kirusi kiitwacho ‘human papilloma’.

“Tukishirikiana pamoja kama jamii, watumishi wa Mungu, sisi madaktari, Wizara ya Afya, taasisi mbalimbali kama Muhimbili, Ocean Road, Bugando, Mbeya tunaweza kuleta mabadiliko, naiasa jamii, tuchunguze afya zetu tusisubiri kuumwa", aliongeza Dk. Hellen.

Naye Rais wa Baraza la Mitume na Manabii Tanzania, Nabii Joshua Aram Mwantyala alisema wamepokea ujumbe wa mapambano ya saratani kwa uzito mkubwa na ataongoza mapambano hayo nchini kote katika kutoa elimu na hamasa kwa watanzania kujitokeza mapema kupima afya zao.

“Natoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake za kuchukua hatua za moja kwa moja kukabiliana na saratani, Mitume na Manabii baraza letu limeenea kila wilaya, kwa kushirikiana na taasisi ya Gezi tutaendeleza mapambano haya katika kuhamasisha wananchi kufuata miongozo yote inayotolewa na wataalamu wa saratani katika kukabiliana na ugonjwa huo", alisema Rais Nabii Joshua.

Awali Balozi wa Saratani nchini mbaye pia ni Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ukombozi, Nabii BG Malisa aliwashauri watanzania kubadilisha mfumo wa maisha katika namna ya ulaji na kufuata malekezo ya wataalamu wa afya.

“Semina hii imekuwa ya baraka sana, mimi kama Balozi nitashirikiana na taasisi ya Gezi katika kuhakikisha elimu hii inaenea nchi nzima kwa haraka zaidi kuelekea siku ya uzinduzi rasmi wa kampeni yetu.

“Lakini pia nashauri turuhusu utaalamu na elimu ya afya uendelee kuenezwa katika nyumba za ibada, makanisani na misikitini, hatukatai kuamini, nimeshuhudia watu wanaponywa, lakini pia turuhusu elimu ya afya", anashauri Nabii Malisa.

Saratani ni uvimbe unaojitokeza mahali popote katika mwili wa binadamu, uvumbe huu unakuwa hauna maumivu yoyote katika hatua za awali, kuna saratani za aina nyingi kutegemea na mahali lilipo tatizo, kama vile saratani za shingo ya mfuko wa kizazi, matiti, tezi dume, koo, mfumo wa chakula, Ngozi, damu, mapafu, kibofu cha mkojo na nyinginezo.


Vifuatavyo vinaweza kuchochea uwezekano wa kupata saratani; pombe, sigara, madawa, mtindo wa maisha na virusi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Gezi Health Initiatives, Dk. John Zomola (kushoto), akiwakaribisha baashi ya viongozi wa dini, wakati wa mkutano kujadili mikakati ya kupambana na janga la ugonjwa wa Saratani, uliondaliwa na taasisi hiyo, jijini Dar es Salaam jana.
Rais wa Baraza la Mitume na Manabii Tanzania, Nabii Joshua Aram Mwantyala (katikati), akizungumza katika mkutano huo, jinsi baraza hilo likivyoguswa na ujumbe wa mapambano dhidi ya saratani na jinsi walivyojipanga  kutoa elimu na hamasa kwa watanzania kujitokeza mapema kupima afya zao. 
Mshauri wa Taasisi ya Gezi Health Initiatives mdau wa afya, Vicent Manyilizu akiratibu mijadala mbalimbali iliyokuwa ikifanyika wakati wa mkutano huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Gezi Health Initiatives, Dk. John Zomola (kulia), akizungumzia mikakati ya taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini katika kukabiliana  na janga la ugonjwa wa Saratani, wakati wa mkutano huo, jijini Dar es Salaam jana.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya saratani na mmoja wa wakurugenzi wa taasisi ya Gezi, Dk. Hellen Makwani (kushoto), akitoa ufafanuzi wa kitaalamu kuhusu saratani kwa washiriki wa mkutano kuhusu namna bora ya kupambana na ugonjwa wa saratani, jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Gezi, Dk. John Zomola.
Rais wa Baraza la Mitume na Manabii Tanzania, Nabii Joshua Aram Mwantyala (katikati), akizungumza katika mkutano huo, jinsi baraza hilo likivyoguswa na ujumbe wa mapambano dhidi ya saratani na jinsi walivyojipanga  kutoa elimu na hamasa kwa watanzania kujitokeza mapema kupima afya zao. 
Balozi wa Saratani nchini mbaye pia ni Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ukombozi,  Nabii BG Malisa (kulia), akizungumza wakati wa mkutano huo. Alitoa rai kwa  watanzania kubadilisha  mfumo wa maisha katika namna ya ulaji na kufuata malekezo ya wataalamu wa afya ili kujikinga na saratani na magonjwa mengine yasiyoambukiza.
Baadhi ya viongozi na watumishi wa Taasisi ya Gezi pamoja na viongozi wa dini, wakipiga picha ya kumbukumbu muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano huo jijini Dar es Salaam jana. 


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad