Kuendeleza wasichana kielimu katika fani za sayansi ni jambo muhimu ambalo litaongeza ushiriki wa wanawake katika maendeleo ya viwanda nchini Tanzania.
Prof. Elifas Bisanda, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, ametanabaisha hayo katika kikao cha kamati cha masuala ya jinsia ya Chuo iliyoketi Novemba 13, 2023 makao makuu ya chuo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
“Tunaipongeza sana serikali yetu chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutoa ufadhili wa masomo ya Sayansi kwa wasichana wapatao elfu moja (1000). Tayari wasichana 141 waliopatikana awamu ya kwanza wameshaanza masomo kupitia ufadhili huo. Ni mafanikio makubwa nchini kwani tunakwenda kuongeza ushiriki wa wanawake katika maendeleo kupitia sayansi, hesabu, uhandisi, kilimo na teknolojia. Hivyo, tunawahimiza wenye sifa stahiki kutuma maombi yao kwa ajili ya awamu ya pili ili wadahiliwe na kuanza masomo yao na kunufaika na ufadhili wa asilimia 100.” Amesema Prof. Bisanda.
Aidha, ametoa rai kwa viongozi wa wilaya, watendaji wa kata na mitaa kushiriki katika kuipasha jamii habari hizi njema ili kuibua matumaini ya wasichana walioanza kukata tamaa ya kuendelea kielimu katika maeneo yao.
Ufadhili huo unahusisha wasichana waliokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupata ujauzito, ukatili wa kijinsia, umasikini, kuondokewa na wazazi na walezi na sababu nyingine zozote.
Ufadhili unatolewa kwa Watanzania wote kutoka bara na visiwani ikihusisha kulipiwa ada yote, kupewa vishikwambi, kupata malazi wakati wa mafunzo ya ana kwa ana, nauli na bima ya afya.
Aidha, sifa za kitaaluma ambazo mwanafunzi husika anatakiwa kuwa nazo ni:
(a) Awe mhitimu wa kidato cha sita mwenye ufaulu wa angalau pointi 1.5 kwenye masomo mawili ya tahasusi za Sayansi, hesabu, uhandisi, kilimo na teknolojia.
(b) Mhitimu wa Stashahada katika fani za sayansi, hesabu, uhandisi, kilimo na teknolojia mwenye ufaulu wa GPA ya 2.9-2.0
(c) Mhitimu mwenye NTA level 5/Professional Technician level II Certificate
Waombaji wenye sifa tajwa wafike kwenye vituo vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambavyo vipo katika mikoa yote ya Tanzania bara pia Tanzania Visiwani (Unguja na Pemba) kujaza fomu za maombi.
Pia, maombi yanaweza kufanywa kwa muombaji kupakua fomu ya maombi kupitia www.out.ac.tz na kuijaza fomu hiyo kisha kuituma kupitia barua pepe ofpheet@out.ac.tz
Mwisho wa kupokea maombi ya awamu ya pili ni tarehe Novemba 30, 2023.
Wednesday, November 22, 2023
Home
Unlabelled
PROF. BISANDA: SERIKALI YATOA UFADHILI WA MASOMO YA SAYANSI KWA WASICHANA
PROF. BISANDA: SERIKALI YATOA UFADHILI WA MASOMO YA SAYANSI KWA WASICHANA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment