HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 24, 2023

NMB, CTM Tanzania wazindua mikopo ya kumalizia ujenzi

NA MWANDISHI WETU

BENKI ya NMB wamesaini makubaliano na Kampuni ya CTM Tanzania yaliyopewa jina la ‘Lipa Baadae,’ yatakayowawezesha wateja wa benki hiyo kupata mikopo ya fedha za manunuzi ya bidhaa za umaliziaji ujenzi wa nyumba ‘finishing,’ zinazouzwa na kampuni hiyo, huku wakinufaika na punguzo la asilimia 2 hadi 10.

Lipa Baadae ni mfumo utakaowawezesha wateja wa NMB na CTM kupata suluhu za kifedha kupitia mikopo ya kuboresha nyumba, kununulia bidhaa za kampuni hiyo bobevu kwa usambazaji na uuzaji wa marumaru ‘tiles’, vyoo, majakuzi, mabeseni ya kunawia na kabati za bafuni na vyooni, pamoja na ushauri wa vipimo vya ujenzi bure.

Hafla ya kusaini makubaliano hayo imefanyika Jumatano Novemba 21, katika Ofisi za CTM Tanzania zilizoko Barabara ya Mwai Kibaki, Kawe jijini Dar es Salaam, ambako NMB iliwakilishwa na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi huku CTM ikiwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wake Shiraz Satchu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mponzi alisema wanajisikia fahari kubwa na wanajivunia kuingia makubalino hayo na wauzaji hao wa bidhaa bora za nyumbani na hata ofisini, hivyo muunganiko wao unazikutanisha taasisi mbili bora na bobevu kwa masuluhisho ya kifedha na ujenzi kwa wateja wao.

“Leo tuko hapa kusaini ushirikiano na CTM ili kuwawezesha Watanzania kupata bidhaa bora kutoka kampuni hii. NMB tumekuwa vinara wa suluhishi za wateja, lengo likiwa ni kuwafanya wafurahie huduma zetu, ikiwemo mikopo ya ujenzi, kununua nyumba iliyokamilia, kuanza ujenzi au kumalizia.

“Badala ya mteja kufanya ujenzi kwa manunuzi ya kusuasua, Lipa Baadae inakupa wigo mpana wa kukopa pesa ili kununulia bidhaa za CTM, hivyo kutoka kununua bila mkopo, hadi kuingia katika manunuzi ya pamoja vifaa vyote na kulipa Baadae kwa riba nafuu mno, sambamba na ushauri wa vifaa na jinsi ya kujenga.

“Ushirikiano huu unaenda kumaliza changamoto wanazokabiliana nazo wateja wetu wakati wa ujenzi, na tofauti na aina nyingine za mikopo tuliyonayo NMB kwenye Sekta ya Nyumba kama nilivyoitaja hapo juu, Lipa Baadae utamuwezesha mteja kukopa hatua kwa hatua kulingana na mahitaji yake katika umaliziaji ujenzi.

“Huduma hii itapatikana katika matawi yetu yote kote nchini, mteja anaweza kufika CTM na kuchagua bidhaa kisha kuja NMB kukopa pesa, ama anaweza kuanza kuja kukopa kisha kwenda kufanya manunuzi na kurejesha mkopo wake taratibu kulingana na kipato chake,” alisema Mponzi na ku

Kwa upande wake, Satchu aliishukuru NMB kwa kufikia muafaka na kusiani makubaliano hayo kuhitimisha mchakato wa mazungumzo ya takribani miezi tisa, na kwamba wana uzoefu wa kutosha katika Sekta ya Ujenzi, ambako wanatimiza miaka 40 ya uuzaji na usambazaji wa bidhaa rafiki za ‘finishing’.

“Tumechakata suala hili kwa takribani miezi tisa, kuchambua na kutathmini mpaka kufikia hapa leo, lengo kuwezesha Watanzania kutimiza ndoto zao za kuishi katika nyumba bora na za kisasa, tukiamini kuwa thamani ya nyumba ni ujenzi na umaliziaji kwa kutumia bidhaa bora, ambazo ndio tulizonazo,” alisema Satchu.

Akaongeza ya kuwa CTM wana uzoefu wa miaka 40 katika uuzaji na usambazaji wa vifaa bora ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata vifaa bora kulingana na mazingira yake, kipato chake na malengo yake na kwamba hafla hiyo ni maalum kushuhudia muungano mpya na bora, unaojumuisha ushauri wa bure kwa wateja.

“Ujenzi wa Kitanzania unakabiliana na changamoto nyingi, zikiwemo za ujenzi holela, hasa katika maeneo yasiyo na vibali au hati miliki. Watanzania wanapawswa kubadilika na kujenga kisasa kwa kufuata sheria na kanuni, ili kuwa huru kujenga nyumba bora na za kisasa, pamoja na kuzikatia bima.

“Wengi wa Watanzania kipato chao ni kidogo, hivyo kujikuta wakinunua maeneo kiholela, na kukosa amani ya kujenga ama kuzifanyia maboresho ya thamani nyumba zao. Kupitia Lipa Baadae, CTM na NMB sasa tuko tayari kutoa ushauri kumuwezesha kila mtu kujenga na kuishi katika nyumba ya ndoto zake,” alisisitiza Satchu.






No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad