HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 24, 2023

Mkuu wa Chuo cha CATC amtembelea Katibu Mkuu wa CCM kumwelezea mikakati mbalimbali ya chuo hicho katika sekta ya usafiri wa anga Tanzania

 


Mkuu wa Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC) Bw. Aristid Kanje amemtembelea Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe.Daniel Chongolo na kufanya naye mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo chuo hicho ikiwemo mkakati wa kujenga majengo ya chuo kipya cha kisasa.

Mkutano huo ulifanyika Novemba 24, 2023 Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM Lumumba, ambapo Mkuu wa Chuo cha CATC alimweleza Mhe. Chongolo kwamba chuo hicho kinachotoa mafunzo ya muda mfupi katika sekta ya usafiri wa anga nchini ni miongoni mwa vyuo 9 barani Afrika na 35 duniani vinavyotambuliwa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani(ICAO) katika utoaji wa kozi za usalama katika usafiri wa Anga.

Mkuu wa Chuo Kanje alisema pia chuo hicho ni mwanachama kamili wa shirika linalosimamia Usafiri wa Anga Duniani yaani ‘ICAO TrainAir Plus Full Member (Gold)’ ambapo wahitimu wake wanaweza kufanya kazi mahali popote Duniani.

Kanje alisema miongoni mwa wateja wa chuo cha CATC ni pamoja na wamiliki wa viwanja vya ndege, mashirika ya ndege, Mashirika yanayotoa huduma katika viwanja vya ndege, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, Majeshi, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mabenki na watu binafsi.

Wateja wengine ni kutoka mataifa 16 Barani Afrika yakiwemo Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda, Msumbiji, Botswana, Somalia, Namibia, Eswatini, Guinea Conakry, Liberia, Sierra leone, Nigeria Sudan Kusini, Zambia, na Afrika Kusini.

Kanje alisema chuo hicho kinachotoa mafunzo kwa wastani wa washiriki elfu mbili kwa mwaka toka ndani na nje ya Tanzania kinakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa miundombinu ya kutolea mafunzo yenye hadhi ya kimataifa.

Mkuu wa Chuo CATC alisema Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ambayo ndiyo mmiliki wa CATC chini ya Wizara ya Uchukuzi ipo kwenye mkakati wa kujenga miundombinu ya kisasa katika eneo la Banana Ukonga.

Mkuu wa Chuo ametoa shukrani nyingi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TCAA kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa eneo la ekari 18 kwa ajili ya ujenzi wa Miundombinu ya kisasa ya Chuo hicho.

Mkuu wa Chuo ameongeza kwamba, upembuzi yakinifu ulibaini kwamba gharama za mradi huo zinakadiriwa kuwa kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 78 na kwamba tayari serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imeshatenga kiasi cha shilingi Bilioni tano za awali kwa mwaka wa fedha 2023/24 kuanza mradi huo.

Mkuu wa Chuo kanje alisema ujenzi wa chuo hicho cha Kisasa ni mojawapo ya vipaumbele vya Wizara ya Uchukuzi.

Mkuu wa Chuo ametoa pongezi kwa Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa Mnyaa, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu pamoja na Menejimenti ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ikiongozwa na Mkurugezi wake Mkuu Bw. Hamza Johari kwa kusimama kidete katika mchakato wa mradi huu wenye manufaa makubwa kwa Taifa kuingiza fedha za kigeni.

Kwa upande Katibu Mkuu wa CCM Chongolo alisema amefurahishwa sana kusikia habari za kina za CATC na kuongeza kwamba hata yeye anaona umuhimu wa chuo hicho nchini na amemhakikishia Mkuu wa Chuo kwamba utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati utafanikiwa.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo akizungumza na Mkuu wa Chuo cha Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC) Aristid Kanje kuhusu namna chama hicho kitakavyoweza kuchangia katika ujenzi wa Chuo cha CATC wakati wa kikao kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo akimsikiliza Mkuu wa Chuo cha Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC) Aristid Kanje alipokuwa anatoa maelezo kuhusu kozi mbalimbali zinazotolewa na Chuo hicho pamoja na mkakati wa kujenga majengo ya chuo kipya cha kisasa wakati wa kikao kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Chuo cha Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC) Aristid Kanje mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad