HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 10, 2023

DIWANI MAKURUMLA, HOSPITALI YA EKENYWA WASHIRIKIANA KUTOA HUDUMA ZA MATIBABU BURE KWA WANANCHI WILAYA YA UBUNGO

 

 Na Said Mwishehe, Michuzi TV


KATIKA kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi Diwani wa Kata ya Makurumla iliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam Bakari Kimwanga ameungana na Hospitali Bingwa ya Ekenywa kutoa huduma za matibabu bure kwa wananchi wa kata hiyo na halmashauri ya Ubungo kwa ujumla.

Huduma ya matibabu bure kwa wananchi hao imetolewa kupitia program maalumu iliyopewa jina la Afya Check yenye lengo la kuwezesha wananchi kupima afya bure na kupata matibabu ya kibingwa ambapo program hiyo itafanyika kwa siku mbili huku ikikadiriwa watu zaidi ya 2000 watapata nafasi ya kupatiwa matibabu na madaktari bingwa wa Hospitali bingwa ya Ekenywa.

Akizungumza kuhusu program hiyo Diwani wa Kata ya Makurumla Bakari Kimwanga amesema tamasha la Afya Check limelenga kupeleka huduma ya matibabu ya afya bure kwa wananchi wa Kata hiyo pamoja na kata nyingine nane zinazounda Halmshauri ya wilaya ya Ubungo.

Aidha amesema ofisi yake kwa kushirikiana na Hospitali bingwa ya Ekenywa wameona wawe na ushirikiano huo ambao wanaamini wanakwenda kusaidia jamii ya watu wa Makurumla na maeneo mengine yanayounda Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo

Amesema mwitikio kwa ujumla ni mkubwa kwani wananchi wengi wamejitokeza kwenye tamasha hilo kwa ajili ya kuwaona madakatari bingwa na wamepata huduma huku akifafanua wapo waliofanya uchunguzi wa macho, kisukari, shinikizo la damu na wengine wamekwenda kuwaona madaktari bingwa wa magonjwa ya Sikio,Pua na Kinywa.

“Pia wapo wananchi ambao wamekuja kuchangia damu na wengine wamekuja kuchunguza magonjwa ya akina mama.Kama tunavyofahamu sasa hivi jamii yetu imekuwa ikiteseka na suala la uzazi hivyo katika tamasha hili wananchi wamewaona madaktari bingwa wakiongozwa na Daktari Bingwa wa magonjwa ya akina mama na uzazi Murete Sanare Lukumay ambaye ameona akina mama.

“Kwa hiyo kwetu ni fursa kwetu kama wananchi wa kata ya Makurumla ambapo na sisi ni sehemu mojawapo tunaonufaika na uwekezaji thabiti na makini wa hospitali bingwa ya Ekenywa.Kutokana na umahiri wa utoaji huduma za kibingwa unaofanywa na hospitali hii kumuona daktari bingwa ni kati ya Sh.15000 mpaka Sh.40,000 lakini hapa wananchi wanawaona madaktari na kupata matibabu bure.”

Aidha amesema kwa wale ambao watabainika magonjwa waliyonayo yanahitaji rufaa hasa katika saratani ya Shingo ya kizazi watapelekwa Hospitali ya Ocean Road na wengine Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na ugonjwa husika na hatua uliofikia.

Amesisitiza katika siku mbili hizo wanakwenda kusaidia jamii kwa kuokoa maisha ya mamia ya wananchi wa Kata ya Makurumla pamoja na kata jirani.“Mkuu wa Wilaya wa Wilaya ya Ubungo wakati anazindua tamasha hili kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa ameeleza kwa kina mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha na kuimarisha sekta ya afya.

“Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo msaada mkubwa pamoja na kuupata kwenye hospitali za Serikali lakini kwa kiasi kikubwa tunaupata kupitia sekta binafsi kwasababu hao ndio wawekezaji wakubwa, kwa mfano tunayo hospitali ya Palestina lakini unapokuja kwenye magonjwa ya kibingwa lazima utakimbilia Hospitali Bingwa ya Ekenywa .

“Tumekuwa na ushirikiano mkubwa na hospitali ya Ekenywa kwani mara nyingi tunapokuwa na wagonjwa wamekuwa wakisaidia lakini kwa mwaka wametupa nafasi ya kutusaidia watu 30 lakini wakati idadi inaongezekana kulingana na mahitaji .Hivyo kwetu hospitali ya Ekenywa imekuwa kiunganishi muhimu cha kuwafikia wagonjwa,”amesema Kimwanga.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya akina mama na uzazi ambaye pia ni Daktari Mfawidhi wa Hospitali Bingwa ya Ekenywa Dk.Murete Lukumay amesema kauli mbiu katika tamasha la Afya Check inasema Jali afya yako, ishi ndoto yako huku akifafanua kuwa lengo kuu la tamasha hilo ni kuendelea kujitangaza kwa wananchi yaozunguka Kata hiyo.

Pia amesema hotuba nyingi zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imekuwa ikizungumzia kuhusu kuboresha afya za wananchi, hivyo wameamua kuunga mkono juhudi za Rais Dk.Samia kwa vitendo.

“Ndio maana tumeandaa tamasha hili na tumejipanga kuhudumia wananchi wote watakaofika hapa.Katika hospitali yetu tumekuwa tukipata wagonjwa zaidi ya 200 kwa siku kwa hiyo katika siku mbili hizi tumekadiria kwa siku tutahudumia wagonjwa 300 mpaka 500.”

Amefafanua wamekuwa wakihudumia magonjwa ya siki,pua na koo na kwa kina mama wamekuwa wakifanya uchunguzi wa saratani ya matiti pamoja na saratani ya shingo ya kizazi.Pia wamekuwa wakitoa elimu ya afya kuhusu lishe , elimu ya afya ya akili , hudma za chanjo, kupima afya ya VVU pamoja na magonjwa yasiyoyakuambukiza.

“Tumekuwa tukipata wagonjwa wengi kutoka nje ya Dar es Salaam hivyo tumeona tuwaambie wananchi wa Magomeni kuwa hizi huduma ziko hapa badala ya kuwanufaisha watu wa mbali,”amesema Dk.Lukumay.

Awali Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Hospitali Bingwa ya Ekenywa Dk.Peter Ole Lengine amesema katika tamasha hilo huduma zote wanazotoa ni bure na wanatoa huduma za mama na mtoto, huduma za pua, koo na masikio, magonjwa ya mayo pamoja na huduma nyingine za kibingwa.

Aidha amesema kupitia tamasha hilo wanaamini wataitangaza hospitali yao katika ngazi zote hasa Halmashauri ya wilaya ya Ubungo lakini pamoja na Magomeni ambako ndiko waliko .“tumeona tutangaze huduma zetu tena ili wananchi walioko jirani waje.”

Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam Hamish Komba( wa pili kulia) akishuhudia mmoja wa wananchi akipatiwa huduma ya matibabu ya Sikio kutoka kwa mmoja wa madaktari wa Hospitali Bingwa ya Ekenywa wakati wa tamasha la Afya Check linalofanyika Kata ya  Makurumla iliyopo Magomeni.Mkuu wa Wilaya Komba ameshuhudia utolewaji wa huduma ya matibabu kwa mgonjwa huyo kama ishara ya uzinduzi wa tamasha hilo la siku mbili.











 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad