HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 8, 2023

Benki ya Letshego Faidika yapata faida ya Sh1.3billion kabla ya kodi

 Benki ya Letshego Faidika ambayo ni muunganiko wa iliyokuwa taasisi ya kifedha ya Faidika (Faidika Microfinance) na Benki ya Letshego (Letshego Bank) imepata faida ya Sh1.3 billioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 234 kwa kipindi cha robo ya mwaka ya utendaji wake mpaka Septemba 30 mwaka huu.

Faida hiyo ni ya kwanza tangu taasisi hizo mbili kuunganishwa mwezi Juni mwaka huu ambapo mwaka 2022 katika kipindi hicho hicho walipata hasara ya Sh981 milioni huku robo ya awali ya mwaka 2023, kabla ya kodi, Letshego ilikuwa hasara ya Sh464 milioni.

Mafanikio katika utendaji wa benki hiyo mpaka kufikia robo ya kwanza yametokana na uwekezaji katika huduma bora na za kisasa na kufanya mageuzi chanya ya kifedha ndani ya robo moja tu.

Afisa Mtendaji Mkuu wa benki ya Letshego Faidika Bw Baraka Munisi alisema, "Tumefurahishwa na mabadiliko chanya ya faida kabla ya kodi katika kipindi kifupi. Baada ya muunganiko na kufanya kazi pamoja , sasa tunalenga kutumia faida za ufanisi mkubwa wa uendeshaji na nguvu kuelekea kutoa faida endelevu kwa wadau wetu."

Bw Munisi aliongeza kuwa baada ya muungano huo Juni mwishoni mwaka huu, mali jumla ya Benki iliongezeka kwa asilimia 213 hadi Sh108 bilioni ikilinganishwa na Sh34 bilioni katika robo ya pili ya mwaka 2023.

Alisema kuwa upande wa mikopo nayo iliongezeka kwa asilimia 465 katika kipindi hicho hicho hadi kufikia Sh 72.7 bilioni ikilinganishwa na Sh12.8 bilioni katika robo ya pili ya mwaka 2023.

“Katika kipindi kama hicho pia, robo ya tatu inayomalizika tarehe 30 Septemba 2023, amana za benki ziliongezeka kwa asilimia tisa ikilinganishwa na robo iliyopita,” alisema.

Kwa mujibu wa Bw Munishi kutokana na ukuaji wa kitabu cha mikopo na ufanisi wa ukusanyaji na kurejeshwaji, kiwango cha mikopo isiyolipika kwa benki kiliboreshwa kutoka asilimia 44 hadi 18 robo kwa robo wakati mali zenye faida kwa jumla ziliongezeka hadi asilimia 72 kutoka asilimia 59 robo kwa robo. Kiwango cha gharama kwa mapato kiliboreshwa hadi asilimia 83 kutoka asilimia 176 katika robo iliyopita.

Bw Munisi alithibitisha azma ya Benki ya Letshego Faidika kuwa moja ya benki za kati zinazoongoza nchini Tanzania katika kipindi cha miaka mitatu hadi mitano.

"Nina matumaini na nimehamasishwa kuhusu mustakabali wa benki yetu huku tukiendelea kuwa na lengo la kutoa utendaji endelevu pamoja na mifumo imara ya utawala wa kiwango cha dunia, kutoa thamani inayoweza kupimika na inayoweza kuhisika kwa wateja na wadau wetu wote.

“Nawapongeza wafanyakazi, wateja, wanahisa, Benki Kuu ya Tanzania, Tume ya Ushindani ya Haki, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na washirika wetu wa biashara kwa ushirikiano na msaada wao unaendelea,” alisema.

Alisema kuwa benki hiyo inaendelea kuwa na azma ya kujenga uthabiti wa biashara ili kukabiliana na changamoto za masoko yanayojitokeza na vile vile kuhakikisha kuwa inaendelea kuboresha maisha ya wateja na wanachama wa jamii kupitia bidhaa na huduma rahisi, nafuu, na zinazofaa.

"Nawashukuru wafanyakazi wote kwa kazi ngumu, uaminifu, na jitihada zisizochoka kwa miaka michache iliyopita kwa kufanikisha mchakato huu kwa Pamoja! Tuko hakika #TunaNguvuPamoja,” alisema Munisi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa benki ya Letshego Faidika Bw Baraka Munisi akisisitiza jambo wakati wa kutangaza utendaji wa taasisi hiyo wa mwaka mpya wa fedha na kuweza kupata faida bila kodi ya Sh1.3 bilionibila kodi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad