HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, October 29, 2023

WAZIRI WA ELIMU AELEZA SABABU ZA NIT KUPEWA FEDHA NYINGI MRADI WA EASTRIP

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akiwa katika chumba cha kujifunzia kuendesha ndege kilichopo chuoni NIT jijini Dar es Salaam. 

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema sababu ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kupewa fedha nyingi kutekeleza mradi wa Eastrip ni kutokana na umuhimu wa kozi wanazozitoa.

Amesema kuwa wanahitaji kuwa na wataalamu wa kutosha ili kutimiza mikakati ya nchi kwa kuwa sekta ya usafirishaji ni nyeti na ina mchango mkubwa kwa taifa.

Profesa Mkenda ameyasema hayo Dar es Salaam wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi mradi wa Eastrip.

Amesema kuwa "Tunahitaji kuwafundisha marubani wetu wenyewe ili kuongeza idadi yao lengo ni kuwawezesha na kuwapa fursa watanzania ambao hawana uwezo wa kifedha lakini wako vizuri kichwani kusoma."

Waziri huyo amesema kuwa chuo hicho kinatakiwa kutojifungia badala yake kuwapeleka wataalamu wao kwenda nje ya nchi kuongeza ujuzi katika masuala ya usafirishaji, nishati na gesi ili kujiandaa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Amesema sekta ya usafirishaji inachangia katika kuongeza watalii hivyo, wanatakiwa kuwafundisha vijana wao kukidhi mahitaji ya soko la ajira la ndani na nje.

Akizungumzia kuhusu mikopo ya diploma, amesema kuwa stashahada ni muhimu katika kupata mafunzo ya amali na nguvu kazi yenye ujuzi wa kutosha licha ya kwamba wanaonekana kutokuwa na thamani kama waliohitimu au kusomea shahada.

Amesema serikali imeona umuhimu wa stashahada hivyo ikatenga Sh bilioni 48 kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi 8000 wa ngazi hiyo ya stashahada kwa mwaka wa masomo 2023/24.

Alitaja fani za kipaumbele ambazo zitagharamiwa kuwa ni pamoja na afya na Sayansi shirikishi, Ualimu, usafiri na Usafirishaji, Uhandisi Nishati, Madini, Sayansi na Ardhi pamoja na Kilimo na mifugo.

Ameeleza kuwa lengo lao ni kuhakikisha wanazalisha wataalamu watakaoweza kufanya kazi popote duniani ili kukabiliana na tatizo la ajira.

"Kozi za diploma kwa chuo hiki cha NIT ambazo waombaji watapata mkopo ni katika Uhandisi wa Ndege, ujenzi na urekebishaji wa meli, ujenzi wa miundombinu ya reli na usafirishaji. Pia kwa watakaosomea uhandisi wa nishati ikiwemo mafuta, gesi na mabomba ya mafuta," amesisisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa NIT, Profesa Zacharia Mganilwa amesema chuo hicho kinatoa mafunzo ya diploma kwa kozi 25, shahada ya kwanza 19, shahada ya uzamili tatu na postgraduate tisa.

Amesema katika mradi huo wamejiandaa kupeleka wakufunzi kwenda nchi mbalimbali kusomea masuala ya reli, meli, usafirishaji na nishati ili waweze kuwa na leseni ya kufanya kazi katika miradi mikubwa iliyopo.

"Tumejiandaa kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kupata wakufunzi watakaowafundisha walimu wa hesabu katika vyuo vyote nchini. Tunahitaji wataalamu kwa ajili ya ndege za mafunzo tulizopokea," amesisisitiza

Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Estrip, Dk Robert Msigwa amesema kuwa walipokea Dola za Marekani 21,250,000 na kwamba wamefanikiwa kupeleka watumishi kupata ujuzi wa kufundisha katika maeneo hayo, kununua vitendea kazi ikiwemo magari na vitabu.

"Ujenzi wa mradi huu umefikia asilimia 55 na mabweni yamefikia asilimia 40. Kutokana na changamoto mbalimbali tunaomba kuomgezewa muda wa kununua vifaa vya ndege," amesema Dk Msigwa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda pata maelezo baada ya kutembelea mitambo mbalimbali alipotembelea Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) jijini Dar es Salaam.

Matukio mbalimbali Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alipotembelea  Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alipotembelea  Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na wafanyakazi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) jijini Dar es Salaam.
No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad