HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 10, 2023

WAKULIMA WA KAHAWA WILAYANI MBINGA WAISHUKURU SERIKALI MFUMO WA STAKABADHI GHALAN

 

Mwenyekiti wa Chama kikuu cha ushirika wa kahawa wilayani Mbinga(Mbifacu)Philipo Ndunguru kushoto,akiwasikiliza baadhi ya wakulima wanaofanya kazi katika shamba la Chama hicho eneo la Ugano jana.
Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika wa kahawa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma(Mbifacu) Philipo Ndunguru katikati na Kaimu meneja wa chama hicho Faraja Komba kulia,wakimsikiliza Mtangazaji wa kituo cha ITV& Radio One mkoani Ruvuma Emmanuel Msigwa baada ya kutoa taarifa za minada ya zao hiyo inayoendelea kufanyika.

Na Muhidin Amri, Mbinga
WAKULIMA wa zao la kahawa wilayani Mbinga,wameishukuru serikali kuweka mfumo mzuri wa ununuzi wa zao hilo uliosaidia kukomesha vitendo vya wafanyabiashara wanaopita mashambani kununua kahawa kwa bei ndogo isiyolingana na gharama halisi za uzalishaji.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema,hatua ya Serikali kuimarisha mfumo wa ushirika umewawezesha wakulima kupata soko la uhakika na bei nzuri kupitia minada mbalimbali inayofanyika kwa njia ya mtandao(online).

Joshua Martin mkulima wa kahawa wa kijiji cha Luwaita alisema,mfumo huo umewakomboa wakulima hata katika upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwani baadhi yao walilazimika kukopa pembejeo kwa makubaliano ya kulipa kahawa.


“mfumo wa kuuza mazao kupitia vyama vya msingi vya ushirika umetusaidia sana sisi wakulima wadogo kuondokana na unyonyaji,wafanyabiashara walikuwa wanatukopesha pembejeo ambapo mfuko mmoja wa kilo 50 unaouzwa kwa Sh.70,000 mkulima anatakiwa kulipa gunia moja la kahawa lenye ujazo wa kilo 100 ambalo gharama yake ni zaidi ya Sh.300,000 alisema Martin”.

Aidha ameiomba bodi ya kahawa Tanzania(TCB),kuwabana wanunuzi waongeze bei ili wakulima wanufaike na kuhamasika kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa kuwa wanatumia gharama kubwa.

Mkulima mwingine Maria Ndunguru kutoka kijiji cha Kindimba, ameiomba serikali kuendelea kutoa pembejeo za ruzuku kila mwaka ili waweze kuitumia katika uzalishaji wa zao hilo ambalo ni tegemeo kiuchumi kwa wananchi na wilaya ya Mbinga.

Akizungumzia kuhusu bei ya kahawa alisema,kwa ujumla hali siyo nzuri kwa sababu bei imekuwa ikipanda na kushuka hivyo kusababisha baadhi yao kukata tamaa ya kuendelea na kilimo cha zao hilo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Chama kikuu cha Ushirika wa kahawa wilayani Mbinga (Mbifacu) Philipo Ndunguru,amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia suala la ushirika ambao umekuwa na faida nyingi kwa wakulima wa zao hilo.

Alisema,kupitia vyama vya msingi vya ushirika wakulima wengi wamenufaika kwa kupata fedha nyingi na kwa wakati baada ya kuuza kahawa kwa njia ya minada.

Amewaomba wakulima ambao ni wanachama wa vyama ushirika(Amcos), kukataa kurubuniwa na wafanyabiashara wanaokwenda mashambani kwa ajili ya kununua kahawa kwa kutumia vipimo haramu (magoma).

“watu wanaopinga mfumo wa stakabadhi ghalani ni wale wanaokwenda moja kwa moja kwa wakulima kuwashawishi kununua kahawa kwa bei ndogo ambayo hailingani na gharama za uzalishaji”alisema Ndunguru.

Aliongeza kuwa,wafanyabiasahara hao ndiyo wanaonufaika na kazi za wakulima kwa kuwa baada ya kupata kahawa wanakwenda kuuza kwenye minada kwa bei ya juu na kuwaacha wakulima wakiwa maskini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad