HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 31, 2023

WAKAZI WA KIJIJI CHA VIKONGE, TANGANYIKA WAANZA KUPATA MAJI YA BOMBA


Meneja wa Ruwasa wilaya ya Tanganyika Mhandisi Alkam Babuni kushoto,akiwaonyesha wajumbe wa chombo cha watumia maji ngazi ya jamii wa kijiji cha Vikonge mtambo unaotumika kutibu maji kabla ya kwenda kwa wananchi. 

Tenki la kuhifadhi lita 100,000 za maji lililojengwa katika kijiji cha Vikonge wilayai Tanganyika kwa ajili ya kuhudumia wakazi wa kijiji hicho.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Vikonge wilaya ya Tanganyika mkoani Ktavai wakichota maji katika moja ya vituo vya kutoa huduma ya maji vilivyojengwa na wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa).

Na Muhidin Amri, Tanganyika

WAKAZI wa kijiji cha Vikonge wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, kwa mara ya kwanza tangu Uhuru wameanza kupata na kutumia maji ya bomba baada ya wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji hicho.

Meneja wa Ruwasa wilaya ya Tanganyika Alkam Sabuni alisema kuwa,mradi huo unahudumia jumla ya wakazi 8,400 na umegharimu Sh.milioni 608 na umeanza kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.

Sabuni alisema,utekelezaji wa mradi huo umehusisha ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lita 100,000 vituo vya kuchotea maji 31 ambavyo vyote vimekamilika na vinatoa huduma na kujenga miundombinu mingine.


Alieleza kuwa,kupitia mradi huo Ruwasa imeanzisha chombo cha watumia maji ngazi ya jamii (CBWSO) inayofahamika kwa jina la Mpakato ambacho kinahudumia vijiji 11 kati ya hivyo vijiji 9 vinapata maji ya bomba na 2 vinapata maji kupitia visima vya kusukuma kwa mkono.


Aidha alisema,kabla ya kuanzishwa kwa Ruwasa mwaka 2019 hali ya upatikanaji wa maji katika wilaya ya Tanganyika ilikuwa asilimia 65,lakini katika kipindi kifupi cha miaka mitatu cha Ruwasa upatikanaji wa huduma ya maji imefikia asilimia 81.


“kati ya watu laki tatu na sabini na tano wa wilaya ya Tanganyika,zaidi ya watu laki tatu na thelathini wanapata huduma ya maji safi na salama kupitia vituo vya kuchotea maji(DPS) na ndani ya nyumba zao hivyo kutimiza kwa vitendo adhima ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani”alisema Sabuni.


Alisema,wilaya ya Tanganyika yenye jumla ya watu 300,075 ina vijiji 55 na kata ya 16, kati ya vijiji hivyo 39 vimefikiwa na huduma ya maji safi na salama ya bomba.


Pia alisema,kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Ruwasa inaendelea kutekeleza miradi 8 yenye thamani ya Sh.bilioni 7.9 ambayo utekelezaji wake uko katika hatua mbalimbali na baadhi ya miradi hiyo imeanza kutoa huduma kwa wananchi licha ya kutokamilika kwa asilimia 100.


Alisema,ifikapo tarehe 30 Disemba mwaka huu miradi hiyo itakamilika na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya hiyo kutoka asilimia 81 hadi kufikia asilimia 86 hivyo kuvuka lengo la kitaifa la asilimia 85 kwa maeneo ya vijijini.


Katika hatua nyingine Sabuni alisema,kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Ruwasa wilaya ya Tanganyika imepangiwa kutumia Sh.bilioni 4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vinne.


Sabuni alieleza kuwa,vijiji hivyo ni kati ya vijiji 16 ambavyo bado havijafikiwa na mtandao wa maji ya bomba na miradi hiyo itakapokamilika itaongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 86 hadi kufikia asilimia 92 mwaka 2024.


Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Busweru,amemshukuru Rais wa awamu ya sita Dkt Samia Suluhu Hassan kuipatia wilaya hiyo zaidi ya Sh.bilioni 9 ambazo zimetumika kutekeleza miradi ya maji katika vijiji mbalimbali.


Alisema,fedha hizo zimetumika kuimarisha na kuboresha huduma ya maji safi na salama na kuwataka wananchi kuhakikisha wanaunga mkono jitihada za serikali kwa kulinda miundombinu na miradi ya maji inayotekelezwa katika maeneo yao.


Mkazi wa kijiji cha Vikonge Anna Peter,ameipongeza serikali kuwaleta mradi huo ambao umemaliza kabisa changamoto ya huduma ya maji safi na salama.


Alisema,hapo awali hali ya upatikanaji wa maji safi na salama haikuwa nzuri kwani walitumia maji ya visima vilivyochimbwa vya asili vilivyochimbwa tangu enzi za ukoloni,hata hivyo havikutosheleza mahitaji yao kutokana na idadi kubwa ya watu walipo katika kijiji hicho.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad