HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 13, 2023

RC CHALAMILA ATAKA ELIMU YA BIMA KWENDA KWA WANANCHI



* NIC yadhamini Mafunzo ya Mawakala wa Bima , yanena mafanikio katika sekta ya bima

Na Chalila Kibuda, Michuzi TV

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema kuwa elimu ya Bima na faida ya bima watanzania walio wengi hawaelewi hivyo kutaka wadau wa bima kufanya kazi ya kutoa elimu hiyo.

"Kungekuwa na uwekano suala bima lingekuwepo katika wimbo wa Taifa naona watu labda wangepata uelewa na faida zake na kuwa suala jepesi katika kutoa elimu" amesema Mkuu wa Mkoa Chalamila.

Chalamila ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Mafunzo kwa Chama cha Mawakala wa Bima (IAA) ulioandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) kwa kufadhiliwa na NIC Insurance jijini Dar es Salaam.

Ameitaka NIC Insurance kushirikiana na wadau kuhakikisha elimu ya Bima inamfikia kila mtu ili kufikia malengo ya serikali ifikapo 2030 na kuwa asilimia 90 ya watanzania wanakuwa na uelewa kuhusu Bima pamoja na watanzania hao kukata Bima ya maisha.

Amesema NIC inajukumu kubwa la kuhakikisha inahamasisha mawakala wa Bima kutoa elimu kwa jamii na kuhakisha watu wanajiunga katika Bima zao ili kusaidia uelewa mpana wa shughuli za Bima katika maisha ya kila siku.

"NIC Insurance naiagiza kukaa na wadau wake mbalimbali wajadili ili kuhakikisha Bima inakuwa muhimu kwa kila mtanzania aifikilie kama anavyofikilia kula yake ya kila siku" amesema Chalamila.

Ameongeza kuwa semina hiyo inatarajiwa kujadili mpango utakaowezesha kufikia 2030 kila mtanzania anakuwa na uelewa kuhusu Bima lakini pia kumiliki Bima.

Sambamba na hayo Chalamila amewataka TIRA kujikita kwenye kuwezesha mawakala na si kuishia kwenye udhibiti pekee hali ambayo inafanya kampuni hizo kuendelea na utaratibu ambao unafanya zisikuae.

Aidha Chalamila amewapongeza Mawakala wa Bima kwa kupiga hatua kwenye Bima ya Afya na kuwataka wajitahidi kuboresha kwenye Bima za magari.

"Mawakala mkae mjaribu kutathimi na kuweka mikakati ya namna ya kumsaidia mtu alielipa Bima kwa miaka mingi lakini ajawahi kupata na shida ambayo ingemtaka wakala wa Bima kumsaidia hii itasaidia kuongeza idadi ya watu wanaohitaji kujiunga na Bima zenu"amesema Chalamila.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Bima nchini(IAAT)Sayi Daud ameiomba serikali kuondoa tozo mbalimbali ambazo zimekua kikwazo kwa mawakala hao ikiwemo kodi za mabango"

"Ombi letu kwako mkuu wa mkoa tunaomba uzungumze na Halmashauri watuondolee kodi ya mabango lakini pia kodi ya huduma ambayo kimsingi ilitakiwa itolewe na makampuni kutokana na kutouza mali ghafi "amesema Daud

Nae Meneja Ukaguzi TIRA Frank Shangali amesema sekta ya Bima inatoa ajira zaidi ya 2000 zinazozalishwa kwa wanafunzi wanaotoka vyuoni kila mwaka.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Bima za Maisha Hardbert Polepole ambae amemuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa NIC amesema wamekua wakifanya kazi na mawakala kwa miaka 60 sasa na kazi hiyo imekua na tija kwa taifa.

Amesema NIC Insurance imeweza kufikia jamii kupitia mawakala hao hivyo muunganiko wao umekua ni tija na fursa.

"NIC Insurance tunaendelea kufanya kazi na mawakala lakini pia kuongeza mawakala wapya ili kufikia malengo ya serikali kuhakikisha sekta ya Bima inakua"amesema Polepole.

Nae Meneja wa Biashara wa NIC Insurance Kafiti Kafiti amesema NIC Insurance ndio kiongozi katika kampuni za Bima kwani ina zaidi ya mawakala 700 katika Bima za maisha na Bima za ajali na magari.

 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila akizungumza wakati akifungua mafunzo ya Mawakala wa Bima yaliyoandaliwa na TIRA kufadhiliwa na NIC Insurance jijini Dar es Salaam.
 

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Bima Tanzania (IAAT) Sayi Daud akitoa taarifa ya Chama kabla ya mafunzo kwa mawakala wa bima hayajafunguliwa jijini Dar es Salaam.
 

Meneja wa Ukaguzi wa TIRA Frank Shangali akizungumza kuhusiana na usimamizi wa sekta ya bima nchini na uboreshaji wa mifumo ya usajili kwa kampuni za bima nchini , Jijini Dar es Salaam.

 

Baadhi ya matukio katika picha wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa mawakala Bima

 

Picha ya pamoja ya wadau wa Taasisi za Serikali katika mafunzo kwa mawakala wa bima yaliyofadhiliwa na NIC Insurance jijini Dar es Salaam .

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad