HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 19, 2023

NAIBU WAZIRI MWINJUMA KUFUNGUA MAONESHO YA ART & HOME WEEK DAR

 

NAIBU Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma 'Mwana FA' anatarajiwa kufungua maonesho ya sanaa za ubunifu nyumbani Tanzania, maonesho yatakayowahusisha wabunifu mbalimbali wa Sanaa zikihusisha ujenzi, utengenezaji samani na usanifu majengo ambayo yatafanyika kuanzia Agosti 25 hadi 27 mwaka huu katika viwanja vya Warehouse Masaki jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam mmoja ya wakurugenzi wa kampuni ya Art & Home na waandaaji wa wiki ya Art & Home Ameniel Lukumay amesema, maonesho hayo yatawakutanisha pamoja wabunifu wa masuala ya nyumbani ambayo pia ni fursa kwa watanzania kupendezesha nyumba zao kupitia wabunifu hao wazawa.

"Kuna wabunifu wengi wapo mtaani, wanafanya kazi nzuri lakini ni ngumu kuwapata, Art & Home tunawakutanisha wabunifu hawa na walaji ni wiki ya ubunifu na kupendezesha nyumba kwa samani, kuziba nyufa na nakshi mbalimbali zinazotokana na wabunifu wa hapa nyumbani..... watakuwepo wajenzi, wataalam wa landscaping, interior and exterior designers." Amesema.

Amesema, Sanaa ya ufundi inaonekana kusahaulika na wakaona kupitia wiki ya Art & Home ni vyema kuwakutanisha wanasanaa ya ufundi na walaji pamoja na kuwa na wiki ya kuzingatia masuala ya nyumbani ikiwemo kupanda miti, maua na kubadilisha samani.

Pia Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA,) Adrian Nyangamalle amesema, zaidi ya watanzania milioni nne wanajihusisha na sanaa za ufundi ambayo pia inachangia pato la Taifa pamoja na kutoa ajira.

"Changamoto zinazoikabili sekta hii ni soko, uwepo wa wiki ya Art & Home utasaidia sana wabunifu kupata masoko na kubadilishana uzoefu...pia wananchi watapata fursa ya kuona na kupata bidhaa zenye viwango kutoka kwa wabunifu wa hapa nyumbani." Amesema.

Aidha amewahimiza watanzania kupenda bidhaa zinazozalishwa nyumbani na kuwataka wabunifu kutumia fursa hiyo kwa kujitokeza kwa wingi na kuonesha bunifu zao.

" Maonesho haya yatazinduliwa tarehe 25 mwezi huu ambayo ni siku ya sanaa duniani, mabanda yapatayo 100 yaliyoandaliwa yajae na nitoe wito kwa kampuni mbalimbali zijitokeze kudhamini maonesho haya ambayo yamelenga kukuza na kutangaza bunifu za sanaa ya ufundi hapa nchini." Ameeleza.

Aidha Msemaji na Mhamasishaji wa maonesho hayo Japhet Ole amesema, wabunifu mbalimbali wakiwemo wasanifu majengo na wajenzi watakutana pamoja walaji pamoja na wabunifu hao kukutana kubadilishana ujuzi na uzoefu.

Aidha amesema, viongozi na wadau mbalimbali wa fani hiyo watashiriki maonesho hayo na kujadili namna ya kuiendeleza zaidi Sanaa ya ufundi.

Kwa upande wake Meneja mauzo wa Art & Home Week Doris Lyimo amesema kuwa maonesho hayo hayana kiingilio na wabunifu wakiwemo wajenzi na wasanifu majengo wataonesha bidhaa zao na kuwahimiza kuendelea kupata mabanda ya maonesho kupitia 0717664472.

Bi. Doris amesema washiriki wote wa maonesho hayo watapata vyeti vya ushiriki pamoja na tuzo kwa bunifu na waoneshaji bora katika maonesho hayo ambayo washiriki kutoka Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar watashiriki huku mpango wa kushirikisha nchi nyingine katika maonesho ya mwaka ujao ukielezwa.

Msemaji na Mhamasishaji wa maonesho hayo Japhet Ole (kushoto,) akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maonesho hayo na kueleza kuwa viongozi mbalimbali na watu mashuhuri watashiriki maonesho hayo. Leo jijini Dar es Salaam.

Mmoja ya Wakurugenzi wa Kampuni na waandaaji wa wiki ya Art & Home Ameniel Lukumay (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mkutano huo na kueleza kuwa maonesho hayo yatawakutanisha wabunifu hao pamoja na walaji na kuwa na wiki ya kuzingatia masuala ya ubunifu wa nyumbani, Leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja wa bidhaa wa kampuni hiyo na anayefuatia ni Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA,)Adrian Nyangamalle. Leo jijini Dar es Salaam.

Meneja mauzo wa kampuni ya Art & Home Bi. Doris Lyimo (kushoto,) akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maonesho hayo na kutoa mwito kwa kampuni mbalimbali kujitokeza na kudhamini maonesho hayo. Leo jijini Dar es Salaam.

 Mkutano ukiendelea.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad