HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 19, 2023

LATRA YAONGEZA MAPATO MARADUFU , YAFIKIA ZAIDI YA ASILIMIA 32

Na Humphrey Shao,Michuzi Tv

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imefanikiwa kuongeza mapato kwa asilimia 32 katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hayo yamebainishwa na CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa (LATRA) leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari akitoa taarifa ya mafanikio ya mamlaka ya udhibiti usafiri ardhini (LATRA) kwa mwaka wa fedha 2022/2023

Amesema Mapato ya Mamlaka yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2021/22, mapato ya Mamlaka yaliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 25.945 hadi Shilingi Bilioni 28.53 ikiwa ni ongezeko la Shilingi Bilioni 2.58 sawa na ongezeko la 10%.

“Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 hadi 2022/23, mapato ya Mamlaka yaliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 28.53 hadi Shilingi Bilioni 34.17 (kabla ya kukaguliwa na CAG) ikiwa ni ongezeko la Shilingi Bilioni 5.64 sawa na ongezeko la 20%.

“Kwa jumla, katika kipindi cha miaka mitatu (3) ya utekelezaji wa majukumu ya LATRA, mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2022/23, mapato ya Mamlaka yaliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 25.95 hadi Shilingi Bilioni 34.17 (kabla ya kukaguliwa na CAG) ikiwa ni ongezeko la Shilingi Bilioni 8.22 sawa na ongezeko la 32%.

“Mapato yatokanayo na adhabu yamepungua na mapato yatokanayo na leseni kujenga tabia ya utii wa Sheria na kupunguza adhabu kwa watoa huduma za usafiri ardhini nchini.”amesema.

CPA Habibu Suluo, amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeiwezesha LATRA kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi na hivyo imeipa mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Nitumie fursa hii kutoa Pongezi za dhati kwa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa Uongozi wake Mahiri wenye mafanikio makubwa katika Awamu hii ya Sita.

“Kwa uchache niseme Uongozi wa Mhe. Rais katika Awamu hii, umetujengea mazingira mazuri na bora ya kusimamia sekta hii katika eneo letu la Udhibiti Usafiri Ardhini. Haya yamekuwa yakifanyika kwa ufanisi kutokana na Uongozi mahiri na madhubuti wa wasaidizi wake, ambapo hivi karibuni Mhe. Rais ameunda Wizara mpya ya Uchukuzi na kuwateua Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), kuwa Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb), kuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Godius W. Kahyarara, kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi pamoja na Mhe. Dkt. Ally Posi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi.” Amesema.

Aidha, CPA Suluo amesema kuwa, katika usafiri wa barabara, kwa kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2022/23, idadi ya leseni za usafirishaji iliongezeka kutoka leseni 230,253 hadi leseni 284,158 ikiwa ni sawa na ongezeko la leseni 44,205 ambayo ni ongezeko la asilimia 18.4.

“kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1) ( b) cha Sheria ya LATRA, Mamlaka inao wajibu wa kutoa, kuhuisha, kusitisha na kufuta leseni za usafirishaji, hivyo Mamlaka hutoa leseni kila mwaka kwa vyombo vya usafiri kibiashara. Leseni hizi hutolewa baada ya mtoa huduma kukidhi masharti yanayotakiwa kwa aina ya huduma husika. Leseni hizi hutumika kutambua idadi ya watoa huduma wanaodhibitiwa,” ameeleza CPA Suluo.

Vilevile amesema kuwa, Mamlaka ina jukumu la kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa vyombo vinavyodhibitiwa kwa lengo la kupata madereva wenye sifa na weledi kuendesha magari yanayotoa huduma kwa usafiri wa umma kwa kupima umahiri wao hasa maarifa waliyopata ili kuimarisha usalama.

“Hadi, kufikia Septemba 30, 2023, madereva 17,990 wamesajiliwa na kuingiza taarifa zao kwenye kanzidata ya Mamlaka ambapo madereva 1,617 wamethibitishwa baada ya kufaulu mtihani wa kuthibitishwa na LATRA. Miongoni mwa madereva hawa madereva wa mabasi wapatao 645 wamesajiliwa kwenye mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi (VTS) na kupatiwa kitufe maalumu cha utambulisho (identification button, i-button). Matumizi ya kitufe hicho ni kurahisisha utambuzi wa dereva anayeendesha gari kwa wakati husika kupitia mfumo wa VTS.”

Katika Usafiri wa Reli, CPA Suluo ameeleza kuwa Mamlaka, imeendelea kutoa mafunzo kazini kila mwaka kwa Wafanyakazi Muhimu wa Usalama katika uendeshaji wa reli (Safety Critical Workers) kwa TAZARA na TRC ili kuwaongezea ujuzi wa kutimiza majukumu yao kwa weledi na kwa mwaka wa fedha 2023/2024 LATRA imepanga kuhakikisha usalama wa abiria na mizigo unazingatiwa katika usafiri wa reli.

“Mafunzo ya aina hii husaidia kuwajengea uwezo wafanyakazi hao muhimu kuzuia ajali zitokanazo na makosa ya kibinadamu (Human Errors). Tathmini inaonesha kwamba, makosa ya kibinadamu katika uendeshaji wa shughuli za reli huchangia zaidi ya asilimia ya 85% ya ajali zote za treni kwa TRC na TAZARA. Hivyo, mafunzo hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali zinazosababishwa na makosa ya kibinadamu,” amefafanua CPA Suluo.

Aidha, CPA Suluo ameeleza kuwa, LATRA imepiga hatua kubwa katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo Mamlaka inatumia mifumo mbalimbali ikiwemo Mfumo wa Usimamizi wa Shughuli za Kiudhibiti (RRIMS), Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), Mfumo wa Tiketi Mtandao, Mfumo Tumizi wa LATRA (LATRA App), Mfumo wa e-Mrejesho pamoja na Mfumo wa Taifa wa Ununuzi wa Umma wa Kieletroni (NeST).

“RRIMS imeunganishwa na mifumo ya taasisi nyingine za Serikali kama vile TRA, TIRA, NIDA, GePG na BRELA na pia imeunganishwa na mifumo ya wadau wengine kama vile watoa huduma wa tiketi mtandao ili kurahisisha utoaji huduma za Mamlaka kwa wananchi.”

Vilevile amesema LATRA imeanza kutumia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) tangu mwaka 2017 na hadi sasa, zaidi ya magari 9,420 yameunganishwa na mfumo huu ambapo, magari 7,620 yapo hai na yaendelea kutoa taarifa kupitia mfumo huu. “Mfumo umesaidia Kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani zinazotokana na mwendokasi, umepunguza madhara ya ajali zinazotokana na mwendokasi na umerahisisha uchunguzi wa ajali pale zinapotokea.”

Ameelezea mifumo mingine ni Mfumo wa Tiketi Mtandao ambao umesaidia kudhibiti upandishaji holela wa nauli. Mfumo Tumizi wa LATRA (LATRA App) unaopatikana ‘Play Store’ kwenye simu zote za Android na unamwezesha mwananchi kupata taarifa za nauli za mabasi ya masafa marefu na mabasi ya mijini na Mamlaka inaendelea kuboresha huduma za mfumo huo ili kuwezesha abiria kutambua mwendo kasi wa gari.
 

Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA), CPA Habibu Suluo, akitoa taarifa ya mafanikio ya Mamlaka hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 jijini Dar es Salaam leo Oktoba 19, 2023, ikiwa ni muendelezo wa mikutano ya taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina.
 

Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara LATRA, Johansen Kahatano, akizungumza katika mkutano huo.
 

Kaimu Mkurugenzi Udhibiti Uchumi Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini, Fahamueli Mkeni.
 

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA, Salum Pazzy
 

Kaimu Mkurugenzi Usafiri wa Reli, Mhandisi Hanya Mbawala.
 

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Neville Meena, akitoa neno la shukrani wakati wa mkutano na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA) na Wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 19, 2023. Mkutano huo umeratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad