HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 27, 2023

KAMPUNI YA ORYX GAS YATOA MITUNGI 600 PAMOJA NA MAJIKO YAKE KWA WANAWAKE WILANI KASULU

Na Mwandishi Wetu,  Kasulu.

KATIKA kuunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia Kampuni ya Oryx Gas imeendeleza jitihada hizo kwa kugawa bure mitungi ya gesi 600 yakiwa na majiko yake kwa vikundi mbalimbali vya wanawake wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Mitungi hiyo imekabidhiwa ushirikiano wa  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu)Profesa Joyce Ndalichako huku kampuni ya Oryx ikisisitiza malengo yao ni dhahiri kuona mabadiliko makubwa katika matumizi ya nishati safi na salama kwa ajili ya kupikia kwa jamii zote za Watanzania.

Akizungumza mbele ya vikundi vya wanawake wa Wilaya ya Kasulu wakati wa kukabidhi mitungi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas Tanzania Araman Bonoite  amesema kampuni yao inafahamu kundi hilo la akina mama ambao kila siku wanahudumia chakula cha Watanzania wengi, wameathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi ya kuni na mkaa hivyo, kampuni ya Oryx Gas kwa kushirikiana na Waziri Ndalichako wameamua kuiunga mkono jumuiya hii ikiwa ni hamasa kwa wengine.

"Mikoa ya Kigoma na mikoa jirani imeharibiwa kwa kiasi kikubwa na ukataji miti kwa ajili ya matumizi ya nishati ya kupikia chakula, hivyo jitihada kubwa zinahitajika ili kulinda afya na kuokoa mazingira ya mkoa huu na maeneo mengine nchini, amesema.

Amefafanua kwamba  Oryx Gasi inawekeza katika siku zijazo kwa kutekeleza mipango ya kukabiliana na kaboni kupitia elimu ya upishi safi, uchangiaji wa vifaa vya kuanzisha LPG bila malipo kwa baadhi ya mikoa, uhamasishaji wa matumizi ya gesi ya kupikia majumbani  kupitia uuzaji mkubwa wa mitungi ya gesi kwa bei nafuu, mafunzo kwa wingi kwa matumizi salama ya LPG na kadhalika.

" Juhudi hizi zinalenga kuhakikisha Watanzania walio wengi wanapitisha hatua kwa hatua suluhisho la nishati safi ya kupikia kama ilivyoagizwa na Mheshimiwa rais Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Na mipango ya kampuni yetu katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia inakwenda sambamba na mipango ya Serikali."

Benoite amesema kwamba Rais Dk.Samia ameweka lengo la Watanzania kutumia nishati safi, ikiwa ni pamoja na LPG, kuwa angalau asilimia 80 ya watu wote ifikapo mwaka 2032. Kampuni ya Oryx Gas Tanzania inajivunia kuunga mkono maono yake katika kutoa nishati safi ya kupikia kwa Watanzania wengi.

Kwa upande wa Waziri wa  Nchi , Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini ameishuku kampuni ya Oryx Gas kushirikiana naye kugawa mitungi ya gesi kwa akinana mama hao kwani sasa wataachana na kutumia kuni na mkaa na kuanza kupika kwa nishati safi lengo likiwa kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapewa kipaumbele.

"Kugawa mitungi hii kwa wananchi wetu ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono juhudi za Rais Dk .Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akihamasisha utunzaji wa mazingira kwa kutoharibu misitu yetu kwa kukata miti kwa ajili ya kupata kuni na mkaa.Hivyo niendelee kuwaomba wananchi tutunze mazingira."

Amefafanua matumizi ya kuni na mkaa yamekuwa na athari kubwa za kiafya hivyo ni vema wananchi wakatumia nishati safi ya kupikia ili kuhakikisha afya za wananchi zinakuwa salamba.

Aidha ametoa ombi kwa Oryx Gas kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya nishati ya gesi ya kupikia ili kuhakikisha wananchi wanakuwa salama wakati wote huku akiendelea kuwaomba wananchi wa Kasulu kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutunza na kuhifadhi mazingira.
 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad